KCMC YAIBUKA KINARA WA KULIPA KODI MKOANI KILIMANJARO HOSPITALI - TopicsExpress



          

KCMC YAIBUKA KINARA WA KULIPA KODI MKOANI KILIMANJARO HOSPITALI ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro (KCMC), imetangazwa kuwa mlipa kodi bora kwa mwaka 2013 mkoani Kilimanjaro katika kitengo cha walipa kodi wakubwa wa mkoa huo. KCMC imekuwaya kwanza kati ya Makampuni na Taasisi mbalimbali mkoani hapa yaliyoshindanishwa katika kitengo cha walipa kodi wakubwa kutokana na juhudi zake katika kuhakikisha inalipa kodi kutokana na huduma wanazotoa kwa jamii. Hii ni mara ya pili kwa Hospitali hiyo kuibuka wa Kwanza kwani mwaka 2011 KCMC ilifanikiwa kupata tuzo ya mlipa kodi bora tuzo zinazotolewa kila mwaka na wakala waKodi na makato nchini (TRA). Akikabidhi cheti cha ubora kwa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo katika maadhimisho ya siku ya mlipa kodi yaliyofanyika kimkoa jana katika viwanja vya Uhuru Hostel, ya mjini Moshi, Meneja wa TRA mkoani Hapa, Patience Minga alisema kwa kuibuka mshindi wa kwanza kama mlipa kodi mkubwa bora, Hospitali ya KCMC imedhihirisha kwamba inawajali wateja wake. Minga alisema kuwa kila mwaka wamekuwa wakishindanisha makampuni na Taasisi mbalimbali katika tuzo hizo kwa lengo la kuingeza ufanisi katika swala zima la ulipaji kodi ikiwa ni pamoja na kuleta hamasa ya umuhimu wa kulipa kodi. “Kila mwaka, TRA tumekuwa tukishindanisha makampuni mbalimbali kwa lengo la kuongeza hamasa katika swala la kulipa kodi ambapo pia huwa tunatoa elimu kwa wananchi wote,” alisema Minga Meneja huyo alisema kuwa kila mwaka wamekuwa wakikusanya zaidi ya shilingi bilioni 10 mkoani Kilimanjaro kutokana na kodi huku akibainisha kuwa malengo yao kwa huu ni kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 74. Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Prof. Moshi Ntabaye alisema uongozi wa Hospitali hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na serikali katika kuhakikisha inarudisha fadhila kwa jamii ya Tanzania ambayo imeendelea kuiamini kwa takribani miaka 42 tangu ilipozinduliwa mwaka 1971, katika huduma wanazotoa kwa kulipa kodi. Ntabaye alisema ushindi huo unatokana na ukweli kwamba Hospitali ya KCMC imekuwa ikitoa huduma bora ambayo inawawezesha kulipa kodi kwa wakati kila mwaka ambapo alisema huwa wanalipa zaidi ya shilingi milioni mia moja kila mwaka. Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Dkt. Ibrahimu Msengi, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliwataka Wafanyabiashara na Wananchi kuendelea kulipa kodi kila mara kwani nchi haiwezi kuendeeshwa bila kodi. “Nchi yoyote ile haiwezi kuendeshwa bila Kodi, inatupasa kulipa kodi kila mara bila shuruti, hatuwezi kuendelea kwa kutegemea misaada hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunalipa kodi ili uchumi wetu ukue,” alisema Msengi. Washindi wengine ni, Mfanyabishara Patrick Boisafi, shule ya secondari ya St. Magreth, shule ya sekondari ya Kiraeni, Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADECO), shule ya sekondari ya international Moshi pamoja na mengine mengi.
Posted on: Sat, 09 Nov 2013 11:11:28 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015