RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA - TopicsExpress



          

RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA Hali hii ikawatia morali askari, wakajiaminisha kuwa Naomi anaweza kuwa mmoja kati ya wachuna ngozi. Na kile kilikuwa kisu cha kazi. Kazi ya uchunaji. Hekaheka……Naomi katika tuhuma nzito. Jeraha la hisia limemkimbiza na kumtupia katika domo la sheria. **** Kibwana alikuwa daktari anayeheshimika sana licha ya tabia zake chafu. Za kubadili wasichana hovyo. Siku hii ilikuwa zamu ya Naomi kutiwa hatiani, akiwa katika hekaheka za kumsaka Kibwana kwa sababu nyingine kabisa anajikuta mikononi mwa polisi. Kukamatwa kwa Naomi ni tofauti na wahusika waliopita ambao mahojiano kidogo pekee yaliwaweka huru. Ndugu zao walijitokeza kwa wingi. Lakini Naomi anakuwa mwoga mwenye hofu, kile kisu kilichokutwa katika begi lake kinamtia katika matata makubwa. Hakuna ndugu wa karibu ambaye alijitokeza. Hakuna mtu ambaye alikuwa anamtambua Naomi katika jiji la Mbeya. Hali hii ikawatia morali askari, wakajiaminisha kuwa Naomi anaweza kuwa mmoja kati ya wachuna ngozi. Na kile kilikuwa kisu cha kazi. Kazi ya uchunaji. Hekaheka……Naomi katika tuhuma nzito. Jeraha la hisia limemkimbiza na kumtupia katika domo la sheria. *** TAARIFA ya daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kunusurika kuchunwa ngozi na mwanamke kiongozi wa kikundi cha wachuna ngozi jijini Mbeya ambao asili yao ni Zambia ilipokelewa katika namna ya mfadhaiko na mwanadada Suzan ambaye alikuwa katika basi akiwa katika safari ya kuelekea jijini Mbeya. Hakufadhaika kwa sababu daktari mwenzake alikaribia kuchunwa ngozi lakini alistaajabishwa na jinsi taarifa ile ilivyosukwa kisasa na kuleta mvuto katika kuisoma. Kibwana alikuwa amedanganya kuwa alikuwa amekabwa na msichana akiwa na kikundi chake cha wachuna ngozi. Ilikuwa poneaponea yake kubakia hai. Kamatakamata ilikuwa inaendelea na hadi wakati huo watu ishirini walikuwa wamekamatwa kwa shutuma hizo za uchunaji ngozi. Lilian ambaye alikuwa anatabasamu kutokana na uongo ule sasa alikunja ndita na kufedheheka. Cheko likatoweka, fadhaa ikatawala. Lilian akatawaliwa na hisia zilizomkera, hisia za kusulubisha roho zisizokuwa na hatia. Hakika alikuwa ana uwezo wa kuzikomboa roho hizo zisizokuwa na hatia. Lilian alikuwa na uwezo wa kuubadilisha uongo wa Dokta Kibwana kisha kuwaweka huru wale wasokuwa na hatia. Macho ya Lilian yakarejea katika lile gazeti la kila siku. Akaitazama vyema ile orodha ya waliokamatwa wakihusishwa na tuhuma zile. Wanawake (9) na wanaume waliosalia. Roho ikamuuma. Maswali kadhaa yakakivamia kichwa chake. Huenda wale wanawake waliokamatwa walikuwa na watoto nyumbani, ama walikuwa ni wajane familia inawategemea. Akajiuliza watakuwa katika hali gani. Hisia zikamnyong’onyesha, akauma meno kwa hasira, uongo wa Kibwana ulikuwa unawatesa wengi. “Lazima niuweke ukweli wazi….ukweli ambao utaniweka huru.” Lilian akajiapiza huku akifunika lile gazeti. Kisha akaliweka mbali naye. Baada ya muda akasinzia huku akijilaani kwa kuziruhusu hisia zake ziweze kutambaa na kumzidi hatimaye zikasimama wima na kumzidi zaidi kisha zikaanza kumpelekesha huku na kule. Akajikuta yu mtumwa wa mapenzi. Akaangukia mikononi mwa Walter na kujikuta wakizini kisha akaukwaa Ukimwi. Usingizi ukapaa