RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU - TopicsExpress



          

RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YATANO Naomi anaiona hukumu mbele yake, hukumu ya kuuawa, anamkumbuka Mungu wake. Anamsihi aingilie kati ili apate nafasi nyingine ya kuishi kwa amani. Ombi lake linakuja wakati muafaka. Ghafla mwanaume aliyekuwa anahaha huku na kule anateleza na kutulia tuli baada ya kuanguka. Waliokuwa wanamwandama wanakimbilia eneo la tukio. Naomi anaupata upenyo wa kutoroka. Haipotezi baati hii. Anatoweka.kimya kimya kuepusha tafrani mbele yake. * * * "Mbona niko hapa, gari la wagonjwa liko wapi? limembeba nani? da Maureen yuko wapi?" maswali mfululizo yalimtoka Walter baada ya kuzinduka na kujikuta kwenye kitanda hospitali. Nesi aliyekuwa pale hakuwa na jibu lolote lile. "Naomi Naomi yule ni Naomi, Naomi wangu" Walter akaanzisha mkasa mwingine, nesi akadhani tayari mgonjwa ana matatizo ya akili. Mbiombio kaenda kumwita daktari, lakini kama vile alikuwa ameitwa Walter naye aliruka kutoka pale kitandani akatoka nje ya chumba cha hospitali huku akiwa na bandeji kichwani, kwa jinsi ambavyo hakuwa na hofu na wala hakutetemeka hata kidogo hakuna aliyeweza kumdhania kuwa alikuwa anatoroka hospitali. NESI alikuwa amefanya kosa kubwa sana kumwacha mgonjwa peke yake katika kile kitanda. "Tabata shilingi ngapi?" Walter alikoroma mbele ya taksi. "Buku saba mjomba" "Nipeleke fasta!" alijibu Walter alipotajiwa bei na dereva taksi. "Dah! nyie wagonjwa hamuaminiki nipe changu kwanza" akasema dereva yule wakati akianza kuiwasha gari yake. Haraka haraka kwa kujiamini, Walter ambaye alionekana kuwa na haraka sana akazama mifukoni mwake, tofauti na matarajio yake hakukuta wallet yake mfukoni na aliambulia shiingi elfu mbili ya Uganda tu katika mfuko wake wa shati. "Nilijua tu! yaani watu wengne bwana" alianza kuponda dereva alipogundua Walter hakuwa na kitu mfukoni. Walter hakuwa na hadhi tena mbele ya macho ya madereva wengine. "Hapana nilikuwa na wallet kaka, sijui...." "Huna lolote mzazi nenda ukapande daladala tena hizo zinapita!" alijibu dereva huku akimwonyesha Walter magari yanayotokea Muhimbili kwenda Buguruni. Walter kwa mfadhaiko mkubwa alisogea barabarani akapiga gari mkono akapanda japo lilikuwa limejaa. "Yuko wapi mgonjwa!" daktari aliyefuatwa na nesi alihoji. "Alikuwa hapa..." kwa uoga na kutetemeka alijibu nesi, kwani Walter hakuwepo tena pale. "Maskini wa Mungu atakuwa ameenda wapi huyu kijana" alijiuliza daktari huku akijikuna kichwa chake. **** Foleni ya siku hiyo ilikuwa ndefu sana tofauti na siku nyingine zote, kuanzia maeneo ya Magomeni gari alilopanda Walter lilikuwa halisogei mbele na tayari lilikuwa limezimishwa, abiria walikuwa wamekasirika mno na kila aina ya matusi kwa serikali yalisikika. Walter alikuwa mkimya sana, moyoni aliwaza mengi mazito, hakuwa hata na simu aweze kumpigia Muga wala Frank. Akiwa ndani ya gari kuna mazungumzo yalimvutia kusikiliza. "Jamani walikuwa wanamkimbiza hospitali na ajali imewazuia tena, mimi simlaumu dereva hata kidogo alikuwa anawahi" mama mmoja alikuwa akimwambia abiria mmoja katika gari alilokuwa amepanda Walter. Mama huyo aliyekuwa anatembea kwa miguu alionyesha huzuni yake dhahiri. Maneno hayo yalipokelewa kwa hofu na