Kwanini Uchumi Ukue kwa Kiwango cha 6% - 7% Lakini Ushindwe - TopicsExpress



          

Kwanini Uchumi Ukue kwa Kiwango cha 6% - 7% Lakini Ushindwe Kutengeneza Ajira..!? Uchumi wa Tanzania unakuwa kwa 7% lakini Serikali imefilisika! Kwa mikataba ya 3% hata kama uchumi ungekuwa kwa 20% kwa mwaka bado hatuwezi kutengeneza ajira wala kupunguza umasikini! Uchumi wa Tanzania umekuwa ukikuwa kwa muda wa miaka nane kwa kiwango kati ya 6% na 7% lakini umeshindwa kutengeneza ajira! Kwa kipindi cha miaka 4 sasa Serikali haiwahi kuajiri lakini inajivunia kwa mafanikio hayo makubwa ya kiuchumi! Je, ni kweli kuna fananikio ya kiuchumi kwa watanzania au ni hila za watawala na wawekezaji? Kwenye makala zangu za nyuma nimekuwa nikijiuliza kwamba inawezekana vipi uchumi ukue kwa kiwango cha 6% na 7% lakini ushindwe kutengeza ajira za moja kwa moja na zile ajira shirikishi (direct and indirect jobs)? Pia nimekuwa nikijiuliza inawezekana vipi uchumi unakuwa kwa kiasi kikubwa kila mwaka lakini Serikali haina pesa kabisa? Jambo lingine lililokuwa linanitatiza ni kwamba mbona ripoti inayotolewa na Serikali kuhusu kiwango cha mfumuko wa bei (inflation) ni kidogo sana (6%) lakini mfumuko wa bei za vyakula na huduma mbalimbali ni mkubwa sana!? Mfumuko wa bei wa bidhaa na huduma mbalimbali umekuwa ukikuwa kwa kiwango cha 50% hadi 60%, lakini takwimu zinazotolewa na serikali ni ndogo kupita kiasi; na hii imenifanya niwe mdadisi zaidi. Kutokana na utafiti wangu nilioufanya nimegundua pamoja na uchumi kukua kwa kiwango hicho cha 6% hadi 7% kwa miaka nane sasa mfululizo, lakini hauwezi kutengeneza ajira mpya kwa vile ukuaji wa uchumi wetu unachochewa na sekta mbili muhimu ambazo ni sekta ya madini na sekta ya utalii; sekta zote hizi mbili ni sekta ambazo zimeadhirika sana kwa kuwa na mikataba ya kifisadi. Kwa mfano, sekta ya madini ya dhahabu serikali inapata 3% na 97% iliyobakia wanachukuwa wawekezaji na washiriki wao, hivyo tunazalisha kiwango kikubwa sana cha dhahabu ambacho kiwango hicho hurekodiwa na World Bank na IMF lakini kiwango cha pesa kinachorudi nyumbani kwa ajili ya kujenga uchumi ni 3% tu, ambayo ni kiasi kidogo sana, hata hivyo kulingana na utafiti wangu nimeweza kugundua kwamba kiasi halisi kinachoingia katika pato la taifa hakizidi 1.5% kwa vile kulingana na kiwango kikubwa cha ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma bado hiyo 3% haiendi yote hazina kwa vile kuna wajanja hapo kati kati ambao wanaikamata na kuipiga panga! Hivyo basi tunaona kwamba uchumi unapigiwa debe kwamba unakuwa sana kwa vile serikali na mashirika ya fedha duniani World Bank na IMF hawaangalii kwamba kiasi cha pato la dhahabu kinachorudi nyumbani ni 3% na hata wakati mwingine chini ya hapo, bali wao wanaangalia kiasi chote cha pato la dhahabu kilichopatikana wakati asilimia 97% inaenda nje ya nchi na kujenga uchumi wa makapuni wawekezaji na uchumi wa Switzerland ambapo pesa nyingi chafu zinaishia huko. Nikirudi kwenye sekta ya utalii ambayo nayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi; sekta hii nayo kama ilivyo sekta ya madini nayo imekamatwa na wakubwa na wamejenga mazingira ya ufisadi kiasi kwamba pamoja na kwamba inazalisha sana pesa nyingi za kigeni, lakini asilimia 95% ya mazalisho haya huchukuliwa na makampuni ya wale tuowaita wawekezaji wakishirikiana na washirika wao ambao ni watawala wetu! Na makampuni haya ya wawekezaji ofisi zao kuu zipo huko Ulaya na watalii wote wanalipa pesa zote huko huko kabla ya kuja hapa