Mpenzi msikilizaji wa 102.1 ILASI FM REDIO Tunakualika kuungana na - TopicsExpress



          

Mpenzi msikilizaji wa 102.1 ILASI FM REDIO Tunakualika kuungana na watangazaji wako Stephano Simbeye na Bosco Nyambege katika Kipindi cha Global Planet ili tukujuze mambo mbalimbali kama ifuatavyo:- KIPINDI CHA GLOBAL PLANET MEI, 24,2013 SAIKOLOJIA NA MAISHA. Neno wivu katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, limeelezewa kama hali ama tabia ya mtu kusononeka au kukasirika muda amuonapo mpenzi au rafiki yake ana uhusiano wa mapenzi na mtu mwingine. Kamusi hiyo pia imeeleza kuwa neno hilo hilo wakati mwingine hutumika kama ngoa ama kijicho. Ngoa ni hali ya kuona uchungu, vibaya au chuki kwa kukosa kitu ambacho mwingine amekipata. Kijicho nalo limeelezwa kuwa ni tabia ya mtu kutopenda mwingine apate mafanikio. Sasa hali ambayo leo napenda kuizungumzia haitahusiana na masuala ya kimapenzi kama kamusi hiyo ilivyoelezea. Naizungumzia ile ya kuona uchungu, vibaya na kuumia kutokana na mtu mwingine kupata mafanikio. Watu wengi wanaposikia neno wivu masikioni mwao huona ni kitu kibaya na hata siku moja hakiwezi kuwa kizuri. Ni sawa wivu ni kitu kibaya sana kama isipoangaliwa lakini pia ni tabia ambayo ikitumika vilivyo inaweza kuleta faida katika maisha ya binadamu. Wivu ni kitu cha asili ambacho kila binadamu anacho. wanyama pia wana wivu kiasi kwamb Hakuna hata binadamu mmoja ambaye hana tabia ya wivu, achilia mbali binadamu hata a hakuna sababu za wazi kwa nini binadamu ana wivu. Hiyo ni hali ya kawaida ambayo kila mtu anazaliwa nayo. Ni wivu wa aina gani ambao unakubalika na una faida? Kwa wale ambao wako mashuleni wivu unahitajika ili uweze kufanya vizuri katika masomo yako. Usipokuwa na wivu unaweza kuona kwamba mwenzako kupata 100% wewe ukapata 30% ni kitu cha kawaida tu. Lazima uwe na wivu na huyo aliyepata alama nzuri ili uweze kufanya jitihada za dhati kuhakikisha unamfikia kama siyo kumpita kabisa. Kama unaishi na mtu ambaye amekuwa na mafanikio makubwa siyo vibaya kama utakuwa na wivu juu yake kwa kujiuliza kwa nini yeye kafanikiwa. Lazima ikuume na wivu huo ukufanye kuwa na juhudi katika kuhakikisha na wewe unafanikiwa kama yeye. Kama uko kazini na mwenzako kapandishwa cheo, kuwa na wivu kwa kujiuliza kwa nini mwenzako amepandishwa cheo wewe umeachwa? Je, ni kutokana na kufanya kazi kwake kwa bidii au ni nini? HABARI MUHIMU ZA MAGAZETI YA LEO. GAZETI LA NIPASHE Brigedia Jenerali wa Marekani kutua nchini leo Mkuu wa Kamandi ya Utafiti wa Tiba wa Jeshi la Marekani (MRMC), Brigedia Jenerali Joseph Caravalho, akifuatana na ujumbe wa watu watano atawasili nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia leo. Taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana ilisema, ujumbe huo ukiwa nchini utaungana na maafisa wawili kutoka Kituo cha Tiba cha Walter Reed Army Institute of Research’ (WRAIR) kilichopo Dar es Salaam. Ratiba ya ziara ya ugeni huo iliyotolewa na JWTZ inaonyesha kuwa, kesho utakabidhi Jengo la Mama na Mtoto katika zahanati ya Mwenge. Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, atapokea jengo hilo kwa niaba ya JWTZ. Membe: Ujio wa Obama ni neema kwa Tanzania Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema ujio wa Rais wa Marekani Barack Obama ni wa umuhimu kwa nchi kwani utaipatia Tanzania zaidi ya dola milioni 800 (sawa na Sh. Trilioni 1.3) kwa ajili ya kukamilisha malengo ya milenia. Membe alizungumza hayo jana katika wa mkutano baina yake na mabalozi wa nchi za Umoja wa Afrika nchini pamoja na wanahabari jijini Dar es Salaam. Membe alisema fedha hizo zitasaidia kukamilisha miradi mbalimbali katika sekta za barabara, maji na elimu, akiwa nchini rais Obama ataongozana na ujumbe wa wafanyabiashara 700. Kwa mujibu wa Membe, rais Obama atafanya mkutano na wakurugenzi wa mashirika makubwa kwa pamoja na wale kutoka Marekani huku ujumbe wa mkutano huo ukiwa Power Afrika (Saidia Afrika). Pia rais Oboma ambaye katika ziara yake ataambatana na mkewe Michele Obama, atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Kikwete. Alisema kabla ya kuwasili kwake nchini, tayari ameshatuma timu kwa ajili ya kumwandalia mazingira ya ujio wake huo huku ya pili ikitarajiwa kuwasili muda wowote. Membe aliongeza kuwa, ujio wa Obama Julai Mosi na 02, mwaka huu utakutana na mambo mengi muhimu yakiwamo ya ‘smart dialogue partnership’ yatakayofanyika nchini