Walter, kwa wakati huo aliamini kila mgonjwa ni dada yake (Maureen) hivyo bila kujali jeraha lake kichwani alishuka na kuanza kujikongoja kuelekea kule alipotoka yule mama. "Ni huyu ni huyu jamani" Walter alisikia maneno hayo nyuma yake lakini hakugeuka kwani macho yake yalikuwa yanatazama gari ya wagonjwa iliyogongwa vibaya ikiwa imeziba barabara. Huku akizidi kukaza mwendo alishtukia akikamatwa kwa nguvu na kufungwa kamba mikononi na miguuni. Hakujua ni kwa nini kwani tayari alishasahau kuwa ametoroka hospitali Ilimchukua dakika chache Walter kugundua tayari alikuwa mikononi mwa wauguzi na wahusika wa hospitali ambayo alikuwa ametoroka "Jamani mimi ni mzima naenda kumwangalia dada yangu ni mgonjwa na alikuwa kwenye ile gari" aliongea Walter huku analia akiwaonyesha gari ya wagonjwa iliyokuwa imepata ajali mbaya sana. Wale watu hawakutaka kumwelewa waliamini amerukwa akili na hakujua anachokizungumza wakati ule. Kwa usalama wa maisha yake hawakumwachia. "Jamani naomba mnielewe japo kidogo dada yangu anaitwa Maureen ndio namtafuta na mimi naitwa Walter hata nyie nafahamu ni wahusika wa hospitali sijachanganyikiwa mimi najitambua" alijaribu kwa kila hali Walter kuwashawishi watu hao kumwachia lakini badala yake walizidi kuimarisha ulinzi asiweze kupata nafasi ya kutoroka. Walter hakuwa na njia mbadala hakuwa na nguvu za kuwazidi watu hawa hivyo alilazimika kwa shingo upande kukubali kupandishwa kwenye gari waliyokuja nayo watu hawa na kusubiri hadi foleni ilivyoanza kwenda akarudishwa hospitali alipochomwa sindano za usingizi na kufungwa mikono yake kikamilifu ili akizinduka asiweze kutoroka tena. Fahamu zilipomrejea yalikuwa yamepita masaa kadhaa. * * * Ilikuwa taarifa ngumu sana kuingia na kukubalika katika kichwa cha Frank (baba mdogo wa Walter) pamoja na Anko Muga rafiki yake,taarifa ya gari aliyokuwa amepakizwa Maureen ili akimbizwe katika hospitali ya Muhimbili kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya ilikuwa imepata ajali kwa kugongwa na gari kubwa upande wa ubavuni ambapo mwili wa mgonjwa ulirushwa nje ya gari "hali yake ni mbaya sana na foleni ni kubwa inashndikana kuwahishwa hospitali,na hata madaktari waliopigiwa simu wafike haraka hawawezi kwa sababu ya foleni kubwa" ilimalizia kwa huzuni kubwa sauti ya mwanadada aliyekuwa anasoma habari ya ghafla ama mpasuko "BREAKING NEWS"katika kituo maarufu cha luninga hapa nchini. "Walter atanielewaje mimi,huyo pekee ndiye ndugu yake aliyebaki hapa ulimwenguni!" Frank alijiuliza huku amejishika kichwa akitembea bila kujua anapoelekea hasa "Frank nadhani si muda wa kujilaumu, tusubiri na Mungu atatuonyesha njia ya kweli labda atapona" Anko Muga alimpa matumaini Frank ambaye alionyesha kuchanganyikiwa kabisa kwa taarifa ile ya kushtusha. Nyumba yake ilikuwa shaghalabaghala aliamini umati uliofika pale siku ya tukio lazima walikuwepo vibaka hivyo alitegemea sana wizi pia umefanyika. "Naomi yuko wapi?" ni swali la pekee aliloamini jibu lake lingemfungua akili yake, hakupata wa kumjibu Naomi hakuwa eneo lile tena,na hakuna aliyejua ameondoka saa ngapi pale, Frank alizidi kuchanganyikiwa. Lakini hakuweza kuibadili siku hii. Hakuweza kuubadili ukweli uliopo. Yaliyopangwa yakatimia. * * * "Ulale pema peponi Maureen, msalimie bibi