RIWAYA: BARUA KUTOKA JELA MTUNZI: Ibrahim GAMA SEHEMU YA KUMI NA - TopicsExpress



          

RIWAYA: BARUA KUTOKA JELA MTUNZI: Ibrahim GAMA SEHEMU YA KUMI NA TANO Sajenti Kubuta sasa akawa kama mtu aliepagawa vile. Akaangalia maeneo yote ya jirani na Baa ile lakini mambo yalikuwa kama anavyoyaona, hakuna gari ya Inspekta Jamila, wala yeye mwenyewe! Ikambidi akate shauri. Mara akaona kundi la watu wanawake kwa wanaume, wakikimbia katika barabara ya Uhuru kuelekea upande wa kulia kule kwenye taa za kuongozea magari pale Buguruni sheli. Sajenti Kubuta akiwa anatafakari, ukasikika mlio wa Risasi! Na sasa akaona watu wengi zaidi wakikimbilia kule kulikosikika mlio wa Risasi! ******* Inspekta Jamila akiwa ametulia ndani ya gari pale nje kwenye Baa ile ya Y2K pale Buguruni, alivutiwa sana na yule Ombaomba! Kwani alipokwenda kwenye meza iliyokuwa na kinywaji cha Dokta Masawe, hakuonesha mkono kama ishara ya kuomba pesa, aliyokuwa anaifanya katika meza za watu wengine! Inspekta Jamila alimuona yule Ombaomba akimtazama kwa makini Dokta Masawe, na kisha kichwa cha yule Ombaomba kililazwa upande kidogo sana, kikielekeza upande wa uwani wa Baa ile! Baada ya kufanya vile, yule Ombaomba akaelekea uwani mwa Baa ile, na katika muda usiozidi dakika mbili Dokta Masawe alifanya ishara iliyoashiria kwamba anataka kwenda chooni. Inspekta Jamila moyo ulimripuka ripu, na damu yake ikaanza kuchemka! Huku mapigo ya moyo yakiongeza kasi katika mapigo yake! Inspekta Jamila akiwa mle ndani ya gari alimshuhudia Sajenti Kubuta, akimruhusu Dokta Masawe aende chooni. Na Dokta Masawe akaelekea uwani mwa Baa ile ambapo vyoo vyake ndipo vilipokuwa. Inspekta Jamila akaongeza umakini mara dufu, na hapo akamuona Koplo Michael Chazza, aliekuwa ameshika mti maalum wa kuchezea mchezo wa pool Table, akiuweka ule mti pale juu ya meza na kuelekea uwani sanjari na Dokta Masawe. Na baada ya kama dakika tano hivi, Inspekta Jamila alimuona yule Ombaomba akitoka na kuondoka zake eneo lile akiifata ile barabara ya Uhuru kwa mwendo wa haraka kidogo! Inspekta Jamila alimshuhudia yule Ombaomba akiipita gari aliyokuwemo yeye mle ndani, na aliporudisha macho yake kule kwenye Baa ya Y2K Dokta Masawe alikuwa bado hajarudi katika meza yake! Kitendo bila kuchelewa, Inspekta Jamila aliwasha gari nakumfatilia yule Ombaomba kwa mwendo wa taratibu. yule Ombaomba alikuwa ameshachanganya mwendo, na sasa alikuwa ameshaikaribia ile barabara ya Uhuru, akageuka nyuma kutazama kule kwenye Baa ya Y2K, huku akiwa anatembea kwa mwendo wa haraka, akaiona gari ndogo yenye vioo vya kiza ikija taratibu. Hamadi! Yule ombaomba akagongana na Dada mmoja hivi aliekuwa anaelekea kule wenye bar ya Y2K. Yule Ombaomba akakutanisha viganja vyake vya mikono kifuani kwake, na kuinama kidogo kama ishara yakumtaka radhi yule dada aliegongana nae. Lakini yule dada badala yakupokea samahani ile, alitoa msonyo mrefu kisha akashika Hamsini zake. Yule Ombaomba akapinda kulia kuelekea Buguruni Sheli. Inspekta Jamila alipofika pale kwenye barabara ya Uhuru alisimama na kumfatilia kwa macho yule Ombaomba aliekuwa anazidisha hatua. Inspekta Jamila akaiingiza gari katika barabara ya Uhuru