..RIWAYA: HATIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA ISHIRINI NA - TopicsExpress



          

..RIWAYA: HATIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA Adrian alikubali na kukata simu, akasimama na kuongoza mwili wake bafuni, akaoga kisha akajiandaa akaelekea Makoroboi kwa usafiri wa daladala. Mida ya mchana akafika rafiki yake wa shule ya msingi aliyeitwa Mark ambaye aliacha shule kitambo na kujiingiza katika vitendo vya kihuni. Alikuwa ameambatana na mwenzake. Adrian alitoa maelekezo yote, akaeleweka, kisha akawatajia jina la muhusika kuwa ni John Mapulu. “Nahitaji apigwe na apewe onyo la kuachana na mke wake!!” “Laki tano unusu!!” alitaja bei Adrian akakubaliana nayo akatanguliza nusu. Akawa ameingia rasmi katika vita ya kumgombea Matha!!!! Msichana aliyeamini kuwa aliumbwa kwa ajili yake. **** Baada ya siku mbili Adrian alipigiwa simu na Mark kuwa mambo yanakaribia kuiva hivyo wanatakiwa kukutana kwa ajili ya makubaliano ya mwisho baada ya utafiti. Adrian alijiona mshindi katika vita hii, akaacha shughuli zake na kufuata maelekezo, kiherehere cha kuona John anaaibika kilimsumbua. Akaamini kuwa kudhalilika kwa John kutapooza machungu yake yote ya miaka kadhaa nyuma na pia utakuwa ni mwanzo wa safari mnpya ya kummiliki Matha jumlajumla. Walikutana maeneo ya Nata, Adrian akaelezwa kwamba alitakiwa akutane na Nunda mwenyewe ili aweke kiapo cha siri. Adrian hakusita akakubali, hamu yake ilikuwa kumuona Matha akiwa huru ili aweze kumtambulisha kwa wazazi wake badala ya Monica. Hivyo alikuwa tayari kwa lolote jambo. Walipanda daladala zinazoelekea Nyakato Sokoni ndani ya jiji la Mwanza, kila abiria alikuwa ametingwa na jambo lake, waliofahamiana walijikita katika kupiga soga hapa na pale, wapenzi waliegemeana wajuavyo, wengine walijikita katika kusoma magazeti. Adrian akiwa mmoja kati ya abiria wengi ambao walikuwa kimya tu wakingoja mwisho wa safari yao. Hali hii ya kila mtu kujikita katika namna apendayo ilileta amani ndani ya gari, na ilidumu kwa muda mrefu hadi pale abiria mmoja alipobadilisha hali ya hewa. Kwanza alianza kwa kuwasukuma abiria wenzake waliokosa nafasi za kukaa, walimshutum,u lakini hakuonekana kujali!! Hili wakalipuuzia. Mara akaanza kuongea mwenyewe huku akijipekua kwa jitihada zote. Hili nalo watu wakalitathmini kama kuvurugwa asubuhi asubuhi. Tatu, akaanza kukaba watu waliomzunguka!! Hili halikuvumilika, akkaripiwa. Naam!! Akapata nafasi ya kujibu mashambulizi, yule mama nadhifu akageuka mbogo, akadai kuna simu yake ameibiwa ndani ya ile daladala. Sauti yake ikawa juu sana kuliko sauti za watu wengine, akamsihi dereva asimamishe gari!!!. Alikuwa ni mwanamama aliyekuwa na heshima zake kabisa kila mtu alimuamini kimtazamo, na jambo la kushtua zaidi ni pale walipojaribu kuipiga namba yake ikaita mara moja na kisha simu ikazimwa. Kila mmoja akawa upande wa yule mama, wakaamua kumuunga mkono juu ya kitu alichofanyiwa!! “Sikubali mimi simu ya mume wangu jamani halafu mwizi yupo hapa hapa ndani sikubaliiiiii….” Alilia kwa uchungu yule mama kila mmoja akawa anamuonea huruma. “Dereva ingiza gari kituoni huu ushakuwa ujinga sasa!!! Mnawachekea sana na mnawajua” abiria mmoja aliyekuwa kimya muda mrefu alitoa tamko hilo, akaungwa mkono na wengi, taratibu daladala ikakata kushoto ikaingia kituo cha polisi maeneo ya mabatini kondakta akiwa makini kabisa na abiria wake, hakuna aliyeruhusiwa kushuka wala kutupa kitu chochote nje!!. Abiria wasiokuwa na hatia walilalamika sana kupotezewa muda lakini je utajuaje huyu ana hatia na