HOTUBA YA UFUNGUZI WA MJADALA WA BIASHARA HARAMU YA WANYAMAPORI - TopicsExpress



          

HOTUBA YA UFUNGUZI WA MJADALA WA BIASHARA HARAMU YA WANYAMAPORI KAMA ULIVYOANDALIWA NA MANET (Mazingira Network Tanzania) MR HOTEL, IRINGA. Ndugu wageni waalikwa, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kunipa nafasi ya kushirikiana nanyi leo hii hapa kama mmoja wa wadau muhimu katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori. Kwa muda mrefu nimekua mstari wa mbele katika vita dhidi biashara haramu ya wanyamapori si kwa kua nina maslahi binafsi na sekta hii, bali kwa kuwa nina dhamana hiyo kama mtanzania yeyote yule na kwa kuwa ni moja ya wajibu wa kila mtanzania kama ambavyo katiba ya nchi yetu inavyotuongoza. Ibara ya 27(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba “Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine”, Pia katika ibara hiyohiyo ya 27 (2) inasema kwamba “Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao”, Ni dhahiri matakwa haya ya kikatiba hayatenganishi utu wa mtu kwa mujibu wa kikatiba ndani ya nchi katika nafasi zake kimamlaka katika usimamizi wa rasilimali za taifa. Ndugu wageni waalikwa,napenda kutambua mchango wa MANET pia kama wadau muhimu hasa katika kuhakikisha kuwa mazingira ya taifa letu hususani katika sekta za misitu, uvuvi na wanyamapori vinalindwa si tu kwa matumizi ya leo bali kwa ajili ya vizazi vijavyo. Zaidi natambua mchango wa MANET kama shirika ambalo lipo mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa jamii inakua mstari wa mbele kupiga vita rushwa hasa kwa kushirikiana na wananchi pamoja na mamlaka za serikali za mitaa. Ni jambo la kujivunia kuwa mzawa wa nchi ambayo imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi huku tukiwa tumejaliwa maliasili na vivutio vya kutosha Duniani. Lakini ni jambo pia la kusikitisha, kuona kuwa tupo katika taifa ambalo sasa lipo katika ramani ya dunia kwa kushindwa kusimamia, kudhibiti na hata kutunza rasilimali hizo hasa wanyamapori ambao ndio moja ya utambulisho wa Taifa letu duniani. Takwimu mbalimbali zimeendelea kuishtua dunia juu ya kasi ya vitendo hivi vya biashara haramu hasa kwa nchi ambayo watu wake wanasifika kwa ukarimu na amani. Ndugu wageni waalikwa, suala la biashara haramu ya wanyamapori nchini limeendelea kukua kwa kasi ya ajabu huku Serikali ikionesha wazi kushindwa kudhibiti suala hili na hivyo kutoa mwanya kwa majangili kuendelea kuteketeza wanyamapori huku baadhi ya viumbe hai vikiwa hatarini kutoweka kabisa katika ramani ya Taifa letu. Watanzania wenzangu, ni masikitiko makubwa kuona kuwa mkutano mkuu wa wanachama wa Mkataba wa Biashara wa Viumbe walio hatarini (The Convention on Trade in Endangered Species - CITES) uliofanyika Bangkok, mwaka huu Tanzania na Kenya zilitajwa kati ya nchi nane duniani, ambazo zinaongoza kwa biashara haramu ya wanyamapori na hivyo mkutano ule ulipendekeza kuwa nchi hizi lazima ziwekewe vikwazo vya biashara. Swali la msingi la kujiuliza , ni kwa nini kama Taifa tufikie mahali ambapo tunaweza kuwekewa vikwazo vya biashara kwa kushindwa kutekeleza wajibu wetu na kulinda maslahi ya watu wachache? Ukiangalia takwimu mbalimbali nchini na za kimataifa, Taifa letu limeendelea kuwa katika ramani ya dunia kwa kuwa moja ya nchi vinara zinazotia doa hasa kwa biashara haramu ya wanyamapori, hali inayohatarisha maisha ya baadhi ya viumbe hai. Mara kadhaa tumesikia viongozi wa Serikali wenye dhamana wakisema kuwa mtandao wa majangili na wafanyabiashara haramu wa wanyamapori ni mpana