akapinda kulia katika ile barabara inayoelekea Buguruni Sheli, huku macho yake yakiwa hayampotezi yule Ombaomba. Yule Ombaomba alikuwa nae akiitazama ile gari ya Inspekta Jamila kwa makini na kituo, ambayo sasa alikuwa nayo sanjari yeye akiwa upande wa kulia katika njia ya watembea kwa miguu, na ile gari ikiwa upande wa kushoto katika njia ya gari kwenye ile barabara ya Uhuru. Yule Ombaomba mara akasimama ghafla na kuingia katika duka moja la kuuza Vipuri vya magari, lakini pia akitaka kuthibitisha kwamba ile gari ilikuwa inamfata yeye au ilikuwa na safari zake! Akiwa pale dukani aliishuhudia ile gari ikiegeshwa pembeni, na hata baada ya kuegeshwa kulikuwa hakuna mtu alietelemka kutoka katika gari ile, wala aliepanda! Yule Ombaomba akiwa anabawabu muelekeo, mara akaja Bwana mmoja akiwa na pikipiki aina ya Honda 750 GL, akashuka na kutaka kuingia dukani mle. Kilifanywa kitendo ambacho hata Inspekta Jamila hakukitarajia kama kingeweza kufanyika, tena kwa wepesi wa ajabu namna ile! Yule Ombaomba aliingiza mikono mifukoni mwake, alipoitoa mikono ile ilikuwa imekamata bastola iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti, na kuifanya bastola ile ionekane ndefu kiasi! Akamnyooshea bastola ile yule bwana aliekuja na pikipiki, huku akimtaka ampe funguo za pikipiki ile bila ya kuchelewa, na yule bwana aliekuja na pikipiki huku akigwaya kwa kitendo cha kuonyeshewa silaha ya moto namna ile, alimrushia zile funguo yule Ombaomba ambae kwake yule bwana mwenye ile pikipiki alimuona kama mtu mzima aliechanganyikiwa, Lakini pia dhalili na masikini wa kutupwa! Yule Ombaomba alizidaka zile funguo na kuirukia ile pikipiki iliyokuwa inaangalia mjini, akaipiga stati na ile pikipiki bila hiyana, ikawaka ikisubiri safari! Yule Ombaomba bila kufanya ajizi, kitendo bila kuchelewa akaigeuza kwa kupiga msele pikipiki ile. Ikawa inatazama Buguruni Sheli! Kila mtu ambae ameiona ile pikipiki ilipogeuzwa angeamini kuwa ni pikipiki yake yule mzee namna alivyoimiliki. Aliingiza barabarani kiufundi katika barabara ile ya Uhuru akawa anatembelea barabara inayoruhusu kupita magari yanayotoka buguruni kwenda mjini! yaani alikuwa anatembelea barabara ‘NO ENTRY’ Bahati njema kwake ni kwamba, kulikuwa hakuna magari yanayokuja upande ule kwani taa za pale katika makutano ya barabara ya Uhuru na Mandela ilikuwa imeziruhusu gari kutoka Ilala kwenda Tabata, na usawa wa Tazara na hakukuwa na gari ilyokuwa inakata kuelekea Ilala. Inspekta Jamila alipoona kitendo kile nae akaiingiza gari barabarani katika mwendo uliowaacha hoi watu wote walioiona namna gari ile ikichimba huku ikitoa mlio wa tairi zilizokuwa zikisuguana na barabara, na kusababisha vumbi kubwa sana sehemu ile. Ikawa sasa upande wa kulia kulikuwa na pikipiki aina ya Honda 750 GL, na upande wa kushoto kulikuwa na gari aina ya Toyota Soluna XL zote kwa pamoja zikiiwahi sehemu ya maungio ya barabara ile pale kwenye kituo cha mafuta pale Buguruni. Pikipiki iliongwezwa mwendo kwa mkono, na gari iliongezwa mwendo kwa mguu! Kiasi kulikuwa hapatoshi eneo lile la Buguruni, kwani watu waliokuwa wanatokea Buguruni upande wa sokoni, na wale waliokuwa wanatokea upande wa