JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA - TopicsExpress



          

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA 26 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI UTEKELEZAJI WA DIPLOMASIA YA UCHUMI Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imekuwa inatekeleza Sera Mpya ya Mambo ya Nje iliyoanza kutumika rasmi 2001. Lengo la sera hii ni kufanya mageuzi katika sera ya awali ya mambo ya nje ya Tanzania ili iendane na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yaliyotokea ndani nan je ya nchi. Sera mpya inaweka kipaumbele kwenye diplomasia ya uchumi, na kazi kubwa ya Wizara ya Mambo ya Nje ni kuratibu shughuli za wizara nyingine na Asasi za serikali na binafsi katika kukabiliana na changamoto za maendeleo kwa kufuata diplomasia ya uchumi madhubuti na endelevu. Mikakati inayotumika kutekeleza sera ya mambo ya nje ni pamoja na kujenga mazingira wezeshi ya ndani ya kukuza uchumi; kuimarisha ubia wa kimataifa; kuweka mbele malengo ya uchumi katika ushirikiano wa pande mbili (bilateral cooperation); kuimarisha uhusiano wa kimataifa (multilateral cooperation); kukuza ujirani mwema na kukuza ushirikiano wa kikanda. Njanja zinazotumiwa kutekeleza malengo ya kukuza ushirikiano ni mikutano ya pande mbili, tume za pamoja za ushirikiano, mikutano ya kimataifa, balozi zetu nchi za nje na ziara za viongozi wetu wa kitaifa nchi za nje na viongozi wa mataifa ya nje hapa nchini. Wizara imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, ambayo yamejidhihirisha katika sekta mbali mbali, zikiwemo za afya, kilimo, nishati, mifugo na uvuvi, viwanda, miundombinu na uchukuzi. Baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2011/12 hadi sasa ni pamoja na yafuatayo:- Sekta ya Afya Mwezi Oktoba, 2012, Bloomberg Philanthropies ya Marekani ilitoa Dola za Marekani milioni nane(US$8,000,000) kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya vijijini hapa nchini. Ufadhili huo ulizinduliwa mjini New York, Marekani, na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Msaada huo utatumika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya za dharura kwa wanawake wajawazito na kuendesha mafunzo kwa maafisa tabibu wasaidizi na wakunga. Sekta ya kilimo Katika mwaka wa fedha wa 2012, Mradi wa Rais Barack Obama wa Marekani wa kuendeleza uzalishaji wa chakula katika nchi zinazoendea (Feed the Future) ulisaidia zaidi ya wakulima 14,000 kutumia mbinu mpya za kilimo katika mashamba yao ya jumla ya hekta 22,430, chini ya mpango wa Taifa was kukuza kilimo ukanda wa kusini (SAGCOT), wakati wakulima wengine 13,000 walisaidiwa kuongeza uzalishaji kwa hekta kwa asilimia 46. Mradi huo pia ulifadhili mipango ya lishe iliyofaidia watoto 96,000 nchini. Aidha, wizara ilifanikiwa kushawishi mamlaka za Chakula za Jamhuri ya Watu wa China kuruhusu tumbaku inayozalishwa Tanzania kuingia kwenye soko la China. China peke yake inanunua asilimia 46 ya tumbaku yote duniani na inalipa bei ya juu kuliko nchi nyingine. Sekta ya Nishati Serikali ya China imetoa mkopo wa masharti nafuu kujenga bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na mitambo ya kusafishia gesi hiyo. Jumla ya gharama za mradi huu utakaoongeza uzalishaji wa umeme nchini ni dola za Marekani bilioni 1.2. Aidha, Tanzania ni kati ya nchi saba za Afrika zitakazofaidika na mradi wa upanuzi wa uzalishaji wa umeme utakaogharimiwa na Serikali ya Marekani (dola za Marekani bilioni 7) na Washirika wengine wa maendeleo (dola bilioni 9). Sekta ya Mifugo na Uvuvi Wizara iliratibu ziara ya ujumbe wa wataalam kutoka serikali ya Oman uliokuja nchini kutafuta fursa za biashara ya nyama na mazao yake. Mazungumzo yanaendelea kati ya Oman na Kampuni ya Ranchi za Taifa ili kuwezesha nchi yetu kufaidi9ka na biashara ya mifugo na kuboresha maisha ya wafugaji. Sekta ya Viwanda Wizara imeratibu mipango ya kampuni ya Nitori ya Japan kuwekeza katika sekta ya viwanda hapa nchini. Nitori itajenga kiwanda cha nguo katika Ukanda Maalum wa Uwekezaji uliopo Bagamoyo, na tayari imepatiwa eneo la kulima pamba huko Handeni, Tanga. Uwekezaji huo utatoa ajira kwa maelfu ya Watanzania. Wakati huohuo, Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wetu New Delhi, india, inaratibu mpango wa Serikali ya India kufadhili miradi ya kuendeleza teknolojia ya viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO). India itatoa dola za Marekani milioni 2 ikiwa ni sehemu ya msaada ulioahidiwa na Waziri Mkuu Dkt. Manmohan Singh alipotembelea Tanzania Mei, 2011. Sekta ya Miundombinu na Uchukuzi Wizara imeshiriki kuivutia kampuni ya China Merchant Holding International