MTUME MUHAMMAD (swallallahu alaihi - TopicsExpress



          

MTUME MUHAMMAD (swallallahu alaihi wasallam) ..SUNNA-SIYRAH.....RAHMA KWA WALIMWENGU SEHEMU YA THELATHINI NA MBILI MAFUNZO Hii ni mifano michache ya mashambulizi na mateso aliyotendewa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na sahibu zake (Radhiya Llaahu ‘anhum) ikisadikisha kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Aliposema: أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ... لا يُفْتَنُونَ “Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?” Surat al-‘Ankabuut- 1 Na Akasema: أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُواْ الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْاْ مِن قَبْلِكُم مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاء وَالضَّرَّاء وَزُلْزِلُواْ حَتَّى يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ مَتَى نَصْرُ اللّهِ أَلا إِنَّ نَصْرَ اللّهِ قَرِيبٌ “Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyowajia wale waliopita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walioamini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Allaah itakuja? Jueni kuwa nusura ya Allaah ipo karibu.” Al-Baqarah-214 Imepokelewa kuwa siku moja Khubaab bin Al-Arat alimuendea Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamuambia: “Ewe Mtume wa Allaah, makafiri wanatutesa sana, si bora ungelimuomba Allaah atusaidie?” Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikaa chini kwanza huku uso wake ukiwa mwekundu kisha akasema: “Waliokuja kabla yenu, mtu alikuwa akichunwa nyama yake au mishipa iliyo juu ya mafupa yake kwa msumeno wa chuma, na mateso hayo hayakuweza kumtoa katika Dini yake. Kisha akiwekewa msumeno juu ya kichwa chake na kukatwa pande mbili na hayakumtoa hayo katika Dini yake. Allaah Ataitimiza (ataipa ushindi) Dini hii, na itafika siku mtu ataweza kusafiri kutoka Swan’aa (Yemen) hadi Hadhramawt bila ya kuhofia chochote isipokuwa Allaah.” Al-Bukhaariy na Ahmad Kutokana na aya hizi pamoja na mateso yale, tunaelewa kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Hampi mja wake ushindi mpaka kwanza Ampambanishe na mithihani na majaribio. Na kutokana na yaliyotangulia, tunapata pia fundisho kuwa Allaah Alimpa ushindi Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) dhidi ya adui zake waliokuwa wakimfanyia isthizai na kumkejeli na kumtesa kwa kuuliwa makafiri hao na kutupwa ndani ya kisima. Allaah Anasema: إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli. Al-Hijr - 95 Wanasema Maulamaa pia kuwa katika darsa iliyotangulia tunapata fundisho kuwa mtu anatakiwa kuwalingania watu wa karibu yake kwanza, ndugu na jamaa zake kabla hajawaendea watu wa mbali. Kwani si jambo la busara kwa mtu kuwaita watu wa mbali katika tabia njema kwa mfano wakati watoto wake na watu wa nyumba yake wako katika upotovu (upotevu). Isitoshe mlinganiaji anahitajia watu wa kumhami na kumlinda na kumsaidia, na bila shaka watu wake watakapomfuata watakuwa msitari wa mbele katika kumhami mlinganiaji kupita watu wa mbali. Ndiyo maana watu wa mwanzo kusilimu walikuwa mkewe Bibi Khadiyjah na Zayd na ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliokuwa wakiishi nyumbani kwake, na pia Abu Bakr (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa sahibu yake. Tunapata fundisho pia kuwa kule kusimama imara Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) baada ya mateso yote yale ni dalili ya imani yao ya kweli isiyotetereka, na kwamba walikuwa wakishirikiana na kupendana, na walikuwa tayari kujitolea kwa roho zao na nafsi zao na mali zao kwa ajili ya kuisimamisha Dini ya Allaah, na walikuwa wakitegemea kutoka kwa Allaah zawadi tukufu zaidi kupita adhabu ile iumizayo waliokuwa wakiipata hapa duniani kutoka kwa makafiri wa Makkah. Starehe na natija na faida inayomtawala na kumridhisha mtu aliyeamini kikweli inakuwa ya kiroho na siyo kimwili. Maswahaba kwa mfano (Radhiya Llaahu ‘anhum) utawakuta siku zote nafsi zao zikiridhika na mateso ya kimwili kama vile njaa na usingizi na adhabu na kufukuzwa na kukimbizwa na adhabu nyingine za kimwili, kwa kutegemea kupata kilicho kitukufu zaidi, nacho ni radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa). Kwa njia hii azma ilipata ushindi na uhuru wa kweli ulipatikana, na kwa njia hii waliweza kufanikiwa kuwatoa watu katika giza na kuwaingiza katika nuru. MBINU MBALI MBALI Makafiri walipoona kuwa mateso mbali mbali na ukatili waliokuwa wakimfanyia Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na Sahibu zake (Radhiya Llaahu ‘anhum) hayakuweza kuivunja nguvu Dini hii mpya, wakaamua kutumia mbinu nyingine za kuwachukiza watu nayo. Wakaanza kwa kusema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni mwendawazimu, kisha wakasema kuwa ni muongo, wakamtuhumu kuwa ni mchawi, na kwamba Qur-aan ni visa vya watu wa zamani, wapotovu na mambo mengi mengine, ikawa kama Allaah Alivyosema: إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُواْ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ. وَإِذَا مَرُّواْ بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ. وَإِذَا انقَلَبُواْ إِلَى أَهْلِهِمُ انقَلَبُواْ فَكِهِينَ. وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَؤُلَاء لَضَالُّونَ. وَمَا أُرْسِلُوا عَلَيْهِمْ حَافِظِينَ Kwa hakika wale waliokuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walioamini. Na wanapopita karibu yao wakikonyezana. Na wanaporudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi. Na wanapowaona husema: Hakika hawa ndio khasa waliopotea. Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao. Al-Mutwaffifiyn – 29-33 UNAONAJE TUKAABUDU UNACHOABUDU Imepokelewa kuwa siku moja wakati Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akitufu Al-Ka’abah, alisimamishwa na Al Aswad bin ‘Abdul-Mutwallib bin Asad na ‘Abdul’Uzza na Al Waliyd bin Mughiyra na Umayya bin Khalaf na makafiri wengine, wakamuambia: “Ewe Muhammad! Unaonaje sisi tukaabudu unachokiabudu na wewe pia uabudu tunachokiabudu sisi na tushirikiane sisi na wewe katika jambo hili. Ikiwa unachokiabudu wewe kina Kheri kuliko chetu na sisi tutapata kufaidika pia, na kama tunachoabudu sisi kina Kheri zaidi kuliko unachoabudu wewe, na wewe pia utapata kufaidika. Kutokana na kauli yao hiyo, ndipo Allaah Alipoiteremsha Suratul Kaafirun: قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ. لا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ. وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ. وَلا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ. وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ. لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ. Sema: Enyi makafiri!. Siabudu mnachokiabudu. Wala nyinyi. hamuabudu ninayemuabudu. Wala sitaabudu mnachoabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu. Suratul Kaafiruun ITAENDELEA.....
Posted on: Tue, 01 Oct 2013 14:57:07 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015