Buguruni chama na kwa Mnyamani na kule upande wa sheli wote walikuwa wanakimbilia upande ule kulipotokea kizazaa cha pikipiki kelele zake lilipogeuzwa uelekeo, na kule kulipotokea kelele za gari alilokuwa anaendesha Inspekta Jamila. Kwa kweli ilikuwa ni hatari tupu kukimbilia jambo kama lile. Pikipiki ndiyo iliyowahi kufika katika maungio yale ikaingia, huku Inspekta Jamila akiwa amezuiliwa na gari iliyokuwa ikisuasua mbele yake, akaipita gari ile mkweche aina ya Datsun Nissan Old Model yakubebea mizigo, na sasa akawa yeye nyuma ya Pikipiki iliyokuwa imeibiwa na yule Ombaomba wa ajabu kwake! Mara Inspekta Jamila akamshuhudia yule Ombaomba akigeuza uso wake kumtazama, huku mkono wake wa kushoto ukiwa na bastola iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti isisikike {Silence} akimnyooshea pale upande wake usawa wa dereva. Mara akaona kidole kikigusa kile kifyatulio cha risasi {Trigger} Inspekta Jamila kitendo bila kuchelewa aliipeleka gari upande mwingine wa barabara ile kule kwa watembea kwa miguu ‘Service Road’ kwa haraka huku akibonyea mle ndani ya gari na kukanyaga Breki. Na wakati huohuo ikasikika mlio wa kuvunjika kioo cha gari iliyokuwa inasuasua iliyokuwa nyuma yake! Vipande vidogovidogo vya vioo, vikimwagika chini kwa kuwa chenga tupu! Yule Ombaomba alirusha risasi,aliyokuwa amemkusudia Inspekta Jamila, ila kwa kitendo cha yeye kukata kona ya ghafla na kutoka barabarani, risasi ile ikaipiga ile gari mkweche kwa bahati mbaya. Gari aliyokuwa anaendesha Inspekta Jamila ilikipanda kikuta cha barabara ya watembea kwa miguu, huku ikiwa inasota kwa sababu ya Breki za ghafla alizokanyaga, na gari iliposimama akafungua mlango haraka na kutoa bastola mgongoni mwake usawa wa kiuno. Huku mlango ule ukiwa umefunguliwa akaipitisha mikono yake katika uwazi wa mlango pale baina ya Flem ya mlango ule na mlango wenyewe, huku akiwa ameushusha mguu mmoja nje, na kuuacha mguu wake wa kushoto ndani ya gari ile, mikono yake miwili iliyoshika bastola ya kipolisi aina ya Rivolver akalenga shabaha kwa tabu kumlenga yule Ombaomba aliekuwa anakaribia kabisa kuingia katika barabara ile ya Mandela na kufyatua risasi moja. Mlio wa risasi ya silaha ya Inspekta Jamila ulisikika sehemu kubwa kwani bastola yake ilikuwa haina kiwambo cha kuzuia sauti. Yule Ombaomba ilimkosa risasi ile sentimita chache na ikaenda kupiga katika chuma cha ngao ya gari ya mizigo iliyokuwa inaelekea Ubungo na kutoa cheche za moto! Kwa ustadi mkubwa yule Ombaomba akaanza kuiendesha pikipiki ile katika mtindo wa Zigzaga na kuingia katika barabara ya Mandela, akakata kushoto kuelekea Tazara, na kumuacha Inspekta Jamila katika mataa ya Barabara ya Mandela na Uhuru! Inspekta Jamila sasa akiwa ameshuka chini nje ya gari, alilipiga teke tairi la gari kwa hasira! Huku akilaani msongamano wa watu na magari uliyokuwa katika eneo lile, kwani ndiyo uliomfanya asiendelee kurusha risasi nyingine akihofia kuuwa au kujeruhi raia wasiokuwa na hatia, lau kungelikuwa hakuna msongamano wa watu angeliendelea kumrushia risasi yule Zabania mpaka angemdondosha chini! Inspekta Jamila akakumbuka kwa kina Sajenti Kubuta, na akafikiri kuwa kwa vyovyote