nchini, na wanapokuja hapa nchini wanachodai ni huduma tu, kwa vile malipo yote yalishafanyika huko kwao! Hivyo basi kulingana na ukweli huo Tanzania inapata pesa nyngi kimaandishi kutokana na utalii, lakini kiasi cha kweli kinachorudi hapa nyumbani kwa ajili ya kujenga uchumi ni 5% na hata wakati mwingine ni kidogo zaidi ya hicho hasa kulingana na vitendo vya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma vilivyokidhiri hapa nchi; mnakumbuka kwamba wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa TANAPA walikuwa wanalipana US $ 10, 000 kwenye kila kikao wanachokaa, na wakati mwingine hukuna mara mbili kwa mwezi kwa muda wa lisaa limoja! Huu ni moja tu kati ya maelfu ya mifano ya vitendo vya ufisadi wa rasimali za umma. Kulingana na ripoti iliyotolewa hivi karibuni na World Bank na IMF Tanzania imeonyeshwa kwamba ina uchumi mzuri ukilinganisha na nchi nyingi za Kiafrika na hata kidunia; kwa mfano Tanzania imetajwa kuwa ni nchi ya 85 duniani kwa kuwa na kiasi kikubwa cha PPP (Purchasing Power Parity) yaani uwezo wa sarafu wa kununua bidhaa ya aina ile ile kwenye nchi mbili tofauti kwa wakati ule ule. Taarifa hizi pamoja kwamba zimetolewa na taasisi za kimataifa lakini mimi nazipinga kwamba siyo sahihi! Kiwango hicho cha PPP siyo kwa ajili ya Watanzania bali ni kwa makapuni yenye mikataba ya kifisadi yakishirikiana na watawala wetu. Ni World Bank na IMF hao hao ndiyo wanaoandika kwamba mfumuko wa bei Tanzania ni 6%! Wao wapo New York hata kama wana tawi Mirambo Street lakini hawajawahi kutembelea masoko ya Kariakoo, Buguruni, Ilala, Tandika na Tandale wakajionea hali halisi ya mfumuko wa bei kwenye bidhaa na huduma mbalimbali, hivyo kulingana na hali halisi nimegundua kwamba takwimu nyingi za taasisi hizi za kimataifa si sahihi na mara nyingi huwa zina ushawishi mkubwa wa Bank kuu (BOT) ambayo haipo huru bali inaongozwa na wanasiasa wa CCM. World Bank na IMF pamoja na kutoa muhtasari wa takwimu za uchumi za Tanzania, lakini wameshindwa kutoa sababu kwamba ni kwanini nchi inakuwa kiuchumi kwa 6% hadi 7% kwa zaidi ya miaka nane lakini inashindwa kutengeneza ajira! Nadhani World Bank na IMF hili wameliona lakini hawataki kulizungumzia, labda kwa sababu serikali ina wachombezaji (Lobbyists) wake ndani taasisi hizo. Kulingana na taratibu za kiuchumi ni kwamba uchumi ukiweza kukua kwa kiasi cha 5% kwa mwaka basi huo ni uchumi mzuri na unaweza kutengeneza ajira za kutosha kila mwaka kwa soko husika. Ninachotaka kusema ni kwamba uchumi wa Tanzania hauwezi kutengeneza ajira mpya hata kama uchumi wetu ungelikuwa kwa asilimia ishirini kwa mwaka (20%) hatuwezi kutengeneza ajira kwa vile ukuaji wa uchumi huo ni wa maneno tu, na si kivitendo kwa vile kiasi cha fedha zinazorudi hapa nchini au kiasi cha pesa kinachobaki hapa nchini ni kidogo sana kiasi kwamba hakiwezi kutatua tatizo gumu la ajira, bali kiduchu hicho cha fedha hutumia kutatua matatizo ya kawaida kama vile afya na elimu ambayo yamekuwa matatizo sugu kwa muda mrefu. Uchumi wetu utaweza kutatua tatizo la ajira ikiwa tu tutabadilisha mikataba ya madini, utalii na sekta zote muhimu katika uzalishaji ili serikali ipate kiasi kikubwa cha murahaba kitu ambacho kitaiwezesha serikali kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kutengeneza ajira mpya kwa vijana wa Kitanzania. Hivyo bila ya kubadilisha mikataba ya dhahabu, utalii, gesi, umeme, mashirika ya simu za mikononi, kilimo na mingineyo, uchumi wa Tanzania utakuwa ni uchumi tasa, yaani uchumi wa