RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron mosenya SIMU: 0655 - TopicsExpress



          

RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron mosenya SIMU: 0655 727325 SEHEMU YA KUMI NA TANO Hatimaye mvua ikaanza kumwagika. Walter akazidi kupagawa, alikuwa mpweke katika mji wa kigeni kabisa lakini katika ardhi ya Tanzania. Walter akajipekua na kugundua kuwa kuna kitu kikubwa sana anachokikosa. Alijikuta na pesa taslimu shilingi elfu ishirini, hizi zilisalia baada ya kulipa bili yake ya hoteli. Akili ikasimama, joto kali katika mvua. Walter hakuwa na kadi yake ya benki. “Nimeisahau nyumbani kwa Lilian” alisema kwa sauti ya juu. Joto likatoweka tena, ikafuata baridi kali, mwili chepechepe kwa kunyeshewa na mvua. Walter akapagawa. Alikuwa amepanga kwenda kituo cha mabasi aweze kuukimbia mji. Lakini sasa anagundua hawezi kutoka bila kuwa na kadi yake ya benki. KIZUNGUMKUTIII. **** Walter akazizima kwa baridi, mianga ya radi ikamulika, ikawa kama bahati. Akaona maneno kadhaa. “UTULIVU LODGE” matumaini yakarejea upya, akakatisha katika matope bila kujali lolote akaifikia nyumba hiyo. Mlinzi akamuona akamfungulia geti. “Kuna vyumba.” Akapaza sauti kuu, akasikika. Mlinzi akajibu kwa sauti ya juu pia. Alimjibu kuwa hapakuwa na vyumba huku akifanya jitihada za kumwonyesha kibao kil;ichoandikwa taarifa hiyo. Walter akafadhaika. “Angalia hapo mtaa wa pili.” Mlinzi akamshauri Walter. Walter akatoweka, akazidi kulowana. Akaifikia nyumba ya kulala wageni aliyoelekezwa. Hapa alifanikiwa kupata chumba. Akafanya malipo. Shilingi elfu kumi na tano. Akasaliwa na shilingi 5000 mfukoni. Akakivagaa chumba akavua nguo zake zilizolowana. Akajirusha kitandani na kujifunika shuka zito lililokuwa pale kitandani. Baridi kali ikaondoka na mawazo yake ya awali. Lakini yakajiunda mawazo mengine mazito. Mawazo haya yalichanganyikana na kumbukumbu nyingine mbaya. Kumbukumbu za vifo. Vifo vya wazazi wote wawili, babu na kisha dada yake mpenzi. Vifo hivi vikamkumbusha kiapo alichoapa mbele ya Frank na Muganyizi. Aliapa kamwe hatakanyaga ardhi ya Tanzania, aliapa hivyo kwa sababu ardhi hiyo haikuwa inamtendea haki kwa kumeza ndugu zake wengi kwa wakati mmoja. Kiapo hicho kikalegea baada ya maneno ya busara kutoka kwa Muganyizi, hatimaye Dj Walter akarejea Tanzania katika ardhi iliyomeza uhai wa baba, mama , bibi na dada mpenzi. Ile ardhi aliyoikataa hatimaye ikamkutanisha na Naomi. Msichana wa ndoto zake. Msichana aliyeishi naye na kumpenda tangu utotoni. Ndoa ikafungwa. Ndoa hii ya aina yake ikazua kizaazaa. Cha kumuhamisha Walter kutoka katika jiji la Dar es salaam na kuwa mkimbizi huru katika nchi yake. Akabadili namba za simu na kulikimbia jiji, katika kulikimbia akakutana na Lilian. Lilian akawa msaada mkubwa sana kwake kupitia vitabu vya riwaya, lakini sasa anajaribu kumkimbia Lilian maana anayo kesi ya kujibu. Amebaka!! Walter akamlaani mjomba wake (Muganyizi) kwa kumshawishi kurejea tena nchini