RIWAYA: KIZUIZI MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA - TopicsExpress



          

RIWAYA: KIZUIZI MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA NNE Samaki hawakuwa wakubwa kiasi cha kuugawana mwili wa Derick. Hatimaye kesho yake asubuhi wale wakongwe wa kukaa katika mwamba maarufu wa ‘Bismark’ wakagundua kuwepo kwa mwili wa mwanadamu eneo lile. Taarifa za kifo hicho zilichukuliwa katika hali ile ile ya ‘upelelezi unaendelea’. Magazeti ya Mwanza yakapata cha kuandika siku iliyofuata vifo viwili kwa kutumia bunduki. Huku Derick huku Bibiana. Chanzo hakikujulikana. Sasa nafsi ya James ilikuwa imetulia na aliamini kuwa suala lake la kufunga ndoa lingeendelea kuwa salama. Wazo la kumpigia simu Jose ili wamalize biashara ndio lilimfanya asifikie uamuzi wa kulala mapema badala yake akaamua kuonana na Jose usiku huo huo ili aweze kumalizana naye kwani habari aliyompa kwa kiasi kikubwa imemsaidia kuokoa ndoa yake. Bahati mbaya simu ya Jose haikuwa ikipatikana. James akaghairi kupiga simu uwanja wa ndege kwa ajili ya kuulizia nafasi ya kusafiri siku inayofuata. Usiku huo aliwaza mengi huku akimuunganisha Jose B kati ya wanadamu wanaotakiwa kufa ili aweze kubaki huru kabisa na ndoa yake ifungwe salama. “Nitampatia hiyo pesa kisha nitamuua…kwanza simjui asije kunigeuka tena huyu” alijiapiza James kabla hajalala. Akasinzia huku akimuwaza Jose B. Akiwaza jinsi ya kumuondoa duniani kimyakimya. ***** Mawazo aliyokuwanayo Jose B sasa alitaka kuyabadili na kuwa vitendo kamili. Wazo lake la kuondoka nyumbani na kuishi maisha ya kujitegemea katika nyumba ya kupanga lilimfanya aamue kutembea huku na huku na madalali wakimwonyesha nyumba za hadhi aliyokuwa anataka. Jioni ya siku ya jumanne Jose alikuwa chumbani kwake. Daftari mezani kalamu mkononi akipiga mahesabu ya jinsi atakavyoanza maisha mapya. Akaanzia kodi ya nyumba yenye choo na bafu ndani, isikose marumaru, kitanda cha futi sita kwa sita, mziki mnene, godoro lenye hadhi ya kuitwa godoro, luninga bapa, nguo za kisasa, kabati kwa ajili ya kuzihifadhia hizo nguo, meza, viti, ‘dressing table’, makochi aina ya sofa ya kisasa. Kama hiyo haitoshi Jose B akawazia pia kununua ka-pikipiki kadogo kwa ajili ya mizunguko ya hapa na pale jijini Mwanza watoto wa mjini wanasema ka-kuuzia sura, na pia kumhamisha mdogo wake shule. Mshtuko!! Jumla ikazidi pesa aliyoimiliki, Jose akaumia sana. Malengo yake yakaanza kuingiliwa na kizingiti. Pesa ilikuwa haitoshi. Na hakuna hata kitu kimoja alichotaka kukikosa kati ya orodha aliyoiandika katika daftari lake. Ghafla wazo la pili likamvamia, akajiweka katika utulivu. Akafunika daftari lake akaanza kuiumauma kalamu yake. Ikajijenga picha ya mwanamke mrembo wa haja, akiwa na furaha sana, hakuwa peke yake alikuwa na wenzake watatu wote walikuwa wakimsikiliza huku wakiwa na dalili zote za kumwonea wivu. Alikuwa anazungumzia suala la ndoa yake ambayo inatarajiwa kufungwa hivi karibuni. Jose B naye akajiweka katika mazungumzo hayo japo hakutia neno lolote lakini alinukuu vitu fulani. Alipotoka katika mawazo hayo Jose B akaibuka na wazo la kujiongezea pesa. Pesa kutoka kwa mke mtarajiwa wa James. Ladha ya biashara aliyoianza kwa mafanikio ya kuuza habari ikawa imemkolea. Jose akawa ameamua kuangalia uwezekano wa kuiuza habari hii mara mbilimbili. Kwanza ameiuza kwa James na sasa alihitaji kuiuza kwa Emmy. “Ili iwe tamu zaidi lazima nikijue hicho kizuizi.” Alijisemea Jose