huyu yu salama?. Gari lilipofika pale alishuka dereva peke yake, akaenda mapokezi na kutoa shtaka hilo, askari wawili wa kiume na watatu wa kike walipewa jukumu hilo la kukagua kila mmoja ili simu iweze kupatikana. Mark hakuwa na wasiwasi alikuwa akizungumza na Adrian kwa sauti za kunong’oneza, wote walikuwa na furaha. Wakimtabiria mabaya sana huyo mtu ambaye atakuwa ameiba simu ile!! Askari aliamuru abiria wote kutelemka, likaanza kusachiwa gari, hakikupatikana kitu, baadaye abiria mmoja baada ya mwingine, wasichana kwa askari wa kike na wanaume kwa askari wa kiume. Zoezi halikuwa gumu sana kwani wengi wao hawakuwa na vifurushi. Na waliokuwa na vifurushi hawakuwa na dalili ya kuwa wezi wa hiyo simu, ndio hivyo alivyochukuliwa Adrian, kati ya abiria waliokuwa nadhifu basi alikuwa ameongoza. Kuanzia juu mpaka chini alikuwa anashawishi macho kumtazama. Kifurushi chake kidogo kilipekuliwa kwa wepesi sana katika naqmna ya kutimiza wajibu, askari alijiaminisha kabisa kuwa hakuna utata kwa bwana huyu. Lakini ghafla mambo yakabadilika tena, askari hakuamini alichokiona, yeye pamoja na mwenzake wakajikuta wakihamaki, kutoka katika begi dogo la Adrian tofauti na uwepo wa pesa kulikuwa na risasi nne. Adrian hakuwa akiifahamu risasi ilivyo hivyo alibaki kutabasamu tu, harakaharaka akashangaa amerukiwa na askari mmoja akamnasa vibao halafu akamtia pingu mikono ikiwa kwa nyuma. Abiria waliruhusiwa kuondoka. Simu ilikuwa haijaonekana. Mark kama vile hamjui Adrian na yeye alitoweka!! Alitoweka huku akitetemneka, alijiuliza maswali lukuki kichwani mwake. Akamchukulia Adrian kama mtu hatari sana. Yaani anamiliki bunduki? Ina maana jamaa alitaka kumuua Nunda ama vipi, au angeniua na mimi?.... Mark alijiuliza huku akiusikia mwili wake ukiwa katika mtetemo!! Hali haikuwa shwari!! Mark katika hofu, Adrian matatani!!! Adrian aliingizwa katika chumba cha mahabusu akiwa haelewi nini kinachoendelea, safari yake aliyotegemea ya kwenda kumkomoa John Mapulu sasa ilikuwa imemgeukia yeye. Wasiwasi ukamtawala, ilikuwa mara yake ya pili kuingia katika mahabusu tena mara ya kwanza ilikuwa utotoni ambapo walikamatwa siku ya mkesha wa sikukuu ya krismasi wakiwa wanazurura. Hapo ilikuwa baada ya kuwa wametoroka kanisani. Asubuhi waliruhusiwa kurejea makwao. Hapakuwa na kesi na wala hawakupigwa makofi kama aliyokumbana nayo hapa. Wasiwasi ukazidi nguvu ushujaa wake, akafadhaika!!! Baadaye sana aliruhusiwa kupiga simu nyumbani kwao. Mzee Mhina akaipokea, akapewa taarifa, kama kawaida akawa mbinafsi hakumshirikisha mke wake japo alipaliwa na mate baada ya kupewa taarifa hiyo. Hakuyapenda mambo ya polisi kwani aliutambua usumbufu uliopo kule. Hakutaka kuendesha gari yake binafsi bali alipanda taksi hadi akafika pale kituoni. “Bunduki ya mwanao ipo wapi” askari mpelelezi wa kesi hiyo alimuuliza mzee Mhina wakati akijiweka sawa katika kiti kilichokuwa katika moja ya ofisi. “Bunduki!!! Bunduki gani” alihoji huku akishindwa kukaa vyema, alikuwa amekumbwa na mshawasha. Askari hakujibu lolote aliendelea kupeleleza mafaili yake huku na huko, na kupiga mluzi ambao haukuwa wa nyimbo yoyote ile bila shaka alikuwa ameutunga ghafla ili kumburudisha Mhina. “Kwani mwanangu amekamatwa kwa kosa gani??” “Jambazi!!” “Jambazi nani Adrian??” alihamaki. Askari hakujibu akakaa na faili mkononi akamkazia macho mzee Mhina kisha akajilazimisha kutabasamu. “Jambazi mwanao ilete hiyo bunduki tumalizane!!” alirudia maelezo yale askari huyu ambae alijulikana kwa jina la Moa. Baada ya kuhamaki sana na kulalamika kuwa hatendewi haki