kwenye makaratasi tu lakini hauwezi kufanya lolote. Wawekezaji wote wanaowekeza katika soko la rasimali za Libya wanaondoka na 10% tu na inayobakia 90% ni mali ya Serikali! Na makampuni haya haya yanayowekeza hapa kwetu ndiyo hayo hayo yanayogombania mikataba ya Libya! Sasa ni kwanini Libya waondoke na 10% tu na wawe wamwridhika, lakini hapa kwetu wanaondoka na 97% na bado hawajaridhika..!!?? Siku za nyuma niliwahi kumkosoa Benjamin Mkapa hadharani kwamba ameuweka uchumi wa nchi hii katika mazingira magumu sana, lakini kuna watu waliniona kama ninamkebehi Mkapa na sitaki kuyaona mazuri aliyoyafanya; na mazuri anayosifiwa nayo Mkapa ni kukusanya kodi nyingi sana, kuidhoofisha Tanesco kiuchumi, kubinafsisha mashirika na mali za umma kwa marafiki na yeye mwenyewe, na kujenga uwanja wa mpira! Sasa naamini wale waliokuwa wananipinga kuhusu Mkapa kwamba ametufanya kitu mbaya, naona wameshaanza kukubaliana na mimi kwa vithibitisho kwamba pamoja na kwamba kwa miaka nane mfululizo uchumi unakuwa kwa 6% hadi 7% lakini watanzania wanazidi kuwa masikini, na ukosefu wa ajira limekuwa ni tatizo la kawaida. Nimemsikia hivi karibuni mtu mmoja anayewania kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM huyu si mwingine bali ni Edward Lowasa akijigamba kwamba Boda-Boda ni ubunifu wa chama chake cha CCM katika mikakati ya kupunguza tatizo la ajira!! Ikumbukwe kwamba Edward Lowasa alipiga sana makelele akisema tatizo la ajira kwa vijana ni Bomu na kama kawaida yake akapata washabiki wengi wa vyombo vya habari wakimshabikia kwamba Lowasa amesema tatizo la ajira kwa vijana ni Bomu! Mimi nikamtegemea kwamba kulingana na uzoefu wake wa miaka mingi ndani utawala wa CCM labda ana mikakati endelevu ya kutatua tatizo sugu la ajira hapa nchini, lakini nichoka na kukosa nguvu pale alipojigamba kwamba ajira muhimu kwa vijana ni Boda-Boda..!!! Hata hii mikataba ya siri ya Gesi, Makaa ya mawe, Umeme, Uranium, uuzaji wa ardhi kwa wageni na mingineyo inayofanywa na serikali ya Kikwete itandelea kukuza uchumi lakini si kwa manufaa ya watanzania bali kwa manufaa ya makampuni wawekezaji pamoja na watawala wetu. Uchumi utaendelea kuwa mkubwa kwenye makaratasi lakini pato kubwa la uchumi huo litaenda huko nje ya nchi kwa vile mikataba yenyewe ni ya asilimia ndogo sana kiasi kwamba pesa hizo haziwezi kubadilisha maisha ya watanzania. Watanzania tunajivuna kwamba ni nchi ya tatu barani Africa kwa uchimanji wa madini tukitanguliwa na South Africa na Ghana, lakini je, madini hayo yanatusaidia sisi au yanawasaidia watawala na wawekezaji!?Tanzania pamoja na kwamba uchumi wetu unasifiwa kupanda lakini sisi ni moja kati ya nchi masikini sana duniani kwa per capita ambayo ni US $ 663.108. Mwisho kabisa napenda kuwatahadharisha kwamba msidanganywe na watawala wanaowasifia kwamba uchumi wetu ni mzuri na unakuwa kwa kiwango kikubwa kila mwaka, uchumi ni mzuri na unakuwa kwa makampuni ya wawekezaji wakishirikiana na watawala wetu; hawa ndiyo wanaofaidi matunda ya uchumi wetu kwa 97% na hicho kidogo kinachobakia cha 3% ndicho tunachobakia nacho ambacho kimeshindwa kupunguza umasikini; dhahabu yetu inajenga uchumi wa South Africa, Canada, Australia na Switzerland huko ndipo ajira zinapotengenezwa kutokana na mauzo ya dhahabu yetu, lakini sisi tumeshindwa kutengeneza ajira kabisa! Kilichobakia sisi tuendelee kulalamika tu hadi hapo Yesu atakarudi..!! Dr. Noordin Jella
Posted on: Tue, 30 Jul 2013 10:09:05 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015