kwa kujumuisha nchi mbalimbali huru za Afrika. Aidha, aliwataka wafanyabiashara mbalimbali wakiwamo wa vyombo vya usafiri kama vile teksi na wamiliki wa hoteli kutumia vizuri fursa hiyo ya takribani wiki nzima kwa kuanza na ugeni wa smart dialogue partinership ambao wataanza kuingia mwishoni mwa mwezi huu. Kuhusu maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa kwa Umoja wa Afrika (AU) wakati huo Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, John Haule alisema yatafanyika Mei 26, mwaka huu katika nchi zote za Afrika huku kibara yakifanyika katika makao makuu ya Umoja huo, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Kwa mujibu wa Haule, hapa nchini maadhimisho hayo yatafanyika katika ukumbi wa Karimjee huku mgeni rasmi akiwa Waziri Membe. Alisema kwa Tanzania kufanya maadhimisho hayo ni muhimu kwani ilihusika kwa sehemu kubwa kuzisaidia nchi za Afrika kupata uhuru wao kutoka kwa wakoloni. Aliyataja mafanikio ya umoja huo wakati huo ni nchi nyingi za Afrika kupata uhuru kutoka 32 hadi 53 tangu kuanzishwa kwake Mei 1963 mjini Addis Ababa, Ethiopia. Sumatra yajipanga kudhibiti ajali za majini Katika kupunguza ajali za majini, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) iko mbioni kuandaa kanuni za usalama na vyombo vya majini zitakazotumika kwa wamiliki wa meli na wafanyakazi wake pindi wanapokuwa kazini. Wakiwasilisha rasimu hiyo kwa wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano huo jana jijini Dar es Salaam, aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Bernald Mbakileki, alisema mojawapo ya kanuni hizo zinaeleza kuwa mfanyakazi wa meli pindi anapokuwa amekiuka taratibu atanyang’anywa cheti chake au kusimamishwa kazi na Sumatra. Alifafanua kuwa kuna badhi ya vifungu vitafanyiwa marekebisho ikiwamo kinachoelezea rufaa kupelekwa kwa waziri husika huku sheria mama inaeleza rufaa itapelekwa katika Mahakama Kuu. Alisema endapo ajali yoyote itakapotokea au nahodha kufanya kosa lolote pindi anapokuwa kazini, cheti chake cha kazi kitasimamishwa au kufutwa. Alifafanua kuwa lengo kubwa la kuanzisha sheria hizo ni kuondokana na ajali za vyombo vinavyotumia usafiri wa majini. Baadhi ya wadau waliotoa maoni yao walisema kunatakiwa kuwapo vipengele vya sheria vitakazofafanua kuwapo kwa adhabu kali kwa yeyote atakayebainika amefanya kosa la kizembe. Naye Msajili wa Meli na Mkurugenzi wa usalama wa vyombo vya majini, King Chiragi, alisema sheria hizo zitakazotungwa zitatumika katika upande wa Bara peke yake. Alisema Sumatra imejizatiti kupumguza ajali zitokeazo majini kwa kutengeneza sheria mbalimbali. “Zanzibar wana sheria zao na sisi huku tunasheria zetu, lakini tunajitahidi kufanya kazi kwa pamoja ili sheria hizo zisipishane sana,” alisema Chiragi. Baadhi ya wadau walihudhuria mkutano huo ni Kamandi ya Kikosi cha Wanamaji (Nev), Polisi, kampuni ya usafirishaji wa meli na vivuko vya majini, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Wizara ya Uchukuzi, Ikulu,Zanzibar, Wizara ya Sheria na Katiba, Ofisi ya MwanasheriaMkuu. JWTZ waituliza Mtwara UWAMUZI wa Serikali kupeleka askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mkoani Mtwara kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kukabiliana na wimbi la vurugu, zimeanza kuzaa matunda. Matunda hayo yalianza kuonekana mapema jana askari hao walipoanza kupita katika mitaa mbalimbali ya mji wa Mtwara, ambao juzi uligeuka uwanja wa vita. Katika vurugu za juzi, polisi walilazimika kutumia risasi za moto, mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kukabiliana na wananchi ambao waliamua kujichukulia sheria mkononi kwa kufanya vurugu na kusababisha uharibifu mkubwa. Lakini jana askari wa JWTZ, walionekana katika mitaa ya Mnarani, Shangani, Sokoni, eneo la Stendi Kuu ya Mabasi na Bima. Wakati wote ambao askari hao walipita katika maeneo hayo, walikuwa watulivu na hawakuchukua hatua zozote za kukamata mtu, jambo ambalo lilionekana kupokelewa kwa furaha na wananchi. Jukwaa la Wahariri lalaani vurugu Mtwara JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limelaani vurugu za wananchi zilizotokea mkoani Mtwara na kusababisha vifo na uharibufu mkubwa wa mali za Serikali. Pia limesema baadhi ya habari zinazoandikwa kwenye magazeti na kutangazwa kwenye redio na televisheni zinachangia kuchochea na kuibua vurugu. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga, alisema licha ya wananchi na maoni yao ya msingi juu ya gesi, lakini njia wanayotumiwa kudai haki hiyo sio sahihi. Alisema TEF, imelazimika kukutana kwa dharura kutokana na vurugu hizo ili kupitia nafasi yao wana uwezo wa kusaidia kwa namna moja au nyingi kuwatuliza wananchi wakati Serikali ikiendelea kusikiliza maoni yao. “Vurugu kama hizi zikiendelea kule Mtwara, baadhi ya makundi ndani ya jamii hayawezi kuishi salama na shughuli za kimaendeleo na uchumi zitasimama. “TEF tuna imani na uwezo wa Serikali, itamaliza tofauti zao na wananchi na kuepusha vurugu zinazohatariusha usalama wa raia na mali zao, sisi hatuungi mkoni vitendo hivyo na tunawasihi wananchi kutumia njia mbadala ya kudai haki yao. “Kwa upande wa waandishi waliathirika na vurugu hizo kama kuchomewa nyumba na usalama wao tunaendelea kuwasiliana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na vyombo vingine vya usalama ili kuwapatia ulinzi. Alisema katika kikao hicho, wamebaini kuwa baadhi ya taarifa zilizokuwa zikiripotiwa juu ya gesi kwenye nyombo mbalimbali vya habari zilichangia kuchochea kuwapo vurugu hizo. “Ni kweli tumebaini baadhi ya habari tunazozipitisha kama wahariri zinachangia na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao ambapo tumeafikiana tusiliweke taifa hili katika hati ya sitofahamu na badala yake tubadilike na kuwahabarisha habari ya nzuri na zenye maadili. MTANZANIA Lukuvi: Wananchi wangu msidanganyike MBUNGE wa Isimani ambaye ni Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Willium Lukuvi amewataka wananchi wa jimbo lake kutodanganywa na watu wachache wanaotaka kupuuzia jitihada za serikali katika kuwaletea maendeleo jimboni humo. Badala yake, amewataka watumie fursa za kiuchumi zilizopo katika kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuondokana na umaskini. Akizungumza na wananchi hao katika kijiji cha Migoli, Lukuvi alisema yapo mambo mengi ambayo Serikali imeyafanya kwenye jimbo hilo ili kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na umaskini. Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni mchakato wa kuingiza umeme katika tarafa za Idodi na Pawaga ambako wanazalisha mpunga na kuuza kwa hasara, kufuatia wakulima hao kutokuwa na uwezo wa kuusindika baada ya kukosa nishati ya umeme. Alisema jambo jingine, ni ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma kwa kiwango cha lami ambayo imepita kwenye tarafa hiyo na kuihakikishia ukuaji wa kiuchumi kutokana na fursa nyingi zitakazokuwepo baada ya kukamilika. “Mnataka Serikali ifanyaje? Puuzieni maneno ya watu wanaotaka kutuvuruga na mfanye kazi kwa bidii kwani hizi ndizo fursa tulizokuwa tukiomba kupata miaka yote, mnachopaswa kufanya ni maandalizi ili barabara ikianze muanze kunufaika nayo kwa sababu mtaanza kupokea wageni wengi, ambao watahitaji huduma zenu,” alisema Lukuvi. Amvunja mguu mjukuu, kijiji chamfukuza WAKAZI wa Kijiji cha Lupeta kilichopo Mbeya Vijijini, wamemfukuza makazi mzee Shikunzi Mwasile (70), kwa tuhuma za kumvunja mguu mjukuu wake, Veronika Kabuka, kwa kosa la kuchuma mahindi mawili shambani. Wakitoa azimio hilo la mzee huyo kuondolewa kijijini hapo, licha ya Jeshi la Polisi kuingilia kati, baadhi ya wakazi hao walisema mzee huyo hawezi kuishi kijijini hapo, kwa kuwa tayari ana kumbukumbu ya matukio kadhaa ya kunyanyasa watu wengine. Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema chanzo cha mzee huyo kumpiga mjukuu wake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Swaya, kinatokana na kuchuma mahindi mawili shambani kwake bila ridhaa yake pamoja na kuharibu simu ya mkononi ya bibi yake, hali iliyosababisha kumfungia ndani na kuanza kumpiga. Walisema baada ya binti huyo kufungiwa ndani, alipigwa hadi kuvunjwa mguu, huku akitumia fimbo yenye miiba kwa kumchapa mwilini na kisha kumtelekeza ndani pasipo kumpeleka kupata matibabu na kusababisha damu kuvia. Aidha, walisema baada ya babu huyo kufanya tukio hilo, alimfuata mkewe na kumtisha kwamba asiseme chochote ambapo mama huyo inasemekana alifanikiwa kukimbia akiwa uchi kutokana na nguo zake kuchanika wakati wa mvutano. Walisema mama huyo alifika ofisi ya mtendaji na kueleza hali halisi iliyokuwa ikiendelea nyumbani kwake, huku akiwaomba kwenda kumchukua binti ambaye tayari mwili wake ulianza kudhoofika kutokana na kupoteza damu. