Lamu Mgombea wa kiti cha ugavana Fahim Yassin Twaha amepeleka - TopicsExpress



          

Lamu Mgombea wa kiti cha ugavana Fahim Yassin Twaha amepeleka kampeni zake eneo la Mokowe kaunti hii ya lamu na kuwashawishi wapiga kura kumuunga mkono. Akihotubia wafuasi wake Fahim ameomba ushirikiano wa pamoja kati yake na wananchi ili kuliendeleza gurudumu la maisha ya lamu. Aidha Fahim ameongeza kwamba licha ya kuwa yeye atachaguliwa kama kiongozi ataweza kuheshimu maoni ya wananchi bila ya ubaguzi ya jinsi wanavyotaka kuendelezewa kaunti yao kwa njia ya ufasaha. Hata hivyo Fahim amewaomba wenyeji kujitokeza kwa wingi tarehe 2 mwezi ujao na kumpigia kura. Bungeni Mkutano baina ya Rais Uhuru Kenyatta ,Spika wa bunge Justin Muturi na jaji mkuu Willy Mutunga kutafuta suluhu kati ya bunge na wafanyikazi wa mahakama huenda ukafanyika ingawa tarehe ya mkutano huo haijabainika Vilevile mswada uliopitishwa bungeni wa kumtaka rais Uhuru Kenyatta kuunda jopo la kuchunguza tofauti zilizoshuhudiwa katika idara ya mahakama, ambapo bunge lilipendekeza wafanyikazi sita kuchunguzwa unatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo. Mombasa Msongamano wa magari katika daraja la Nyali unaendelea kuwa kikwazo katika usafiri huku serikali ya kaunti ya Mombasa ikianzisha majadiliano na washikadau katika sekta ya usafiri na wahandisi ili kukabiliana na misongamano hiyo inayoshuhudiwa nyakati za asubuhi na jioni. Katika kikao na wahandisi kutathmini mikakati ya kutatua msongamano huo,gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amesema majadiliano zaidi yanaendelea ili kupata njia ya kutatua msongamano huo. Hatua hiyo huenda ikapelekea kupanuliwa kwa daraja la Nyali au kubuniwa kwa njia ya mkato itakayofanikisha usafiri wa haraka kwa wananchi na magari yanapotaka kufika na kutoka mjini. Vurumai Vurumai limetanda mapema leo katika soko la kongowea baada ya wafanyibiashara kuandamana sokoni humo kupinga hatua ya kufungwa kwa baadhi ya vyoo. Wafanyibiashara hao wamepigwa na butwaa baada ya kukumbana na ua uliozungushwa vyoo hivyo kuwazuia wao kutumia vyoo hivyo jambo lililowaghadhabisha mno na kuitaja hatua hiyo kama yenye lengo fiche kando na kuwanyanyasa wafanyibiashara. Wakiongozwa na mwenyekiti wao Ali Mtsumi wamebomoa ua hilo huku wakishinikiza mdhamini na mwanakandarasi kuanza ukarabati wa vyoo vilivyofungwa takriban miaka minane iliyopita badala ya kufunga vinavyotumiwa kwa sasa. Wakati huo huo wafanyibiashara hao wamemtaka gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho kuingilia kati na kutatua mtafaruku huo walioutaja kuchangiwa na baadhi ya maafisa wa fisadi wenye nia ya kufaidika na mradi huo wa ukarabati wa vyoo vyao vya kibinafsi. Walemavu Mashirika ya utetezi wa haki za walemavu yametaka serikali za kaunti ukanda wa pwani kuweka mikakati itakayoimarisha jamii ya walemavu ili kukabiliana na hali ya umaskini na uhaba wa ajira. Mashirika hayo yakiwemo shirika la ALBINO SOCIETY OF KENYA na VISION OF THE BLIND imesema jamii ya walemavu ipo katika hatari ya kutumiwa iwapo hakutabuniwa sheria kali. Kulingana na mwenyekiti wa walemavu wa ngozi ukanda wa pwani Josphat Mzungu ukosefu wa ajira na elimu kunapelekea walemavu wengi kutumika kutekeleza biashara zisizo halali. Kimataifa Idadi rasmi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Haiyan nchini Ufilipino imepanda na kufikia watu 2,344. Baraza la kushughulikia maafa la taifa limetoa tarakimu hiyo hii leo. Baraza hilo limesema watu 3,804 wamejeruhiwa na wengine zaidi ya 79 hawajulikani walipo. Kimbunga hicho kililishambulia eneo la mashariki mwa nchi hiyo siku ya ijumaa na kuharibu maelfu ya nyumba na kusababisha watu laki sita kukosa makazi. Hata hivyo oparesheni kubwa ya kutoa msaada inaendelea licha ya kuwa watu wengi katika eneo hilo la maafa hawajapata msaada.
Posted on: Thu, 14 Nov 2013 13:10:09 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015