zake za msingi kama mzazi wa mtuhumiwa, Moa alisarenda akamueleza kinagaubaga kila kitu kilivyokuwa na baadaye akaitwa Adrian. Alikuwa peku peku, suruali kiunoni ilipakataa na shingo yake ilikuwa imerefuka, kwa masaa kadhaa Adrian alikuwa amekonda!! Hakukumbuka kumsalimia baba yake kutokana na hali iliyokuwepo. Aliamriwa kukaa chini kisha akaanza kuulizwa maswali akajieleza kila kitu kilivyokuwa huku akimtaja mara kwa mara Mark!! Lakini hakuisema njama aliyokuwanayo yeye na Mark dhidi ya John Mapulu!! Baada ya maelezo kuandikwa alirudishwa rumande dhamana ilikuwa haijatimia kimasharti. Kwa siku nyingine akawa amelazwa tena mahabusu. Siku iliyofuata ilikuwa jumamosi, mpelelezi wa kesi alikuwa na udhuru hakuja kazini, na siku ya jumapili si kawaida yake kuja kazini. Adrian akawa amesalia ndani ya kachumba kadogo ka mahabusu hadi siku ya jumatatu ambapo dhamana ilipitishwa akawa huru. Hewa ya uhuru iliyeyusha hofu aliyokuwanayo, japokuwa alinuka sana hakujali alifurahia kuwa huru. “Usimweleze mama yako chochote!!!” baba alimwambia mwana, lilikuwa neno la kwanza tangu awe huru!!! Adrian alijibu kwa kutikisa kichwa juu na chini mara kadhaa. Macho yake yalikuwa yamevimba bila shaka alipigwa kidogo na wakorofi wa jela aliowakuta pale mahabusu. Mzee Mhina akawasha gari wakaelekea nyumbani kwa Adrian. Baada ya kuoga na kupata chai nzito ya maziwa hatimaye kilikuwa kikao cha dharula. Baba na mwana!! Adrian alimueleza baba yake kila kilichotokea lakini hakutaka kuonekana mjinga mbele ya baba yake huyo aliyemuamini sana. Hakudiriki kumtaja John wala Matha katika mlolongo wa maelezo yake. “Una uhakika kuwa hujui lolote kuhusu zile risasi” “Nikwambie mara ngapi baba??” alihamanika Adrian, mzee Mhina akashusha pumzi kwa nguvu zote kisha akajiegemeza kichwa chake katika sofa. “Nitamalizana na yule mpelelezi japo anahitaji pesa ndefu sana kinyume na hapo ni mahakamani kisha hukumu kwenda jela” Adrian akapaliwa na chai aliyokuwa anaifurahia ladha yake mdomoni!!! Alikohoa sana kabla ya kukaa sawa. “Baba mpe hizo pesa mambo ya mahakamani tena aah!!” alilalamika Adrian. Mzee Mhina hakujibu kitu akawa ameaga na kuondoka!! Adrian hakuendelea tena kunywa chai, akaingia chumbani akajifungia na kuanza kumlaani Mark kwa kitendo cha kinyama alichokuwa amemfanyia. Ina maana alitaka nikafie huko huyu jamaa!!! Alijiuliza huku akikifinyafinya kitanda chake kwa kutumia makucha yake yasiyokuwa na urefu wa kutisha. Alilaani kwa kila namna na mwishowe fikra za ajabu ajabu zikaanza kumvaa akamwona Mark kama mnyama tena mnyama wa kutisha aliyefanya mbinu ili ammeze bila taarifa, mnyama asiyekuwa wa kufugwa, alimfikiria amfananishe na simba akagundua ni yeye alikuwa akiitwa simba na baba yake. Akaona jina lake haliwezi kufanana wala kutumiwa na mtu mwe roho mbaya na muuaji kama Mark. Mwishowe akaamua kumfananisha na JITU. Jitu lisilokuwa na utu, jitu ambalo linaipoteza amani kama ukilichekea lakini mwisho wa jitu ni kutumia makali ya upanga. Adrian akawa amejawa na fikra za kumteketeza Mark ambaye alikuwa amepewa jina la JITU. Wakati huo Matha alikuwa amesahaulika kidogo na John hakuwa kwenye fikra zake. Hakujua kama Mark naye anamlaani huko alipo!!! ***** MAJI ukiyakamia sana mwisho utashindwa kuyaoga. N’do hiki kimemtokea ADRIAN ***ADRIAN matatani akiwa hajafanikiwa kumkomesha MAPULU..... Sasa yu katika hatia ya kukutwa na risasi na kudaiwa kuwa anayo bunduki...... ITAENDELEA KESHO SAA SITA KAMILI MCHANA!!!
Posted on: Tue, 27 Aug 2013 09:00:01 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015