JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA - TopicsExpress



          

JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MRADI WA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA ELIMU YA JUU Katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Elimu ya Juu nchini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatekeleza Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (Science Technology and Higher Education Project - STHEP) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia. Mradi huu umejikita katika nyanja kuu 4 ambazo ni: kuboresha rasilimali watu kwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi (staff development), kujenga, kupanua na kukarabati vyumba vya mihadhara, maktaba, maabara na karakana (Civil Works), kununua vifaa vya kufundishia vikiwemo vifaa vya maabara na TEHAMA, vitabu na magari (Procurement of Goods) na kuboresha mitaala, sera na usimamizi kwa kutumia wataalamu washauri (Consultancy services for curriculum review, policy, capacity building, design and supervision of civil works). Taasisi 15 za umma zinazotekeleza mradi huu ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Dares Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Serikali cha Zanzibar (SUZA). Taasisi nyingine ni Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia (MCST) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Hadi sasa Mradi umegharamia mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 191 wa taasisi za umma masomo ya Shahada ya Uzamivu (PHD) na watumishi 208 wamepata ufadhiri wa mafunzo ya Shahada za Uzamili (Masters) katika fani za sayansi, teknolojia na ualimu. Aslilimia 30 ya watumishi hawa wanasomeshwa katika vyuo vikuu bora katika nchi zilizoendelea ikiwemo Uingereza, asilimia 30 wanasomeshwa katika nchi zinazoendelea mfano Afrika Kusini na kwingineko na waliobaki (asilimia 40) wanasomeshwa hapa nchini. Asilimia 15 ya watumishi wanaosomeshwa na mradi huu wamekamilisha masomo yao na wengine watamaliza mwishoni mwa mwaka huu. Vilevile watumishi 467 wamesomeshwa mafunzo maalum ya muda mfupi. Aidha, mradi umejenga jumla ya majengo 25 ya mihadhara, maktaba, ofisi na karakana ambapo mengi yapo kwenye hatua za mwisho kukamilika katika taasisi mbalimbali. Majengo haya yatatumiwa na jumla ya wanafunzi 36,344 wa elimu ya juu na wakufunzi na wahadhiri 1,640 katika taasisi za ARU, DUCE, DIT, OUT, MUCE, SUA na UDSM. Mradi huu pia umenunua vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo vifaa vya maabara, vifaa vya TEHAMA 1,831, vitabu 4,598, mitambo ya kufundishia na magari 19. Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu umesaidia Tume ya Vyuo Vikuu kujenga uwezo wa TEHAMA na kuwezesha kudahili wanafunzi wote wanaojiunga na elimu ya juu kwa pamoja (Central Admissions System - CAS) na umeiwezesha TCU kutoa mwongozo wa ubora wa Vyuo Vikuu hapa nchini (Universities Standards and Benchmarks). Aidha, mradi umewezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuandaa miundombinu ya TEHAMA ili waombaji wa mikopo ya Elimu ya juu waombe kwa kutumia mtandao (Online Loan Application System - OLAS). Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu pia umesaidia TCU kujenga uwezo wa kukokotoa ada elekezi kwaajili ya wanafunzi wa elimu ya juu (Higher Education Students Unit Cost). Mradi wa STHEP ni wa muda wa miaka 7 ukiwa na duru mbili ziitwazo Adaptable Lending Program-1 (APL-1) na Adaptable Lending Program–II (APL-II). Duru ya kwanza ilianza Julai 2008. Duru ya pili inatazamiwa kuanza kabla ya duru ya kwanza kuisha hapo Desemba, 2013 na kukamilika June, 2016. Mradi huu unalenga kuongeza matumizi ya taaluma katika shughuli za kiuchumi nchini (application of knowledge in economic activities), na malengo ya haraka (immediate goal) yakiwa ni kuongeza idadi ya wanafunzi na kuboresha mazingira ya kufundishia katika elimu ya juu hapa nchini kipaumbele kikiwa katika fani za sayansi,teknolojia na ualimu. Ntambi Bunyazu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini 20/09/2013
Posted on: Fri, 20 Sep 2013 13:44:35 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015