kuja kujenga bandari kubwa ya kisasa (4th generation port) huko Bagamoyo, ambako pia kampuni hiyo itajenga eneo la ukanda maalum wa uwekezaji (Export Processing Zone- EPZ), mji wa kisasa pamoja na miundombinu ya reli na barabara. Mkataba wa Mwongozo (Framework Agreement) kuhusu uwekezaji huo ulitiwa saini wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping hapa nchini, Machi, 2013. Mradi huo mkubwa utatoa ajira za moja kwa moja kwa maelfu ya Watanzania na kuliingizia taifa mapato kutokana na kodi na mrabaha. Aidha utasaidia kupunguza foleni na msongamano katika jiji la Dar es Salaam. Kadhalika, Serikali ya Japan imekubali ombi la Tanzania kupitia Wizara yetu, kufadhili ujenzi wa barabara za kupita juu (flyovers) katika makutano ya Barabara za Nyerere na Mandela, eneo la TAZARA jijini Dar es Salaam. Makubaliano hayo yalifikiwa katika mkutano uliofanyika Arusha Mei, 2012, kati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa JICA. Mkataba wa makubaliano hayo umetiwa saini na Serikali ya Japan inafanya maandalizi ya ujenzi. Sekta ya Maji Wizara imeweza kushawishi nchi mbali mbali rafiki kusaidia ujenzi wa miradi ya maji hapa nchini. Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Serikali za Ujerumani na Tanzania, wamegharamia mradi wa maji wa Swaya mkoani Mbeya, ambao utafaidia wananchi 490,000. EU imechangia shilingi bilioni 36.9, Ujerumani shilingi bilioni 13.5 na Serikali ya Tanzania shilingi bilioni 29.1 Mradi huo ulifunguliwa na Mheshimiwa Rais Kikwete wakatiwa ziara ya Mheshimiwa Jose Manuel Barroso, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya hapa nchini Julai, 2012. Aidha, Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund), imesaini makubaliano ya kugharamia mradi mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, utakaofaidia mamia ya maelfu ya wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Mradi huo utatekelezwa mwaka huu wa fedha. Mafanikio mengine ya Wizara Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC). Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Kituo hicho jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kina uwezo wa kuchukua watu 1600 kwa wakati mmoja na ujenzi wake umegharimu USD Milioni 15.5. Ufunguzi wa Balozi mpya: Tangu kipindi cha mwaka 2007 hadi 2013 Tanzania imefungua Balozi mpya nne ambazo zimefunguliwa katika nchi za Brazil, Malaysia, Uholanzi na Comoro na kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya Balozi 34, Balozi Ndogo 3 na Balozi za Heshima 17. Heshima ya Tanzania Kimataifa: Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka 2008 chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Tanzania sasa ni Mwenyekiti wa Asasi ya Ulinzi, Siasa na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC-TROIKA) kuanzia Agosti 2012 hadi Agosti 2013. • Uteuzi wa Watanzania wengi kushika nyadhifa mbalimbali kimataifa na kikanda: Mfano ni Dkt. Asha-Rose Migiro, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na hivi sasa ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo katika Masuala ya UKIMWI Barani Afrika. Mwingine ni Balozi Liberata Mulamula, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu (ICGLR), na wengine wengi. Ziara za viongozi wa Mataifa Makubwa Duniani Katika kipindi cha utakelezaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje, Tanzania imekuwa mwenyeji wa ziara kadhaa za viongozi wa juu wa mataifa makubwa duniani. Mwaka huu wa 2013 pekee, nchi yetu imetembelewa na Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China na Rais Barack Obama wa Marekani. Rais Xi amekuwa kiongozi wa juu wa pili wa China kutembelea Tanzania ndani ya miaka mitano iliyopita wakati Rais Obama ni Rais wa tatu wa Marekani aliyeko madarakani kuzuru nchi yetu tangu mwaka 2000. Ziara hizi ni kilele cha mafanikio ya sera yetu mpya ya mambo ya nje na zinadhihirisha umaarufu ambao viongozi wetu wameijengea nchi yetu katika uwanja wa kimataifa. Aidha, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Majadiliano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue), uliohudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali saba. Zaidi ya nchi 20 ziliwakilishwa kwenye mkutano huo. Hitimisho Sera mpya ya Mambo ya Nje inayoweka kipaumbele kwenye diplomasia ya uchumi, imeleta manufaa makubwa kwa nchi yetu na kuweka wazi zaidi jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa la kuratibu na kusukuma juhudi za kukuza uchumi wa taifa. IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES N ` SALAAM. JULAI 28, 2013
Posted on: Sun, 28 Jul 2013 10:03:56 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015