B huku akijilaza kitandani. Jose akavuta kumbukumbu zake na kupata jawabu la ni wapi ataanzia, akamfikiria Bibiana ndiye atakuwa suluhisho la tatizo lake. “Huyu nikimpa kama elfu ishirini hivi lazima aniambie tu!!.” Alijiapiza Jose huku akimuwazia Bibiana kama mtu masikini sana ambaye hiyo pesa itakuwa kama almasi kwake. Uamuzi huo ukawa sahihi katika kichwa chake. Hatua iliyofuata ikawa kuzima simu. Hakuzihitaji tena hizo milioni nne zilizobaki mikononi mwa James kwani aliamini kuwa kwa kumuuzia mwanamke habari atapata malipo maradufu kwani aliwatambua wanawake kuwa ni dhaifu sana. Jose B Waukweli akaamua kuzima simu yake ili James asiweze kumpata hewani pindi atakapomtafuta kwa ajili ya kumaliza biashara. Ni wakati huo huo James alikuwa akijaribu kumpigia ili waweze kuonana kwa ajili ya kumalizia malipo na kuiondosha roho yake. Kuzima kwake simu kukaisalimisha roho yake. Laiti kama angeyajua mawazo ya James…. Angejipongeza maradufu kutokana na uamuzi wake ule wa muhimu zaidi!! ***** Chumba kilikuwa tulivu, hapakuwa na maongezi tena kama ni stori za utotoni zote walishazungumza tayari kama ni kukumbushiana jinsi walivyotengana yote yalikuwa yamewatoka vinywani. Habari za jeshini na ugumu wa kuwapa akina mama wasiojua kusoma wala kuandika mikopo yote walikuwa wamesimuliana na kila mtu kumpa pole mwenzake kwa ugumu wa kazi anayoifanya. Kuna jambo walikuwa wanalirukaruka hawalisemi lakini sasa mioyo yao ikaamua kuzungumza, macho yakainuka kuiwakilisha mioyo. Chumba kikawa kimya, sasa pumzi zao zikawa zinasikika zikipishana kwa kasi. Mjeshi akausahau ujasiri na afisa mikopo akauweka pembeni ule umakini wake akiwa kazini. Kazi ya kuhesabu pesa za wateja. Kumbukumbu zikarudi miaka kadhaa nyuma, elimu ya chuo kikuu ikakikimbia kichwa cha Emmy, mikikimikiki ya kwata za jeshi la wananchi Tanzania ikausahau mwili wa Lameck. Ubaba mdogo na u-mtoto wangu ukatoweka ghafla. Mapenzi yakang’ara machoni, subira ikajificha. Bwana harakaharaka akaibuka. Tamaa akaongozana naye, hulka akamwamsha shetani aliyekuwa amelala. Shetani akamuua uvumilivu ndani ya mwili wa Emmy, akamsahaulisha juu ahadi nyingi alizompa James. Hisia akapata uhai na utawala katika serikali ya miili miwili kwa pamoja. Macho ya Lameck yakajaa huba kuliko yale ya James. Emmy akaligundua hilo, bila kutarajia akajikuta anamsogelea Lameck. Lameck upesi upesi akajikumbusha mazoezi ya kubeba vitu vizito jeshini. Akambeba Emmy mzegamzega hadi chumbani. Kitanda kikawatazama kwa namna ya kuwahitaji sana, mashuka meupe yakawavutia wote. Emmy akiwa kama aliyepoteza fahamu akajikuta uchi wa mnyama juu ya kitanda kile. Baadaye…………… Baada ya saa zima fahamu zikamrejea, shuka hazikuwa nyeupe tena bali kuna nakshi nyekundu zilikuwa zimejichora na kutia kinyaa kuzitazama!! Emmy hakuwa akiweza kutembea upesi. Alikuwa mfano wa mwanaume aliyefanyiwa tohara. Hakuna aliyemwangalia mwenzake usoni!!!! Bikra iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya James kwa kiapo cha ‘MPAKA NDOA’ ikavunjika mbele ya mjeshi kamilifu. Ndugu wa karibu kabisa!! *** Usiku wa mang’amung’amu ulimkumba Jose, alitamani asubuhi ifike upesi ili aweze kutimiza azma yake aliyoipanga ya kumwongezea kipato. Japo alichelewa sana kuupata usingizi lakini hatimaye usingizi ulimpitia na asubuhi aliyoihitaji ikafika. Aliwahi kuamka kabla ya wote pale nyumbani. Akafagia uwanja. Akajisafisha mwili na kisha akachomoa kwa tahadhari kubwa noti nyekundu