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupeta, Baita Mwaipasi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na alitoa taarifa kwa polisi ambao walifika na kumkamata babu huyo kisha binti kufikishwa katika kituo cha afya cha matibabu katika Hospitali Teule ya Ifisi. Alisema Mei 21, 2013, aliitisha mkutano wa hadhara wa kujadili suala la mzee huyo, kwa kuwa alishapatiwa mdhamana na aliongozana na baadhi ya askari kwa ajili ya kumuombea msamaha aendelee kuishi kijijini hapo. Walisema mzee huyo hastahili kuishi na jamii ya kijiji hicho, kwa kuwa kitendo alichokifanya ni cha kikatili na tayari alishampotezea muda wa kusoma mwanafunzi huyo. MWANANCHI Wakandarasi walalamikia kukosa mitaji Wakandarasi nchini wanakabiliwa na tatkubwa la ukosefu wa mitaji, jambo linalosababisha washindwe kupata kazi za miradi mikubwa. Matokeo yake, ni miradi hiyo kuchukuliwa na kampuni za nje. Akizungumza katika mkutano wa kujadili matatizo na mafanikio ya Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) katika kipindi cha miaka 15 ya uhai wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Boniface Muhegi alisema mitaji ni tatizo kubwa kwa wakandarasi nchini. Alisema “kushindwa kupata zabuni katika miradi mikubwa, kunawafanya wakandarasi wasipigie hatua za kimaendeleo.” Alisema hata hivyo wataliwasilisha suala hilo kwa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, leo. Waitaka CCM kubatilisha kumvua uanachama diwani Wananchi wa Kata ya Mbebe, wilayani Ileje, wamekijia juu Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani humo, wakipinga kitendo cha kumvua uanachama diwani wa kata hiyo, Ambilikile Kamendu. Inadaiwa kuwa Diwani Kamendu aliandikiwa barua na uongozi wa CCM wa Wilaya ya Ileje ya kumsimamisha kuhudhuria vikao vyote vya kichama na Serikali kwa kile kinachoelezwa kuwa ana madeni mengi kutoka kwa watu , jambo linalokichafua chama hicho. Wakizungumza na Mwananchi mjini hapa, bila kujali itikadi za vyama vyao, wananchi hao wamesema uamuzi wa CCM kumvua uanachama diwani wao na kumfanya apoteze sifa za kuwa diwani bila kuwashirikisha wananchi waliomchagua, haukubaliki. Mmoja wa wananchi hao, Martin Mbotwa alisema wananchi hawana taarifa zozote kuhusu tuhuma zinazotolewa na viongozi wa CCM dhidi ya diwani wao Obama ‘afunga’ hoteli katikati ya jiji Wakati Rais wa Marekani, Barrack Obama akitarajiwa kuwasili na msafara wa watu 700, baadhi ya hoteli zenye hadhi ya nyota tano jijini Dar es Salaam zimeanza kusitisha kupokea wageni kutokana na ujio huo. Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani ilisema Rais huyo, anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi kwa ajili ya ziara ya siku tatu hadi Julai 3 mwaka huu ili kuimarisha uhusiano baina ya nchi hiyo pamoja na nchi za Afrika. Msafara huo utajumuisha watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara. Akizungumzia ziara hiyo jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema tayari timu ya kwanza imewasili nchini kwa ajili ya maandalizi mbalimbali. Hoteli zasitisha upokeaji wageni Gazeti hili lilifanya uchunguzi katika hoteli mbalimbali zenye hadhi ya nyota tano ambazo mara nyingi viongozi wakuu wa nchi mbalimbali huzitumia pindi wanapofika nchini. Hoteli hizo zilizoko katikati ya jiji zimechukuliwa kuanzia Juni Mosi hadi Julai 5. Uchunguzi huo umebaini kuwa,wageni waliochukua nafasi katika hoteli hizo wataanza kufika kati ya Juni 25 na kuondoka Julai 5. Mpaka sasa hali ya usalama katika hoteli hizo umeimarishwa ili kuhakikisha kuwa wateja wanaowasili katika maeneo hayo wanaishi katika mazingira salama. Serikali yawanyooshea kidole wanasiasa Serikali imesema kwamba imebaini kuwa baadhi ya wanasiasa na taasisi za kiraia wanahusika katika kuhamasisha vurugu zinazoendelea mjini Mtwara. Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alirejea kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba Serikali itawasaka watu wote wanaohusika na vurugu hizo ndani na nje ya nchi bila kujali umaarufu na madaraka yao. Alisema Serikali inalaani vikali vurugu hizo akisema wanaozihamasisha “wataipasua nchi, watasababisha vifo vya maelfu ya watu, watajaza taifa vilema na majeruhi na hawatanufaika na matokeo haya mabaya.” Dk Nchimbi alisisitiza msimamo wa Serikali kwamba maliasili hiyo ni ya Watanzania wote... “Tunalo taifa moja la Tanzania ambalo maliasili zake ni za Watanzania wote. Tabia inayoanza kujengeka ya kila eneo kutaka linufaike peke yake na mali za eneo hilo, italigawa taifa letu