akaangaza huku na kule, kila mmoja alikuwa na lake jambo. Basi lilikuwa likikwea milima ya Kitonga. Lilian akapiga mbewe kisha akachukua maji katika chupa yake akayagida kwa fujo. Kisha akajiegemeza tena katika pembe moja ya kiti. Akasinzia tena. **** MAJIRA ya saa tano usiku, Walter akiwa na koti zito lililomfunika kuanzia mabegani hadi ugoko wa miguu yake, alitembea kwa kujiamini sana na kufanana na walinzi ambao wamefuzu katika Nyanja hiyo. Licha ya kwamba ulikuwa ni usiku wa giza kuu lakini hakuyaruhusu macho yake kutoka nyuma ya miwani nyeusi. Akatembea kwa kasi huku akigeuka nyuma mara kwa mara. Hatimaye akafikia mahali ambapo uoga ulichukua nafasi yake. Nyumba iliyokuwa mbele yake iliwashwa taa moja ya nje, huku ndani pakiwa na giza. Eneo lilikuwa tulivu lakini liliamshwa na kelee za mbuzi na ng’ombe wa jirani ambao bila shaka walikuwa wameshtuliwa na kitu chochote kile pale zizini. Walter aliyekuwa jasiri muda wote hatimaye akaanza kuingiwa na hofu. Akahofia kukutana na mtu ambaye alitarajia kukutana naye. Lakini hakuwa na budi kukutana naye. “Nitamuogopaje msichana?” alijiuliza Walter kimyakimya. Swali hili likampa ujasiri wa kuendelea kusonga mbele. Akakaza mwendo. Nia ya dhati ya kukutana na adui yake ikamkumba na kuamini kuwa uoga wake nd’o utayafanya maisha yake kuwa magumu zaidi. Walter alikuwa amefikia maamuzi ambayo kwake aliyaona kuwa sahihi kabisa. Alinuia kukimbilia jijini Kampala nchini Uganda ambapo aliamini kuwa alikuwepo ndugu yake pekee ambaye angeweza kumpa ushauri wa mwisho na kama kuna siri inahitajika kufichwa basi ni huyo pekee angeweza kumfichia. Walter alihitaji kuonana na mjomba wake wa Kampala. Anko Muganyizi. Ni huyu ndugu pekee baada ya Frank ambaye angeweza kumsikiliza, kumshauri na ikiwezekana kumsaidia kwa namna yoyote. Angefika vipi wakati hana pesa? Huenda si sahihi kusema kuwa Walter, Dj maarufu kabisa kuwa hana pesa. Pesa alikuwanayo lakini ilikuwa katika hifadhi salama. Pesa yote ya Walter ilikuwa imehifadhiwa benki. Na kadi pekee ambayo ingemuwezesha Walter kuchota mamilioni yake katika amana yake. Kadi ambayo anakumbuka kwa asilimia zote aliisahau Mbeya katika chumba cha Lilian. Walter hakuwa na ujanja alihitaji pesa ili aweze kuondoka jijini. Ni kweli alikuwa na marafiki wengi lakini hakuwa na imani nao kutokana na hisia zake za kusakwa na polisi kwa kosa la kujaribu kujiua. Marafiki haohao wangeweza kugeuka maadui na kisha kumchomesha kwa maaskari kisha ajikute matatani. Walter akaamua kujipigania mwenyewe. Sasa alikuwa ana kwa ana na nyumba ambayo ndani yake aliamini kuwa palikuwa na kadi yake ya benki. Akaanza kugonga mlango taratibu hakupata majibu. Akagonga tena bado kimya. Nani alikuwa ameiwasha taa ya nje….na nje palikuwa na viatu vya kike, viatu vya Lilian. Ilistaajabisha. Bila shaka pale ndani aidha palikuwa na mtu ama alikuwepo kisha akatoka. Walter akajaribu kuutikisa mlango lakini haukufunguka, sasa akaamini kuwa hapakuwa na mtu. Akashusha pumzi kwa nguvu zote. Kisha mikono ikamlegea kwa kukata tamaa. Jitihada zake hazikuwa na maana hata kidogo. Na kadri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo wasiwasi wake ukazidi kusogea karibu. Hakuwa na pesa ya kutosha walau kumrejesha jijini Dar es salaam vipi kuhusu pesa ya kwenda nje ya nchi? Walter