nyekundu sita akaziweka katika pochi yake. Akaondoka. Saa mbili asubuhi akiwa na rafiki yake aliyempeleka mahali alipokuwa anaishi Bibiana, kauli mbiu ya ‘biashara asubuhi jioni mahesabu’ ndio chanzo cha kuwahi sana. Eneo lilikuwa na watu wengi sana, ni kama aidha ilikuwa harusi ama msiba. Jose akajipenyeza kimyakimya katika umati wa watu matusi aliyotukanwa kwa sababu ya kuleta usumbufu wa kusukuma sukuma watu hakuyajali sana alichokuwanacho makini ni pochi yake mfukoni. Hatimaye alifika mbele kabisa. Akakutana na askari wakamzuia asiendelee zaidi. Maneno maneno ya watu yakamshtua. Kuna jambo la kushangaza lilikuwa limetokea pale nyumbani kwa akina Bibiana, kulikuwa kuna tukio la mauaji. Dakika kadhaa baadaye mwili ukatolewa ndani. Kwa kuwa Jose B alikuwa mbele aliitambua sura ya Bibiana. Mapigo ya moyo yakaenda kasi zaidi aliposikia kuwa ameuwawa kwa kupigwa risasi. Hofu ikatawala akatokomea eneo lile bila kukumbuka kuwa hakuwa amekuja peke yake pale. Jose alikuwa amekumbwa na taharuki kubwa sana. amani ikatoweka. Mtu wa kwanza kumuhusisha katika mauaji haya alikuwa ni James. Jose alizifikiria zile milioni mbili alizopewa kama malipo kwenye biashara ya kuuziana siri, siri ya kizuizi. Katika mawazo haya Jose akaisaliti ile dhana yake ya kwanza kwamba zile pesa zilikuwa chache sasa aliziona kuwa zilikuwa nyingi sana kwa ajili ya kununua habari ile. Tena alipokumbuka kuwa bei ya habari hiyo ilikuwa ni milioni sita, akajipa uhakika kuwa pana kitu hapo!!!! Milioni sita kwa ajili ya kununua habari??? James ameua!!!! Alijiuliza Jose akiwa njiani kuelekea alipopajua yeye mwenyewe. Swali hilo likamfanya atetereke kimawazo. Maana jibu lake lilikaribiana na ndio!! Akajihisi yupo hatarini. Hatari ya kuuwawa. Kuuwawa kwa kuijua siri. Siri ya kizuizi!!! Na sasa siri ya mauaji. Nimemuua Bibiana!! Jose B alikiri…. Kivipi Bibiana afe!!! Kivipi mh!! Hapana kuna kitu. Kizuizi kimemuua Bibiana” Jose alizidi kujiuliza kisha akaamua kujipatia jibu mwenyewe. Wakati akijipa uhakika kuwa huenda ni kizuizi kimemuua Bibiana, alijiaminisha kuwa kizuizi hichohicho kinaweza kumtia yeye matatani. Hatia ya kuwa mbinafsi na kutomshirikisha yeyote tangu mchezo huu unaanza ikaanza kumtafuna, alitamani japo angekuwa amewahi kumshirikisha mama yake, lakini haikuwa hivyo. Sasa mambo yanaanza kuwa magumu. Majuto yanachukua nafasi. Ile pesa ikaanza kuwa chungu hata kabla haijatumika kufikia nusu. Mipango ya kumtafuta huyo mke mtarajiwa ikaonekana kuwa batili. Hatia ikatambaa vyema na kujikita katika moyo wa kijana huyu mwembamba, mrefu wa wastani mwenye macho makavu ya mviringo, kichwa chenye nywele chache lakini kikiwa na siri lukuki na mdomo mdogo lakini wenye maneno mengi. Jose B waukweli. Mara akawaza juu ya kuukimbia mji. Wazo hili akalifutilia mbali mara moja na kujiona kuwa anatawaliwa na uoga usiokuwa na mantiki yoyote. Kwanza huyo James hafahamu ni wapi ninapoishi. Pili .......akazima simu yake kisha akamalizia. “Pili sipatikani kwenye simu. Atanipataje?” ***** James aliamka mapema sana lakini hakubanduka kitandani. Jose B, bado alikuwa hapatikani kwenye simu. James aliamini kuwa Jose ameingiwa kiwewe kwa kuzipata pesa nyingi kiasi kile kwa pamoja, kwa mtazamo wa waziwazi alimwona Jose kuwa alitetemeka sana baada ya kupokea pesa zile za malipo, akaamini kuwa Jose atakuwa amejichimbia katika vilabu mbalimbali vya pombe akifaidi maisha ya kipekee ambayo kamwe hajawahi kuyapitia. James akampuuzia