na mgumu kuumaliza. Mara kadhaa pia Serikali imeendelea kukiri kuwa mtandao huu unawahusisha Wafanyabiashara wakubwa, Wanausalama, Wabunge, Wanasiasa na watu wenye dhamana ya uongozi katika taifa letu. Serikali imeendelea kutoa matamko kuwa itawataja wahusika wa biashara haramu dhidi ya wanyamapori na kuwachukulia hatua lakini cha kushangaza, mara zote hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Jambo moja la msingi ambalo ningependa kulizungumza na kusisitiza hapa leo ni juu ya wajibu wa kila Mtanzania katika kuhakikisha kuwa tunaungana kwa pamoja katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika tamko lake maarufu mwaka 1961 lijulikanalo kama Arusha Manifesto alisema yafuatayo “Uhai wa wanyamapori ni jambo muhimu na linalotuhusu sana sisi sote barani Afrika. Viumbe hawa wa porini, wakiwa katika mapori wanamoishi,sio muhimu tu kwa ajili ya kuajabiwa na kuvutia lakini pia ni sehemu ya maliasili yetu na pia ndio mustakabali wa maisha yetu ya baadaye”. Mwalimu Nyerere alitambua umuhimu wa kutunza wanyamapori kwa wakati huo tukiwa na hazina kubwa ya wanyama, lakini leo viongozi wa Serikali wameshikwa na kigugumizi katika kuhakikisha dira na jitihada za baba wa taifa letu ,vinatimizwa. Kama kiongozi ambaye wananchi wamenipa dhamana ya kuwawakilisha, nawiwa kutumia nafasi hiyo, kuendeleza juhudi zangu na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anakua mdau nambari moja wa kupinga biashara haramu ya wanyamapori kwani si tu kuwa inalitia hasara taifa letu bali pia inaweka hatarini maisha ya wanyamapori kwa vizazi vijavyo. Nachukua nafasi hii kuikumbusha na kuitaka Serikali kutimiza wajibu wake kwa kuwafikisha majangili na wafanyabiashara haramu wa wanyamapori katika vyombo vya dola na watendewe ipasavyo kwa mujibu wa Sheria. Ndugu wageni waalikwa, pamoja na kuisisitiza Serikali kutimiza wajibu wake wa kudhibiti biashara haramu ya wanyamapori ni lazima pia mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kuongeza juhudi zao kuhakikisha kuwa elimu kwa umma inatolewa ili kuongeza nguvu ya pamoja katika masuala ya kulinda wanyamapori. Binafsi, napenda kuchukua nafasi hii kuupongeza uongozi wa MANET kwa kuwa mdau muhimu katika kuhamasisha umma na jamii ya kitanzania katika utunzaji wa mazingira na pia katika kutoa mchango wake mkubwa dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori hasa kwa kupitia fursa mbalimbali kama hizi. Nawashukuru sana MANET kwa kutambua mchango wangu katika suala hili na kwa kunipa fursa ya kuzungumza machache juu ya "Biashara haramu ya wanyamapori". Napenda pia kuwapongeza MANET kwa kuandaa mjadala huu wa Vita dhidi ya biashara ya wanyamapori ambao umewashirikisha wadau mbalimbali. Katika majadiliano mbalimbali yatakayofanyika leo, ningependa kuona mjadala huu si tu utatoa changamoto bali pia utatupa njia mbadala na bora za kuweza kukabiliana na biashara ya wanyamapori ikiwemo kutoa maazimo ya nini kifanyike ili kutatua suala hili pale mjadala utakapokamilika. Napenda tena kuchukua nafasi hii, kuwashukuru kwa heshima mliyonipa kama mgeni rasmi, na nawatakia majadiliano mema yatakayoleta majibu sahihi. Kwa idhini mliyonipa natangaza rasmi kuwa, mjadala huu sasa umefunguliwa. Kwa pamoja, tunaweza. Mungu Ibariki Tanzania. Asanteni sana. ....................................................... Mch. Peter Simon Msigwa,(MB) Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii Iringa Mjini 28.09.2013
Posted on: Sat, 28 Sep 2013 07:20:48 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015