akafadhaika. Akanyanyua kichwa chake kutazamana na anga tulivu isiyo na dalili ya kuhifadhi wingu la mvua. Anga ikamzomea, akaona haya akarejesha kichwa chini taratibu mara akakomea juu ya mlango. Macho yakatulia katika sehemu ile. Kuna kitu alikikumbuka. Mara yake ya kwanza kufika nyumbani kwa Lilian alimshuhudia Lily akiutoa funguo wa chumba chake juu ya mlango. Mlango huu huu anaotazamana nao mbele yake. Kiherehere kikamshika Walter, akauvamia ule mlango akaupitisha mkono wake juu ya mlango akapapasa huku na kule. Lahaula…akaibuka na ufunguo halisi wa chumba kile. Huku akitetemeka alijaribu kuufungua ule mlango. Aliingiza funguo mara kadhaa bila mafanikio. Hatimaye akajituliza vyema akaweka hofu kando akaweka umakini zaidi. Mlango ukafunguka. Chumba kilikuwa kinanukia utuli wa bei ghali. Bila shaka mtumiaji alikuwa ametoka kuutumia muda mfupi uliopita. Lilian alikuwa Mbeya? Kumbe alinitoroka na kuja Mbeya? Walter alijiuliza kwa sauti ya juu kiasi. Macho yake yakiangaza huku na kule kana kwamba muda wowote ule Lilian anaweza kukivamia chumba kile. Walter alibaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa, akili ikiwa katika mnato bila kukumbuka ni kipi alikuwa amekifuata pale ndani. Baada ya sekunde kadhaa akakumbuka kilichomfanya awe jijini Mbeya. Akakivamia kitanda akaanza kupapasa. Akatupa mikoba ya Lilian huku na kule. Hakuna kitu. Akatoa godoro akavuta kitanda kwa fujo, akavamia kabati la nguo la dokta Lilian, akatoa nguo pasi na utaratibu maalumu. Akaangusha viatu kutoka mahali vilipohifadhiwa bado hakukutana na kadi yake ya benki. Mara akafikia koba jingine kubwa jeusi, akakung’uta mara zikatoka chupa ndogondogo na kuvunjika, harufu ya madawa ikatawala, mabomba ya sindano yakasambaa huku na kule. Lilian ni muuaji? Walter akapayuka. Hakujua kuwa Lilian alikuwa ni daktari mzoefu na vile vilikuwa vifaa vya kazi. Hofu ikajijenga upya katika moyo wake. Sasa akaanza kuogopa waziwazi, akaogopa kuwa katika chumba kile. Hali ilikuwa tete. Akiwa katika kushangashangaa mara alisikia vishindo vya harakaharaka kuelekea katika nyumba ya Lilian. Wakati anavuta umakini zaidi mara vishindo vikakoma. Walter akajikuta katika wakati mgumu zaidi kuupitia, alijihisia amezungukwa na watu wabaya ambao muda wowote wanaweza kuondoka na roho yake. Walter akanyata katika dirisha ambalo pazia lake lilikuwa limeshushwa na hakukumbuka kulifunua hapo kabla. Akalifunua lile pazia taratibu aweze kutazama ni nani yule aliyekoma kutembea ghafla baada ya kuifikia ile nyumba. Jicho lake likakutana na kitu ambacho kilimshtua sana, alishtuka kwa sababu hakutegemea kukutana nacho tena. Ilikuwa ni kadi yake ya benki. Walter akaduwaa. Lakini hakudumu katika kuduwaa kwake. Zile hatua zilizokuwa zimekoma zikaanza tena lakini sasa katika namna ya kunyemelea. Walter akaingiwa hofu tena. Sasa ilikuwa hofu kuu. Mlango wa kile chumba ukatikisika, Walter hakuwa amejiandaa kukabiliana na shambulizi la ghafla namna hiyo. Kadi yake mkononi, macho yakitazama mlangoni alikuwa anangoja lolote litakalotokea……… Mikono ilikuwa inatetemeka sana na akili ilikuwa imekoma kujishughulisha. ***** LILIAN hakuwa na muda wa kupoteza, baada ya kuwa amefika jijini Mbeya majira ya saa moja usiku. Licha ya kuwa na uchovu wa safari ndefu kutoka jijini Dar es salaam bado hakuweza kustahimili kulala huku akisumbuliwa na hatia moyoni mwake. Lilian alijipumzisha kwa masaa kadhaa huku akiwa ameiweka simu yake katika mlio uliotegeshwa kwa ajili ya kumshtua majira ya saa nne usiku. Hewala!!