Tanzania. Nchi ambayo sasa inampelekesha puta. Laiti kama asingekuwa Muganyizi, hakika nisingekuwa katika hali hii. Alijisemea Walter. Lakini zile hisia zile zile!!! Zilitoka wapi? Walter alijiuliza huku tukio zima la kufanya mapenzi huku akitumia nguvu likirejea katika kichwa chake. “Sawa ni mrembo, na anavutia lakini sijawahi hata siku moja kufikiri naweza kumbaka Lilian mimi… sijawahi hata siku moja…” Walter akiwa amekaa kitandani alipingana kabisa na akili yake. Au nimerogwa jamani!! Maana zile hisia zile… sikuweza kujizuia Walter mimi… sikuweza kabisa!! Halafu sikufurahia chchote sasa!! Kama kweli yeye ni mrembo mbona sikufurahia kama ninavyofurahia kwa Naomi wangu eeh!! Hapana hapana!! Usingizi ukampitia bila kujua A wala Z. Asubuhi sana aliamka, nguo zilikuwa zimekauka. Akazitupia mwilini. Akaisikia njaa kali ikivuma tumboni. Akajilaza tena kitandani. Baadaye akatoka bila kukabidhi chumba, akauendea mgahawa akajishibisha kabla ya kuamua jambo moja. Kuifuata kadi yake ili akutane na Lilian ana kwa ana ama achukue maamuzi mengine. Sasa alikuwa na shilingi elfu tatu tu mfukoni. Walter akaanza kutembea pembezoni mwa barabara akirejea kule alipotokea usiku uliofika, macho yake yalikuwa makini sana akimtazama kila mtu mapema ili atambue kama alikuwa anafuatiliwa ama la. Hatimaye akafika Ilomba. Akapinda kushoto na kuanza kunyata kwa tahadhari kubwa akielekea ilipo nyumba ya Lilian. Mapigo ya moyo yalikuwa juu sana. Kiubaridi kilipuliza, Walter alikuwa hajiamini hata kidogo. Akiwa katikati ya kundi la watu mara kikatokea kitu ambacho hakutaka kitokee, akajaribu kukibadilisha kuwa ndoto lakini haikuwa ndoto. Muda ulikuwa ni saa nne asubuhi na hakuwa kitandani bali barabarani. **** Chai ya moto iliuchangamsha mwili wa Lilian. Alifanya tabasamu mara ya kwanza baada ya masaa kadhaa kupita. “Mh…jana palikuwa na shughuli aisee.” Alikiri huku akiyatazama mashuka ambayo alikuwa anayaloweka katika maji yenye sabuni ya unga. Baada ya zoezi hilo alirejea ndani, akapita mbele ya kile kioo chake, alikuwa na kanga moja. Akajaribu kutembea na kujitazama akagundua kuwa mwendo wa namna hiyo aliwahi kuutembea siku ambayo alitolewa usichana wake. Lilian akalazimisha tabasamu. Mara simu yake ya mkononi iliita. Akaisogelea na kuitazama, mpigaji alikuwa ni Suzi. Yule muathirika wa gonjwa hatari. Mwili ukamsisimka Lilian, akaipokea kwa hofu. Suzi akamsalimia kwa furaha. Naye akamjibu kwa shangwe ya kujilazimisha. “Eti daktari unafahamu Guda alipo jamani…..nimemkumbuka sana kwa kweli.” Sauti ya manung’uniko kutoka kwa Suzi. “Nitakupigia nahudumia mgonjwa.” Alidanganya Lilian akakata simu. Hapo zikarejea zile hisia za kuambukizwa gonjwa la Ukimwi baada ya kuzini na Walter ambaye kwa hisia zake binafsi aliamini kuwa Walter alikuwa katika mapenzi na Suzi. Lilian akaanza kutetemeka. Picha za wagonjwa wa Ukimwi wakikohoa na kujiharishia vitandani zikapangana kwa fujo, vilio vyao wakiwa katika hatua za mwisho za uhai wao