vile, kutakuwa kumetokea Zahma kubwa, kwani yule ombaomba alikuwa ni mtu hatari kuliko anavyoonekana! Inspekta Jamila akaingiza mkono wake mfukoni mwa suruali yake aina ya Kadeti na kutoa simu ili ampigie Sajenti Kubuta, kumwambia kilichoendelea, akaiona simu yake imezimika! “Shit jana sikuichaji simu, kwani umeme ulikatika na kurudi asubuhi.” Inspector Jamila alijisemea kimoyomoyo baada ya kugundua kuwa simu yake imezimika kwa kukosa chaji ya kutosha. Alijaribu kuiwasha na simu ikawa kama haikubonyezwa kitufe chochote, unaweza kuifananisha na ‘Toy!’ akakata shauri kurudi kule alipowaacha askari wenzake wakiwa na mualifu wao Dokta Masawe ili akajue kilichotokea. Inspekta Jamila akaingia ndani ya ile gari, na kabla hajaufunga mlango wa gari ile, alisikia sauti ya chuma aliyokuwa ameizoea masikioni mwake. Ilikuwa ni sauti ya chuma cha Bunduki aina ya SMG ‘Sub Mashene Gun’ ikikokiwa katika harakati za kupeleka risasi chemba tayari kwa kufyatuliwa wakati wowote! Na namna kilivyolia chuma kile, wakati silaha ile ilipokuwa inavuta risasi, akatambua kuwa silaha iliyokokiwa, imekokiwa katika mfumo wa kutoa risasi mfululizo {Basta / Rapid}na sio ule mfumo wa kutoa risasi mojamoja ‘Single Systim’ na mara akasikia sauti ya mtu ikimwambia “Upo chini ya ulinzi,shuka chini na usalimishe silaha yako!” Inspekta Jamila akashuka kutoka katika ile gari huku akitii amri ile kwa kuiweka chini silaha yake. Akawaona askari polisi wawili, waliokuwa wapo katika sare zao za jeshi la polisi. Askari mmoja akiwa ameshika Bunduki aina ya SMG, na askari wa pili alikuwa amekamata simu ya upepo ‘Radio call’. Eneo lile lililotokea kizaazaa, walikuwa wamejaa watu wengi sana. Yaani lilikuwa jambo la hatari sana sehemu iliyolia Bunduki watu badala ya kukimbia, kinyume chake wao wanakimbilia! Wakiwa hawawazi kwamba risasi inaweza kumkosa mlengwa ikampata raia asiekuwa na hatia, kwa sababu ya kiherehere na kimbelembele kilichowajaa! Ama kweli jambo usilo lijuwa ni kama usiku wa kiza! “Staf Sajenti, mimi ni askari nilikuwa napambana na Jambazi” Inspekta Jamila alikuwa anajitambulisha kwa wale askari, huku akiwaangalia usoni moja kwa moja. “Wewe ni askari kutoka katika kituo gani” Yule askari alieshika “Radio Call” mwenye cheo cha Staf Sajenti, katika bega lake,alimuuliza Inspekta Jamila. Kabla Inspekta Jamila hajajibu swali lile, Sajenti kubuta alitokea na alikuwa anawatambua askari wale! “Afande Majuto huyu ni askari mwenzetu, mwenye cheo cha Inspekta, anaitwa Inspekta Jamila, kutoka makao kakuu.” Sajenti Kubuta aliyasema maneno yale, Kumwambia Yule askari aliekuwa kiongozi katika doria ile, aliekuwa ameshika chombo cha mawasiliano, huku akiiokota ile silaha ya Inspekta Jamila pale chini, iliyokuwa imesalimishwa na kumkabidhi Inspekta Jamila. Wale askari wawili wakakakamaa na kutoa heshima ya utii kwa Inspekta Jamila. Inspekta Jamila alipokea heshima ile kwa moyo mkunjufu, kutoka kwa wale askari waliokuwa katika ulinzi wa kawaida wa jeshi la polisi, katika kila kwenye makutano ya barabara kubwa na kwenye taa za kuongozea magari. ITAENDELEA
Posted on: Wed, 02 Oct 2013 09:00:00 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015