Jose B na kufikiria kwamba hana athari zozote katika mpango wake wa kufunga ndoa. James akazihesabia zile pesa alizompatia Jose, kwa maisha yake ya kimasikini hakika ingemchukua muda mrefu sana kuweza kuzimaliza. Mwanzo wa kuzimaliza zile pesa ndio ungekuwa mwanzo wa kutafuta mbinu za kupata pesa nyingine. Wakati huo ukifika tayari tangazo la tatu litakuwa limepita, na hapo James atakuwa amefunga goli la kisigino!!!! James akampuuzia Jose. Akajichukulia pointi zote upesi upesi na kujichukulia kuwa yeye ni mjanja kuliko Jose. “Kesho narejea Dar!!!” akajihakikishia James, kisha akaitwaa simu yake na kumpigia Emmy. Simu iliita mara ya kwanza haikupokelewa, mara ya pili hali ikawa ileile. “Katakuwa kanaoga ka-Emmy kangu!!!” alijisemea huku akiinuka kitandani. Naye akaelekea maliwatoni kukidhi haja zake. *** Almanusura hisia za James ziwe sahihi juu ya mchumba na mke wake mtarajiwa. Alihisi kwamba yu bafuni anaoga lakini hakuwa anaoga bali alikuwa anaugulia maumivu makali baada ya kuruhusu bikra yake itolewe na mwanajeshi sasa alikuwa anakandwa na mjeshi huyohuyo ili kupunguza adhabu ile ya kuchechemea huku akisingizia kuwa alikuwa ufukweni anaogelea mawimbi yakamchukua vibaya na kumrusha juu, akatua juu ya kitu kigumu. Aliporejea kutoka bafuni alikuta simu yake inawakawaka ishara ya simu iliyokosa majibu. Alipotazama kidogo aitupe chini, aliogopa alichokiona, lilikuwa jina la James ambalo alikuwa amelihifadhi kwa jina la kubuni la ‘Sweet husband’ jina hili lilikuwa likimfanya atabasamu siku chache nyuma sasa likaanza kumkosesha amani. Kile alichomuahidi James hakikuwepo tena. Aibu kuu. Sasa Emmy anaitazama ile simu kama mdudu wa kutisha ambaye akiguswa analeta madhara makubwa. Akatamani ampigie lakini hakuwa tayari kusikia jibu la mume mtarajiwa kuwa yupo njiani anakuja Dar es salaam. Wakati huo lilisalia tangazo moja tu ndoa iweze kuthibitishwa na kanisa. Ile subira aliyokuwanayo na matamanio makubwa ya kufunga ndoa yakaanza kuyeyuka. Akauona uchungu mkubwa ukimkabili baada ya kuifunga ndoa. “Au nisingizie kuwa ilitoka katika ajali ya wimbi la bahari?? Lameck ameniponza Lameck.” Alitafakari. Akiwa bado ametulia bila kujua ni dakika ngapi zimepotea akiwa hajafanya maamuzi, simu yake iliita. Alikuwa Lameck. Hofu nyingine tena. Kwanza aliona aibu kwa kitendo alichofanya na baba yake huyo, kisha akajivunja mshipa wa aibu akapokea. “Unaendeleaje kipenzi changu.” Sauti nzito ya Lameck ilimnong’oneza Emmy. “Lameck...acha kuniita mimi jina hilo tafadhali.” Alijibu kwa ukali Emmy “Nimeongea na mama amenambia upo chumbani peke yako na James bado hajarudi, kuna ubaya gani kwani mamii.” Lameck alibembeleza. Emmy akapagawa na mauzauza ya huyu bwana. “Lakini ninakaribia kufunga ndoa. Lameck please hebu tufanye kama hakuna kilichotokea ndugu yangu. Nakuomba nakuomba sana!! Lameck utaniharibia mwenzio” Emmy alisihi huku akijaribu kuizuia hasira yake. “Mimi sio muigizaji mamii, siwezi kabisa kujifanya sijui kilichotokea...Emmy si unajua nilikupenda nawe ulinipenda hapo kabla na hadi sasa...” “Ndio nakupenda Lameck lakini umeniharibia ujue...” “Kivipi?” “Jamaa anajua kuwa mimi ni bikra. Sa itakuwaje?” “Hayo ndo maneno sasa, kumbe hasira zote hizo ni hilo tu...njoo kesho home kwangu” “Kufanyaje sasa. Kufanyaje Lameck wakati tumeharibu tayari!!” “Njoo utafurahi.” Walimaliza maongezi baada ya makubaliano. Emmy alikubali lakini kwa shingo upande. Majuto yalikuwa yamemzidi nguvu. Akiwa