nazo zikamwandama. Vidonda vinavyowatoka, mkanda wa jeshi unavyowashambulia. Lilian akajiona yu katika mkondo huohuo. Kama mtoto mdogo akaanza kulia. Alilia akizilaani hisia zake. Hisia mbovu kabisa za kimapenzi zilizompelekea kumwekea Walter dawa katika juisi na hatimaye wakazini. “Nimekinunua kifo changu mwenyewe….” Alijilaani Lilian huku akigalagala chini. Akarusha miguu huku na kule lakini haikusaidia. Akajigeuza huku na kule mara kanga ikauacha mwili akabaki kama alivyozaliwa. Ile aibu atakayoipata kwa kufa na gonjwa hili ikamtesa kwa dakika hizo. Alitia huruma kumtazama. Akiwa katika hali hiyo, akamkumbuka Walter. Hakujua yu katika hali gani. Hatia ya kumtenda kijana huyu wa watu kisaikolojia ikamkumba, akakaa kitako. Akajiona hayupo sahihi kubaki kimya. Kilio cha Naomi nacho kikayakabili masikio yake na kuushambulia ubongo wake. Mwanamke analilia penzi la mume wake. Analia kwa kumkosa mwanandoa mwenzake. Lilian akakusudia kufanya mambo mawili. Kwanza amueleze Walter ni jinsi gani mke wake anampenda kwa dhati, na pili ajiue baada ya kumweleza kila kitu Walter kuhusu hisia zake na historia yake. Uamuzi huu ulikuwa sahihi kabisa. Lilian hakutaka kufa kwa mateso makali ya kuteseka kitandani, kuwapa shida ndugu zake wachache kuanza kumlea kama mtoto mdogo huku akiwaharishia na kuwatapikia hovyo. Kisha azikwe akiwa na kilo moja na nusu. Aibu kuu!! Daktari mzima nakufa hivi? Hapana. Nafsi ilikataa. Hisia mbovu za kupata unyanyapaa wa hali ya juu kutoka kwa wauguzi nao ukamsulubu. Hapo ndipo alipoguindua kuwa wale wagonjwa ambao huwakaba madaktari baada ya kupewa majibu kuwa wameathirika huwa wapo sawa kabisa na wanastahili kupagawa. Lilian alikuwa amepagawa haswaa. Mbaya zaidi alikuwa yu peke yake ndani. Akasimama wima akabadili nguo zake akatoka kwa mwendo mkali kuelekea katika hoteli ambayo Walter alikuwa amefikia. Lilian hakuamini kama atamkuta kweli Walter. Na kama ulivyokuwa wasiwasi wake. Hakika hakumkuta. “Aliondoka jana baada ya kukamilisha malipo yake?” muhudumu alimwambia Lilian. Liliy akashusha pumzi kwa nguvu, akamtazama yule muhudumu huku akiwa amekata tamaa. Akaondoka zake bila kuaga. Asingeweza kujiua bila kusema neno na Walter katu. Alihitaji kumweleza kitu kisha afe akiwa na amani. Lilian alitembea bila kujua iwapo alikuwa anaenda wima ama alikuwa katika kuyumbayumba. Akaufikia mlango na kutoka nje. Akaendelea kutembea kwa myumbo ule ule hadi akaufikia umati mdogo wa watu. Hapa akagongana na kijana mmoja. Akili ikasogeleana kidogo. Akawa anatazama mbele. Ghafla kama ndoto. Jicho likaona…..likaona alichokuwa anakitafuta. Lilian alimuona Walter. Wakajikuta wanatazamana, kila mmoja akaganda bila kusogea hatua ya ziada mbele. Walter mdomo wazi, Lilian macho kodo mkono mdomoni. Kwa sekunde kadhaa bila kusema neno mara ghafla Walter aligeuza alipotokea na kuanza kutembea kwa kasi. Lilian naye akili ikafunguka, akanyanyua mguu na kuanza kukimbia. Nyuma Lilian mbele Walter. Riadha ya