mwambie mchumba wangu Naomi sijui alipo, wasalimie baba na mama waambie nawapenda sana, kwaheri dada Maureen"Aliongea hayo Walter wakati anauaga mwili wa Maureen uliokuwa umepondekapondeka vibaya kutokana na majanga aliyoyapata, kwanza umeme halafu ajali mbaya ya gari. Maneno na sauti yake vilimchoma kila mtu aliyeyasikia,Walter alikuwa na jeraha kisogoni, nguo zake zilikuwa chafu sana. Hakuhitaji kubadilisha na hakuwepo wa kuweza kumshawishi lolote. "Nilitegemea kula nawe sikukuu za mwisho wa mwaka kwa nini hukusubiri lakini! Mbona hukutaka walau nipate dakika mbili za kukuona ukitabasamu. Ewe ardhi mwenye tamaa nimeze na mimi uridhike, hivi baba na mama hawakukutosha? Bibi naye je…haya na dadangu umemchukua….eeh Ardhi nimeze sasa hivi niondoke na Maureen" alishindwa kujizuia Walter akaangua kilio kikali, wakati huo Frank alikuwa hajiwezi ameishiwa nguvu akiwa amekaa chini, ulikuwa msiba ulioteka hisia za wengi sana katika mitaa mbalimbali jijini Dar-es salaam. Kilio cha mtu mzima kikachukua nafasi. **** Baada ya ardhi kugoma katakata kukisikia kilio cha Walter na badala yake kuyameza machozi yake bila shukrani hatimaye Walter akajikuta akiilaani ardhi ya Tanzania. Aliilaani kwa kuwa ilikuwa imempa uchungu ambao ulikuwa mgumu sana kufutika. “Huenda hata Naomi naye ilimmeza ardhi hii isiyokuwa na shukrani.” Walter alisema na nafsi yake wakati akimalizia kuilaani kwa lugha zote ardhi ya Tanzania. “Frank.” Walter aliita kisa akendelea, “Anko Muga.” Wote wakawa makini kumsikiliza. “Naapa mbele yenu, ndugu zangu mliosalia. Sitakaa niikanyage ardhi hii tena. Frank, usijisikie vibaya na kuhisi kuwa nakukimbia; hapana umekuwa msaada mkubwa sana kwangu, wewe ni baba mwema sana kwangu. Lakini haikupangwa tu nifurahi pamoja nawe. Labda sikustahili kuzaliwa katika nchi hii, n’do maana inanitenda hivi.” Walter alimaliza kuzungumza alichakuwa amepanga. Frank na Muga, wakabaki kimya, hakuna aliyejazia neno la ziada. Waliamini kuwa maneno yao hayawezi kumbadili Walter na msimamo wake. Baada ya siku mbili Walter akiambatana na Muga, wakaiacha ardhi ya Tanzania. Safari hii waliondoka kwa usafiri wa ndege. Lile gari jipya walilolitumia kwa safari ya Mwanzo, Walter akamtunuku Frank kama zawadi kwa moyo wake wa upendo. Maisha mapya yakaanza tena. **** BAADA YA MIAKA MIAKA MIWILI. Maandalizi ya tamasha kubwa la Muziki nchini Tanzania yalikuwa yamepamba moto, tamasha hili kwa mara ya kwanza liliwagusa hadi wafuatiliaji wengine katika nchi za jirani. Liliwagusa watu wengi kwa sababu moja tu, wasanii mapacha kutoka nchini Nigeria walikuwa wamekubali siku ya kilele cha tamasha lile. Walter aliipokea taarifa hii kupitia vyombo vya habari. Akakuna kichwa chake, akachangamka kuisikia habari hii. Akaikumbuka ndoto yake tangu anaanza kuwika katika shughuli za u-Dj. Ndoto ya kufanya kazi na wasanii wale. Lakini alipokumbuka kuwa wanaifanya kazi yao katika ardhi aliyoilaani nayo ikamlaani, munkari wake ulishuka sana. Na hamu ikamwisha. Kitu bora hutengenezwa na watu bora. Waandaaji wa tamasha lile walihitaji kufanya kitu bora sana katika kilele cha tamasha hilo. Hivyo katika sekta zote za muhimu walihakikisha zinashikiliwa na watu wa maana. “Hebu mpigie simu namba yake hii hapa.” Mshika dau mmoja alitoa wazo baada ya