…kama alivyotarajia, simu ilimgutua usingizini. Akajikokota hadi bafuni akajimwagia maji vyema na kisha akajipulizia utuli. Safari ya kuelekea Uyole. Nia kuu ya Lilian ilikuwa kuupata mwangaza juu ya Kibwana na shutuma zake juu ya kukoswa koswa kuchunwa ngozi na msichana hatari. Lilian alifahamu fika kuwa si Kibwana wala mdogo wake ambaye anaweza kutegemea ujio wake katika kasri yao ya Uyole. Kasri ambayo awali aliitumia sana kuwa anahifadhi gari yake ambayo kwa wakati huu alikuwa ameiacha jijini Dar es salaam kwa sababu za kiusalama. Lilian akautumia mwanya huo wa giza kumtembelea Kibwana kama atamkuta nyumbani kwake aweze kumpa masharti ya kuusema ukweli ili wale watu wema waliokamatwa bila kosa waweze kuachiwa huru. Lilian alichukua taksi ambayo ilimpeleka moja kwa moja hadi nyumbani kwa dokta Kibwana. Akalifikia geti la kuingilia nyumba ya Kibwana. Hapo akashuka upesi katika taksi akafanya malipo na kisha harakaharaka akaelekea katika geti. Alipoanza kugonga geti mara akasikia hatua nyuma yake. “Wewe ni nani?” sauti nzito ya kiume iliuliza kutokea gizani. Lilian alipogeuka akakumbana na kiwiliwili kirefu kilichojaa vyema kimazoezi. “Wewe ni nani?” sauti ile ikarudia kuuliza tena. “Lili…..” alijibu kwa hofu. Majibizano yao yakakatishwa na geti lililofunguliwa. “Dokta…..mweee” aliduwaa mtu aliyefungua geti. “Akwino….huyu ni nani?” Lilian aliuliza kwa mshangao lakini walau akiwa na afueni ya kumuona mtu wanayefahamiana. “Ni afande…Afande huyu ni wa hapa hapa…” Yule kijana akamtoa hofu yule mwanaume mrefu dhidi ya Lilian. Mjinga ameharibu akili za watu huyu…Lilian alijisemea huku akiingia ndani. Akwino akaghairi safari yake aliyokuwa amepanga. Kiherehere kikamshika akatamani kusema maneno kadhaa na yule mgeni. Wakajiweka sebuleni, yule mnyakyusa akaanza kumsimulia Lilian juu ya hali ya afya ya Kibwana. Alipayuka mambo mengi kana kwamba alikuwepo eneo la tukio, “Huwezi amini dokta yaani ilibaki kidogo tumsahau, alipambana huyo aisee….akawashinda sijui wakamchoma sindano gani lakini kwa sasa ana unafuu. Tumuombee kwa Mungu tu aweze kupona. Kwa sasa nd’o kama hivi ulinzi kama ikulu kila muda….na pale nisingetokea haki ya Mungu wangekufunga pingu wale..yaani hawatanii…” Akwino alimaliza kuimba mashairi yake. Lilian akazuga kusikitika. “Kwa hiyo umeenda kumuona tayari na yupo hospitali gani…” “Nd’o kesho nasafiri zangu nasikia yupo Morogoro huko hospitali ya mkoa. Hebu ngoja uone….” Alijibu Akwino kipengele ambacho kilikuwa cha muhimu zaidi kwa Lilian. Kisha akasimama na kuliendea kabati. Akatoka na bahasha. “Kuna picha tunaenda kuzithibitisha…picha za wachuna ngozi.” Akwino akamwonyesha picha kadhaa Lilian. Picha zote zilionekana kuwa ngeni sana kwa Lilian. Lakini picha ya mwisho ilikuwa na utata kidogo. Akaichukua na kuitazama kwa makini sana. picha ile ilifanana na mtu ambaye amewahi kumwona mahali. Alijaribu kuukaataa uhalisia lakini hali ilibaki kuwa ile picha ilikuwa ile anayoifahamu….. Laiti kama picha ingekuwa inasema…………. Akanyanyua macho yake na kuangaza kona hii na ile kisha akamnong’oneza Akwino maneno kadhaa, Akwino