kimya kimya ya viumbe wawili. Lilian akimkimbiza Walter ili amueleze kuwa Naomi anampenda sana kisha ajiue. Walter akikimbia kwa kuhisi anatafutwa kwa kesi ya ubakaji. KIVUMBIII!! !! !! !! Walter alijaribu kukimbia huku na kule mara akaelekea kushoto mara akate kulia. Alipogeuka nyuma, hatimaye akashusha pumzi kwa nguvu sana. Alikuwa amefanikiwa kumpoteza Lilian. Walter akafanya ishara ya msalaba, kisha akajipangusa kijasho kilichoanza kumtiririka. Walter akaanza kupiga mahesabu upya kabisa ya namna ambayo anaweza kutoka katika jiji hilo salama. Kwani aliamini alikuwa anatafutwa na polisi kwa udi na uvumba. Uamuzi alioufikia ni kutafuta mawasiliano na rafiki zake wa karibu ambao wanaweza kumpatia pesa kwa namna nyingine tofauti na benki. Akajisachi na kuipata kadi ya simu yake ambayo alikuwa akiitumia siku zote kabla ya kubadili wakati anaondoka jijini Dar es salaam. Akajibanza pembeni kidogo katika kibanda cha kuuza bidhaa ndogondogo, akabadili kadi ya simu yake. Akaweka ile ya zamani. Akaanza kutafuta majina kadhaa ya watu wanaoweza kumpa msaada. Akapata majina mawili matatu, akajaribu kupiga. Simu haikuwa na salio. Alijitazama mfukoni. Akashusha pumzi kwa kasi zaidi huku akifadhaika. Pesa iliyokuwa katika mfuko wa shati lake, shilingi elfu tatu haikuwepo tena. Akaghafirika. Akasonya mara kwa mara bila kujua ni kwa nini ardhi hii ya Tanzania inazidi kuwa chungu kwa upande wake. Walter akiwa bado hajajua nini cha kufanya, mara ghafla alijikuta amezungukwa na wanaume wawili. Miili yao ilionyesha kuwa aidha wanafanya kazi ngumu ama ni mazoezi yamewafanya kuvimba vifua. “Nini? Kwani nini?” alihoji Walter kwa uoga huku akijaribu kutafuta upenyo akimbie. “Upo chini ya ulinzi mkali.” Mmoja wao alijibu. Walter akataka kukimbia, akakumbana na watu wenye shibe zaidi yake wakamminya. Akatulia. Wawili hawa wakamkwida vyema na kumsihi awe mtulivu. “Lakini mimi sijabaka?” alijitetea Walter bila kuulizwa lolote. Badala ya kujibiwa walimshangaa tu. Walter akaanza kulia akidhani hiyo yaweza kuwa suluhu. **JIFUNZE: MATATIZO hayana njia maalum kwamba unaweza kuyachenga ukapita kushoto na yenyewe yaende zake kulia. Laiti ingekuwa hivyo basi kila mwenye macho angeyakwepa matatizo. MATATIZO yameletwa kwa ajili yetu wanadamu, hatuwezi kuyakimbia… njia sahihi ni kukabiliana nayo kwa kutumia utashi tulioumbiwa!! Wanadamu wengi hujaribu kuyakimbia matatizo ili waishi kwa furaha maishani mwao lakini mwisho wa siku hujikuta katika matatizo mengine makubwa zaidi na furaha zao hupotea moja kwa moja!!! Wanyama wa porini walipewa makucha na meno makali, ili wayakabili matatizo yao kwa kupambana na hata kuua, lakini WANADAMU tulipewa akili na mioyo ya kishujaa ili tuyakabili matatizo yetu. TUMIA AKILI YAKO SASA!!! __WALTER aliyakimbia matatizo jijini Dar es salaam, sasa Mbeya inakuwa chungu kwake… tatizo jipya!! ___LILIAN naye matatani!!! ITAENDELEA!!
Posted on: Wed, 02 Oct 2013 15:00:00 +0000

Trending Topics




© 2015