kuwa wamejadili kwa muda mrefu. Simu ikapigwa na wote wakaunda kimya kikubwa ikabaki kusikika simu pekee. “Hallo…” ilijibu sauti upande wa pili. “Unaongea na timu ya Chizika..bila shaka ni Dj Muga.” “Bila shaka.” Alijibu kwa utulivu. Upande wa pili ukazungumza lengo la kupiga simu. Walikuwa wakimuhitaji Dj ambaye alikuwa anafanya kazi akisimamiwa na Muga kama mkurugenzi wake. “Nitawapatia jibu baadaye.” Alijibu Muga baada ya kuwa amekosa jibu la moja kwa moja. **** MABISHANO yalikuwa makali sana, Walter hakutaka kujadili suala la yeye kurejea Tanzania. Muga alimsisitiza na kumtajia dau kubwa ambalo limetajwa kwa ajili yake. Dau halikumshtua Walter. Tayari alikuwa majeruhi, jeraha la hisia za ardhi ya Tanzania kuwa inamuonea zilimgalagaza na kumfanya ajione yu mtumwa utumwani. “Walter.” Muga alimuita kwa utulivu baada ya damkika kadhaa za kutupiana maneno japo si kwa ubaya. Walter akatikisa kichwa kuashiria amesikia. “Baba, mama, bibi, dada….wako wapi?” “Mbinguni.” Alijibu Walter. “Umewahi kufika huko ukawaona.” “Najua wapo mbinguni. Nilifundishwa hivyo tangu utotoni.” “Ok. Hivi unajua kuwa wanakuona unachofanya duniani.” “Ndio wananiona, hata hilo nilifundishwa pia.” Alijibu Walter upesi bila kuijua nia ya Muga. “Vyema kama unatambua kuwa wanakuona. Na watu wote hao uliowaheshimu wakati wapo hai umeshindwa hata kuheshimu makaburi yao, umeshindwa kuheshimu makazi yao ya sasa, umewakimbia. Walter watu hawa wa muhimu kwetu wanakutazama na wanalia juu yako. Kila mara ni mimi na Frank tunaenda kufanya usafi katika makaburi. Wewe umegoma, umegoma kuzisafisha nyumba zao.” Muga akaweka kituo kisha akaendelea, “Mimi sikulaumu wewe hata kidogo, ila naomba uamini kila kitu huja na hupita hata hayo yalitokea na yamepita. Kama unailaani ardhi ya Tanzania. Je watu wa Rwanda waliopoteza ukoo mzima wafanye nini?” alimaliza Muga. Kimya kikatanda, Walter alikuwa anatetemeka. Akajihisi mkosefu. Maneno ya Muga yalikuwa yamemvuruga kwa kiasi kikubwa. Na kwa upande mkubwa sana yalikuwa yana ukweli ndani yake. Muga alipomaliza akaaga ili aweze kuondoka maana alikuwa nyumbani kwa Walter wakati ule. “Anko….hebu subiri kidogo..” Walter akamzuia. Muga akabaki amesimama akimsikiliza Walter. Walter akatazama juu, kisha akashusha kichwa chake chini. “Kwa heshima yako, Frank na roho nilizozipenda lakini zikaitamanisha ardhi yenye tamaa ikazimeza. Nitarejea Tanzania. Kwa moyo mmoja mweupe kabisa nitarejea katika ardhi niliyoichukia, kama bado ina kinyongo nami kwa kosa nisilolijua basi na inimeze, kama haina kinyongo nami na inihifadhi kwa upendo isiniumize tena siku hizi za karibuni. Ni heri inimeze mimi kuliko kuimeza roho yoyote ninayoifahamu. Nina jeraha kubwa sana ambalo halina dalili ya kupona. Sihitaji kujitonesha upya.” Walter alimaliza kuzungumza. Muga akamsogelea na kumpigapiga mgongoni ishara ya kumpooza. Akazua kilio kingine. Walter hakuweza kustahimili kumbukumbu ngumu za kipindi cha nyuma. Ikabaki kazi ya Muga kumbembeleza. **** ***JIFUNZE. Mkataa kwao ni mtumwa, na mkabili tatizo ni jasiri kuliko yule anayejaribu kulikimbia…. Tiba ya jeraha lolote ni kuliacha wazi. Ukilificha litavunda!!!! ITAENDELEA KESHO JIONI!!!
Posted on: Tue, 17 Sep 2013 15:00:00 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015