vipandevipande.” Alisema kiini cha vurugu hizo ni madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam. Alisema Mei 15, mwaka huu kikundi cha watu kilisambaza vipeperushi kuwataka wananchi wa huko Mei 17, saa 3:00 asubuhi kuacha shughuli na kusikiliza hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kujua mustakabali wa gesi kusafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Alisema juzi, makundi ya vijana yalisikiliza hotuba hiyo maeneo mbalimbali ya Mtwara kama vile sokoni, Magomeni, Mkanaredi na baadaye kupanga mawe na magogo barabarani huku wakichoma matairi. “Hali hiyo iliendelea kusambaa maeneo mengine ya mji kama vile Chuno, Chikongola, Mikindani na kutoka nje ya mji hadi Mpapura, umbali wa kilomita 40 kutoka Mtwara mjini,” alisema. Alisema polisi walikabiliana na vurugu hizo na hadi jana, watu 91 walikuwa wanashikiliwa. JWTZ wakanusha taarifa za askari kujihusisha na makahaba DRC Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ, limekanusha taarifa zilizotapakaa kwenye mitandao kuwa askari wa jeshi hilo waliokwenda huko kwa ajili ya kulinda amani,wameanza kujihusisha na makahaba. Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Mtandao wa congodrcnews wanajeshi wa Tanzania wameanza kujihusisha na ubakaji wanawake katika Mji wa Sake ulioko Goma. Taarifa hizo zimeeleza kuwa askari mmoja wa JWTZ alihitaji kujamiiana na mwanamke mmoja(Kahaba) kwa ujira wa Dola 50. Baada ya kumaliza shida zake ambazo ilielezwa alizifanya bila kinga yoyote,askari huyo alikataa kumlipa ujira wake,hali iliyoleta tafrani na mwanamke huyo kupiga kelele. “JWTZ linapenda kuwaeleza wananchi kuwa taarifa hizo ni za uongo mtupu wenye nia ya kulipaka matope JWTZ na Tanzania kwa ujumla. “Picha iliyotolewa kwenye tovuti hiyo ya congodrcnews ni ya wanajeshi wa Tanzania walipokuwa katika Operesheni ya huko Comoro mwaka 2008. Mtu anayeonekana kuwa chini ya Ulinzi alikuwa ni mshiriki wa Kanali Mohamed Bacar ambaye aliondolewa madarakani. Taarifa hiyo ilisema kuwa JWTZ inapenda kueleza wananchi na dunia kwa ujumla kwamba wanaoneza taarifa hizo wana lengo la kukatisha tamaa juhudi zinazofanywa na Nchi za Maziwa Makuu na SADC kuleta amani nchini DRC kwani JWTZ wako DRC kwa mujibu wa taratibu za kiutendaji za Umoja wa Mataifa. Uzazi wa mpango, uchumi na majukumu ya mama Tanzania Kuruthumu Said, 31, mkazi wa Mbande Manispaa ya Temeke, ni mama wa watoto wanne; wawili wa kike na wawili wa kiume. Mama huyu ambaye ni mjamzito, anasema hafanyi kazi yoyote zaidi ya kuangalia familia yake nyumbani wakati mume wake akifanya kazi ya kushona viatu kwa ajili ya kujipatia kipato. Anasema pamoja na kazi hiyo ya mumewe bado hali yao ya uchumi ni duni,kiasi cha kushindwa kupata Sh2,000 za kuanzia huduma ya kiliniki ya mama mjamzito, hivyo hatambui umri wa ujauzito alionao. Kuruthumu anasema alijifungua mtoto wake wa kwanza mwaka 2002 na wapili mwaka 2004. Alianza kutumia njia ya uzazi wa mpango mwaka 2007 baada ya kupata mtoto wa tatu. Anasema alichagua njia ya sindano, ambayo aliitumia kwa miaka miwili kabla ya kuiacha baada ya kupata madhara ya kiafya. Ingawa anatarajia kujifungua mtoto wake wa tano hivi karibuni, anasema hafahamu idadi ya watoto anaotarajia kuwa nao. “Kila mtoto huja na riziki yake, nitakapojifungua mtoto wa tano ndio nitafikiria kuhusu idadi ya watoto ninaowataka,” anasema. Pamoja na kuwa na mpango wa kuendelea kuzaa watoto wengine, Kuruthumu anasema watoto alionao wameanza kumwelemea kwa kushindwa kuwapa mahitaji yao. “Mara nyingi tunalala na njaa kwa kukosa chakula, mtoto mmoja nimeamua kumpeleka kwa shangazi yake ili apate msaada,” anasema. Anaongeza kuwa hajapata elimu ya kutosha kuhusiana na njia nyingine za uzazi wa mpango, kwani mara nyingi elimu hiyo hutolewa katika machapisho na majarida jambo ambalo ni kikwazo kwake kwasababu hajui kusoma na kuandika. Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo zina viwango vya juu vya vifo vya wanawake vitokanavyo na matatizo ya uzazi. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka 2010 na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) karibu wanawake 20 hufariki kila siku kutokana na matatizo hayo. Kutokana na hali hiyo nchi imejiwekea malengo ya kupunguza kiwango cha vifo kutoka 454 kwa kila wanawake 100,000 hadi 193 ifikapo mwaka 2015. Mikakati kadhaa imewekwa kufikia malengo hayo; kuongeza matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango ili yafikie asilimia 60, ambapo kwa sasa ni asilimia 27 tu ya wanawake walioolewa ndio wanatumia. HABARI LEO Achoma zahanati kwa wivu wa mapenzi SEHEMU ya jengo la Zahanati ya Digarama katika Wilaya ya Mvomero, imechomwa moto na mtu anayedaiwa kufanya hivyo kutokana na wivu wa mapenzi. Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, wanadai aliyechoma chumba kimojawapo cha zahanati hiyo, amefanya hivyo kutokana na sababu za kimapenzi. Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mkata aliyefanya mkutano wa hadhara na wanakijiji, baadhi yao walisimama na kudai aliyefanya kitendo hicho anadai mkewe alikuwa akifanya mapenzi na mkazi mmoja katika jengo hilo lililokuwa katika hatua za mwisho za kukamilika ili lianze kutumika. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, amethibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa, mtu mmoja anahojiwa. Hakutaja jina la mtuhumiwa wala kuthibitisha kama ndiye anayetuhumiwa na wanakijiji, Kamanda Shilogile alisema atafanya hivyo uchunguzi utakapokamilika. Imeelezwa kuwa, kama si wanakijiji kuwahi kuuzima moto ulioteketeza mbao na madirisha yote katika chumba hicho, jengo zima la zahanati hiyo lingeteketea. Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mkata, ameviamuru vyombo vya ulinzi wilayani humo kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Digarama kumsaka aliyefanya kitendo hicho. Zahanati hiyo inatajwa kuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Digarama na vijiji jirani kutokana na kuwa mbali na Hospitali Teule ya Bwagara. Ujenzi wa zahanati hiyo ulikuwa umekamilika kwa asilimia kubwa ikisubiriwa kufunguliwa hivi karibuni. Mkuu wa Wilaya alikutana juzi na wanakijiji na kutoa maagizo hayo. Jengo hilo la zahanati lilichomwa usiku wa Mei 19. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya chini yake, ikiongozana na watendaji wa Idara ya Afya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, ilifika kijijini hapo na kuitisha mkutano wa hadhara wa wananchi kulizungumzia jambo hilo. “Moto uliotokea kwenye zahanati haukuwa wa bahati mbaya, bali ni wa makusudi uliotokana na mtu mwenye sababu zake binafsi kutaka kuteketeza kabisa Zahanati ya Kijiji cha Digarama,” alisema Mkuu wa Wilaya. Katika mkutano huo, wananchi walielezwa faida ya zahanati na kuomba ushirikiano wa wanakijiji kubaini mhusika ili akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya , Mkata, Serikali ilitenga Sh milioni 10 kwa ajili ya ukamilishaji wa hatua za mwisho kabla ya kuifungua kuwaondolea adha ya muda mrefu waliyokuwa nayo kutokana na kukosa zahanati. Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi walitokwa machozi. Walidai kwa muda mrefu wamekuwa wakisafiri umbali wa zaidi ya kilometa 20 kwenda Hospitali ya Bwagara JAMBO LEO Taboa wapinga Noah kubeba abiria WABUNGE wameombwa kupitia upya uamuzi wao wa kuruhusu magari aina ya Noah kubebea abiria. Wamesema pia huenda Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepewa ushauri ambao hakuwa sahihi kuhusu usafiri huo. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani Tanzania (Taboa), Enea Mrutu, alisema ni vema uamuzi huo ukapitiwa upya ili kujiridhisha kama ushauri ulikuwa mzuri wa kuruhusu Noah kubeba abiria. “Tunaamini uamuzi huu wa kuruhusu Noah kubeba abiria hakufanyiwa utafiti wa kutosha. Tunaomba waziri na wabunge watafakari kwa kina katika hili, maana badala ya kuleta faraja unaweza kuleta machungu kwa abiria,” alisema Mrutu. Alifafanua kuwa Noah inatakiwa kubeba abiria wasiozidi saba, lakini kwa bahati mbaya, magari hayo yanabeba idadi kubwa kuliko uwezo wake na wanafanya hivyo ili kukwepa hasara. Alisema kuwa Taboa hawana ubaya na wasafirishaji wala kupinga uamuzi wa serikali, lakini kuna haja ya kuangalia uamuzi huo kwa undani kwani hakuna mmilikiwa wa Noah ambaye yupo tayari kuendesha biashara hiyo kwa hasara. Mrutu alisema, Noah zimekuwa zikitoza nauli tofauti na ile iliyopangwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), na kutoa mfano kuwa nauli ya kutoka Handeni kwenda Korogwe ni sh. 4,000, lakini magari hayo yanatoza sh. 5,000. Pia wanafunzi wanakuwa katika wakati mgumu kusafiri na magari hayo. Taboa wapinga Noah kubeba abiria WABUNGE wameombwa kupitia upya uamuzi wao wa kuruhusu magari aina ya Noah kubebea abiria. Wamesema pia huenda Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepewa ushauri ambao hakuwa sahihi kuhusu usafiri huo. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani Tanzania (Taboa), Enea Mrutu, alisema ni vema uamuzi huo ukapitiwa upya ili kujiridhisha kama ushauri ulikuwa mzuri wa kuruhusu Noah kubeba abiria. “Tunaamini uamuzi huu wa kuruhusu Noah kubeba abiria hakufanyiwa utafiti wa kutosha. Tunaomba waziri na wabunge watafakari kwa kina katika hili, maana badala ya kuleta faraja unaweza kuleta machungu kwa abiria,” alisema Mrutu. Alifafanua kuwa Noah inatakiwa kubeba abiria wasiozidi saba, lakini kwa bahati mbaya, magari hayo yanabeba idadi kubwa kuliko uwezo wake na wanafanya hivyo ili kukwepa hasara. Alisema kuwa Taboa hawana ubaya na wasafirishaji wala kupinga uamuzi wa serikali, lakini kuna haja ya kuangalia uamuzi huo kwa undani kwani hakuna mmilikiwa wa Noah ambaye yupo tayari kuendesha biashara hiyo kwa hasara. Mrutu alisema, Noah zimekuwa zikitoza nauli tofauti na ile iliyopangwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), na kutoa mfano kuwa nauli ya kutoka Handeni kwenda Korogwe ni sh. 4,000, lakini magari hayo yanatoza sh. 5,000. Pia wanafunzi wanakuwa katika wakati mgumu kusafiri na magari hayo. HABARI ZA KIMATAIFA NAIROBI Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto wametajwa katika ripoti inayowahusisha na ghasia za baada ya uchaguzi katika ripoti iliyosubiriwa kwa muda mrefu kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamau nchini humo. Ripoti hiyo hata hivyo haikutoa mapendekezo ya hatua inazotaka kuchukuliwa dhidi ya Rais Kenyatta na makamu wake, William Ruto. Mwenyekiti wa tume hiyo, aliiambia BBC kuwa ni kwa sababu wawili hao wanakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC. Tume ya maridhiano na haki ilikabidhiwa jukumu la kuchunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa tangu mwaka 1963 nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake. Iliundwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/08 uliozua ghasia miaka mitano iliyopita kama njia ya kuleta maridhiano miongoni mwa wakenya. Baada ya uchaguzi huo, watu 1,500 waliuawa na wengine zaidi ya 600,000 kulazimika kukimbia kutoka katika makazi yao. Kenyatta na Ruto, waliokuwa mahasimu katika uchaguzi wa mwaka 2007, walishinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Machi baada ya kuungana chini ya Muungano wa Jubilee. Licha ya kuwa hakuna mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo dhidi ya Rais na naibu wake, inapendekeza uchunguzi zaidi dhidi ya maofisa wakuu waliotajwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007 na hata kufunguliwa mashtaka Baadhi ya waliotajwa ni pamoja na Waziri mpya wa Madini, Najib Balala na maseneta wawili. Hata hivyo tume hiyo ilimtaka Rais Kenyatta kuwaomba radhi Wakenya kwa makosa waliyotendewa chini ya Serikali zilizopita katika kipindi cha miezi sita tangu kukabidhiwa ripoti hiyo juzi. Rais mstaafu Daniel arap Moi pia alitajwa katika ripoti hiyo akihusishwa na mauaji ya waliokuwa wanasiasa mashuhuri wakati wa utawala wake. NEW YORK Rais Obama ametetea sera ya matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani katika kile alichokiita vita halali. Katika hotuba muhimu aliyoitoa kwenye chuo kikuu cha ulinzi wa taifa cha Washington, Obama alisema matumizi ya ndege hizo yameifanya Marekani iwe salama zaidi. Hata hivyo amesisitiza kwamba inapasa kuhakikisha kuwa katika matumizi ya ndege hizo hakuna raia anaeudhurika. Rais Obama pia amesema utawala wake upo tayari kukubali udhibiti zaidi wa mashambulio yanayofanywa na ndege zisizokuwa na rubani, nje ya maeneo ya vita kama Afghanistan. Amesema Marekani ipo vitani dhidi ya kundi ambalo lingewaua Wamarekani wengi kwa kadri ambavyo ingeliwezekana ,laiti hatua zisingelichukuliwa kwanza kulizuia kundi hilo. Juu ya juhudi za kuifunga jela ya Guantanamo, Rais Obama alifahamisha kuwa Marekani imeiondoa hatua ya kuusimamisha kwa muda, mpango wa kuwahamisha wafungwa na kuwapeleka Yemen. Katika hotuba yake kwenye chuo kikuu cha ulinzi wa taifa mjini Washington, Obama aliwaambia Wamarekani kwamba jela ya Guantanamo imegeuka kuwa ishara duniani kote, inayoonyesha jinsi Marekani inavyokiuka sheria. London Wizara ya ulinzi nchini Uingereza imemtaja mwanajeshi alieuawa mjini London kwa kukatwa visu na mapanga ,kuwa ni Lee Rigby aleikuwa na umri wa miaka 25 na aliekuwa mwenyeji wa Manchester. Kutokana na habari za kifo cha kutisha