bado anatafakari kidogo juu ya wito wa kwenda kwa baba yake mdogo, simu ikaita tena, sasa alikuwa James. Mume mtarajiwa. Hofu mpya ikajengeka. Lakini hakuwa na budi, akalainisha koo kwa kukohoa kisha akapokea simu akiulazimisha uchangamfu. “Vipi mpenzi umelala....” Sauti nzito ya James iliuliza. “Wala sema nilikuwa nawatch kideo sikuisikia simu yako...” Lile neno kideo likamshambulia ghafla James aliyekuwa ameketi kitandani, hakushtuka kwa sababu tu mpenzi wake alikuwa amejikita katika kutazama luninga, lakini lile neno kideo liliambatana na jambo jingine la muhimu sana. Ukiondoa KI linabaki jina DEO….. Mdomo ukawa mzito, Emmy aliendelea kukazana kuita ‘halo..halo..’ lakini hapakuwa na majibu. Mara simu ikakatwa. Emmy hakufanya jitihada zozote za kupiga simu, kwanza ilikuwa faraja kukwepa kuzungumza na James mazungumzo marefu.. Akajirusha kitandani aweze kufanya mtihani wa kuwaza na kuwazua. Wakati Emmy akijirusha kitandani, James alikiacha kitanda akasimama wima akakumbuka kuna tatizo kubwa anakaribia kuliacha jijini Mwanza. Deo. Huyu kijana na yeye alikuwa bega kwa bega kumfitini asiweze kufunga ndoa na Emmy John. Kuondoka huku akiiacha roho hii ikifurahia hali ya hewa ya jiji la Mwanza lilikuwa kosa ambalo mwisho wa siku litamfanya aaibike hadharani na kukosa nafasi ya kipekee ya kuwa mwanaume wa kwanza kushirikiana na Emmy. Safari aliyotaka kuiandaa kwa ajili ya siku iliyofuata akalazimika kughairi. Alikiri kuwa anafanya haya yote kwa ajili ya mtu anayempenda kwa dhati, tena muaminifu kwake. Laiti kama angejua ukauzu aliofanyiwa na Emmy, huenda angeubadili uelekeo. James akakiri tena kuwa alikuwa akimuhitaji sana Jose B waukweli ili aweze kumfanikishia mipango ya kuonana na Deo. Atampata wapi? hilo likawa swali. Katika simu ya mkononi hakuwa anapatikana. James akaulazimisha usingizi. Hatimaye akapitiwa. Usingizi ukapaa majira ya saa kumi alfajiri na kuelekea kwa wengine, ukawa umemtupa mkono James. Akabaki kugaagaa kitandani akijiuliza ni namna gani anaweza kukabiliana na Deo pamoja na Jose B kimya kimya bila kuwa hata na mawasiliano nao?? Akakosa jibu. Akasimama akaliendea begi lake dogo akatwaa tembe mbili za dawa akameza. Zilikuwa za kutuliza maumivu ya kichwa. Hakika James alikuwa amezidiwa. Akiwa katika kufikiri zaidi akakumbuka kuwa ameuwa watu wawili tayari, na wala hawakumuumiza kichwa na wala hakujuta. Kifo cha bwana mpenda kujua yasiyomuhusu kule ziwani hakikuwa na uzito sana. Lakini kifo cha Bibiana hiki kilikuwa cha kipekee, aliamini kitawavuta watu wengi sana, akakiri kuwa Deo kama patna wa marehemu Bibiana lao likiwa moja lazima atahudhuria mapema sana katika msiba huo na huenda hatabanduka hadi maiti ifukiwe kaburini na kama hiyo haitoshi hata matanga atayangoja. Pata potea. James akarusha karata kuwa huenda anaweza kupata hisia juu ya Deo katika msiba huo ambao utashangaza zaidi ya kuhuzunisha. Akaamua kuwahi mapema kabisa, miwani yake nyeusi machoni, kofia kubwa kichwani na ile hali ya hewa ya ubaridi akajificha ndani ya koti kubwa jeusi. Ilikuwa ngumu kumfahamu. *** **JAMES bado anahaha….. ameamua kuelekea msibani… Je? Atatimiza azma yake ya kumnasa Deo ….. **EMMY amepoteza bikra ilhali mumewe mtarajiwa na familia kwa ujumla wanatambua kuwa ni bikra….. MBAYA ZAIDI aliyeitoa ni ‘baba mdogo’ TOA MAONI YAKO TAFADHALI!!! ITAENDELEA KESHO!!.....
Posted on: Thu, 24 Oct 2013 15:00:00 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015