Namna ya kutoa Zakaah ya Biashara Mwenye kumiliki mali ya biashara - TopicsExpress



          

Namna ya kutoa Zakaah ya Biashara Mwenye kumiliki mali ya biashara iliyofikia Niswabu, akishakamilisha mwaka anatakiwa ahesabu mali yake yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya biashara. Kama ni mfaya biashara wa nyumba, basi azihesabu nyumba zake (zile tu alizozitayarisha kwa ajili ya biashara), au ardhi au vyombo vya nyumbani, magari au nguo au biashara ya aina yoyote ile. Atavihesabu vitu alivyokuwa navyo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzihesabu pesa zote alizonazo kwa ajili ya biashara kisha atazitolea Zakaah yake, nayo ni mbili unusu katika mia au moja katika arubaini. Atafanya hesabu hiyo bila kujali kama wakati wowote ule ndani ya mwaka ule pesa hizo zilipungua au kuongezeka. Kumbuka Ikumbukwe kuwa vitakavyohesabiwa ni vitu vilivyotayarishwa kwa ajili ya biashara tu. Kwa mfano mtu anamiliki magari hata yakifikia idadi ya magari kumi au zaidi, au atataka kuuza gari lake mwenyewe kwa ajili ya kulibadilisha tu na kununua gari jengine au ardhi au nyumba au chochote kile, ikiwa anataka kuuza kwa ajili ya kutaka kununua kingine badala yake au kwa ajili ya mahitajio mengine yasiyokuwa ya kibiashara, basi mali hiyo haitolei Zakaah ya biashara, na hii ni kwa sababu nia ya kuviuza vitu hivyo si kwa ajili ya biashara. Kumbuka pia kuwa Zakaah inatolewa kutokana na asili ya chochote kilichoongezeka kutokana mali hiyo wakati wowote ule katika mwaka. Ama kile kilichoongezeka kutokana na asili nyingine, basi mwaka wake unaanza kuhesabiwa kuanzia siku ile iliyoongezeka mali hiyo. Kwa mfano; Mfanya biashara alikuwa akiendela kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha Shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa mwisho au hata katika siku ya mwisho kabla ya kutimia mwaka, akapata faida kiasi cha Shilingi laki saba, pesa zote hizo ZITAHESABIWA pamoja na Zakaah ya biashara ya mwaka huo, kwa sababu asili yake (faida iliyopatikana) inatokana na biashara hiyo anayoitolea Zakaah. Mfano mwingine: Mfanya biashara alikuwa akiendelea kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa kumi na mbili au katika siku ya mwisho au siku yoyote ile ya mwaka huo kabla ya kuingia muda wa kulipa Zakaah ya mwaka ule, mtu huyo akarithi pesa kutoka kwa jamaa yake aliyefariki kiasi cha Shilingi milioni moja. Pesa hizo alizorithi HAZITOHESABIWA katika Zakaah ya mwaka huo, bali ataanza kuzihesabia mwaka wake mpya kuanzia siku ile alizozipata pesa hizo. Kwa sababu asili ya pesa hizo hazitokani na biashara ile anayoitolea Zakaah, bali inatokana na asili nyingine, ambayo ni urithi. Inaendela insha Allah
Posted on: Thu, 01 Aug 2013 12:11:01 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015