akastaajabu lakini Lilian hakuonyesha kwamba ni utani alisisitiza tena. Akwino akafanya tabasamu hafifu. Lilian akasimama na kuaga. Akwino akamsindikiza hadi nje. Lilian akatazamana na wale maaskari waliotaka kumtia katika varangati hapo awali, akataka kusema nao neno lakini akahisi kuwa halikuwa na umuhimu wowote. Akaamua kuondoka zake huku akiagana tena na Akwino. “Usisahau nilichokwambia…..” Lilian alisisitiza. Akwino ambaye ni mdogo wake Kibwana akatikisa kichwa kuashiria kuwa ameelewa sana. Lilian akatoweka. Kwa mwendo uleule wa taksi. Hakutaka Taksi ile impeleke nyumbani, badala yake alikifikia kibanda kilichokuwa kinauza vinywaji baridi akashuka na kuketi katika kiti kimojawapo akaagiza soda. Lilian alifanya hivi ili kuwapoteza wale askari iwapo wangefanya hila yoyote ya kumfuatilia bila yeye kujua. Alitumia dakika takribani ishirini bila kuona dalili yoyote ya kufuatiliwa. Akafanya malipo upesi safari hii akachukua pikipiki. Akampa maelekezo na kumpeleka hadi mtaa mmoja kabla ya kuifikia nyumba yake. Hapa akaanza kutembea kwa miguuu lakini kwa mwendo wa kasi. Alipoifikia nyumba yake akashtushwa na vurugu zilizokuwa zinaendelea ndani ya nyumba yake. Kibaya zaidi taa iliyokuwa imezimwa sasa ilikuwa inawaka. Maajabu haya!! Akasita kwa muda kutembea, alikuwa anatetemeka sana. alidhani wale askari wamemtangulia katika nyumba yake na sasa wanafanya upekuzi. Alitamani kukimbia na kurejea alipotokea lakini miguu ikawa mizito. Aliamini kuwa kama wale ni maaskari katika chumba chake basi bila shaka watakuwepo wengine wametapakaa pande zote za nyumba ile na pale alipokuwa walikuwa wanamuona. Lilian akakaza mwendo japo kwa kukata tamaa akaingia ndani ya nyumba aweze kuwakabili maaskari. Lahaula!! Hakuyaamini macho yake kwa kile alichokuwa anakitazama!! Ana kwa ana na Walter……wote wakashangaana, nyumba ilikuwa imevurugwa haswa. Hakuna kilichokuwa katika mkao wake, vyote vilikuwa shaghalabaghala. Walter alitegemea kuonana na Lilian lakini sasa alikuwa akimuhofia kama muuaji mkubwa. Hofu yake haikupungua badala yake iliongezeka baada ya Lilian kuanza kumsogelea. Harufu ya kifo!! Walter akajihami, akanyanyua kinywa chake aweze kusema. “Walter jamani…” Lilian akawahi kusema huku akitaka kumkaribia zaidi. “Lilian…komea hapo hapo…” Walter akaamuru. Lilian akashangaa, hakutegemea kabisa amri ile. Akasita na kuganda akiwa ameyatumbua macho. “Lilian..unataka kuniua..unataka kuniua baada ya kunigombanisha na Naomi wangu..unataka kuniua baada ya kunilaghai nikafanya mapenzi na wewe wakati nina mke wa ndoa Lilian….sasa unataka kuniua, visu vya nini humu ndani Lilian…kumbe wewe ni muuaji…wewe ni mmoja wa wachuna ngozi Lilian…..Lili..Lili kweli ni wewe Lili…haya niue sasa….si ulinidanganya unatoka kidogo kumbe umeharibu umeridhika na sasa unatabasamu tu…muuaji mkubwa wewe…ulidhani ule ujumbe wa Naomi sitauona eeh..” Walter alikomea pale, alikuwa anatetemeka sana hisia zote za usaliti ziliishi naye na kujikuta katika wakati ule mgumu. Lilian alikuwa anaduwazwa na maneno ya Walter. Alijaribu kuisoma akili yake lakini alimuona kama aliyechanganyikiwa na ambaye hayupo tayari kubadilishwa kwa lolote lile katika mawazo yake. ITAENDELEA KESHO!!!
Posted on: Wed, 16 Oct 2013 15:00:01 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015