cha askari huyo,kufahamika zaidi na wananchi, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ametoa mwito wa kuwepo umoja. Amesema watu waliokifanya kitendo cha mauaji wanajaribu kuwagawanya Waingereza. Askari alieuawa,Lee Rigby alijunga na jeshi la Uingereza mnamo mwaka wa 2006 na alilitumikia jeshi hilo nchini Cyprus na Afghanistan. Watu wanaotuhumiwa kumuua mwanajeshi huyo ni waingereza wenye asili ya Nigeria ambao sasa wapo kwenye hospitali tofauti chini ya ulinzi wa maafisa wenye silaha. Irak Watu waliokuwa na silaha wamewaua wanajeshi wapatao saba nchini Irak, katika mfululizo wa matukio ya umwagaji damu ya hivi karibuni. Kwanza watu hao walikishambulia kituo cha udhibiti cha kijeshi, katika mji wa kati wa Taji. Wanajeshi wanne waliuawa katika shambulio hilo na wengine wanne walijeruhiwa.Kundi lingine la wapiganaji lilipambana na wanajeshi na wanamgambo wa kisuni wanaoiunga mkono serikali katika kijiji cha magharibi cha Karma karibu na mji wa Fallujah. Katika kadhia hiyo askari watatu waliuawa na wengine 18 walijeruhiwa ikiwa pamoja na wapiganaji saba wa kisuni. Watu karibu mia tatu wameshauawa nchini Iraq mnamo kipindi cha siku 10 zilizopita ,kutokana na matukio ya umwagaji damu. Niger Watu 20 wameuawa kutokana na mashambulio yaliyofanywa na waislamu wenye itikadi kali nchini Niger kama hatua ya kulipiza kisasi ushiriki wa nchi hiyo kijeshi, katika mgogoro wa nchi jirani ya Mali. Washambuliaji hao waliyaripua mabomu mawili kwenye kituo cha kijeshi katika mji wa Agadez na kwenye mgodi wa madini ya uranium unaosimamiwa na Ufaransa katika mji wa kaskazini wa Arlit. Mabomu hayo yalikuwa yametegwa ndani ya gari. Wizara ya ulinzi ya Niger imesema mshambuliaji wa mwisho alinyamazishwa kwenye kambi ya kijeshi lakini imekanusha habari kwamba palikuwapo na mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliekua anawashikilia mateka,vijana waliokuwa wameandikishwa kuanza kazi jeshini. Wizara ya ulinzi ya Niger imeliambia shirika la habari la AFP kwamba washambuliaji wote wamenyamazishwa na mapambano yamekwisha. Kundi linaloitwa Mujao,ambalo ni tawi la mtandao wa al-Kaida katika Afrika magharibi limedai kuhusika na mashambulio hayo. GENEVA. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema dunia inakabiliwa na tishio jipya kiafya baada ya kuzuka kwa virusi waitwao novel corona. Virusi hao huweza kuambukiza kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kwa kugusana ama kukaribiana. Taarifa hiyo ya Jumapili, Mei 12 imekuja baada ya Waziri wa Afya wa Ufaransa, Marisol Touraine kuthibitisha tukio la kuambikizwa kwa mtu wa pili kwa virusi hao nchini mwake. Nchini Saudia Arabia, imethibitishwa pia kutokea kwa vifo vya watu wawili kutokana na aina hii ya virusi. Kwa mujibu wa WHO, virusi vya aina ya novel corona hushambulia zaidi mfumo wa hewa na pia kuathiri figo na kulisababisha lishindwe kufanya kazi zake vizuri. WHO, inaeleza kuwa haja ya jamii kokote duniani kuchukua tahadhari mapema kutokana na kuzagaa kwa taarifa za kusambaa kwa aina hiyo mpya ya virusi. Kuanzia mwaka jana, 2012 , wagonjwa 34 waliogundulika kuwa na virusi hivi vipya vya novel corona wameripotiwa katika nchi za Ulaya, Mashariki ya Kati, huku wengine 18 wakithibitishwa kufa. Wagonjwa waligundulika zaidi Saudi Arabia na Jordan na kuenea kwa virui hao katika nchi za Ulaya, hasa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa. ‘Kuwapo kwa taarifa katika nchi mbalimbali unaweza kutupa uthibitisho wa kile tunachodhani kua virusi hivi vinaweza kuambukizwa kwa njia ya kukaribiana ama kugusana kutoka mtu mmoja kwenda mwingine, hivyo, tuchukue tahadhari,’ inasema WHO. “Jambo la msingi ni kuweza kufahamu chanzo na namna mwanadamu anvyoweza kuambukizwa katika hatua za mwanzo, vinginevyo ni ngumu kudhibiti tatizo hili,” anaeleza Gregory Hartl wa WHO katika taarifa yake ya Jumapili, Mei 12. “Uambukizi wa virusi hawa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine unabaki kwa kundi dogo tu kwani mpaka sasa haijathibitika kama je ugonjwa huu unaweza kuambukiza na kusambaa kwa wingi katika jamii yetu,” anaeleza Hartl. Kulingana na WHO, mgonjwa wa pili mwenye umri wa miaka 50 alithibika kuwa na virusi vya corona katika mji mdogo wa Vennence, Kaskazini mwa Ufaransa NA HUO NDIO MWISHO WA HABARI ZA KIMATAIFA KUTOKA ILASI FM
Posted on: Fri, 24 May 2013 13:34:28 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015