RIWAYA: MTAFITI MTUNZI: HUSSEIN TUWA SEHEMU YA MWISHO - - TopicsExpress



          

RIWAYA: MTAFITI MTUNZI: HUSSEIN TUWA SEHEMU YA MWISHO - PART 1 Mwisho wa ile ripoti kulikuwa kuna saini ya Grayson Mochiwa kama mtafiti mkuu kwa upande mmoja, na upande mwingine kulikuwa kuna sehemu ya kusainiwa na Luis Kambesera kama mwenyekiti mtendaji wa kampuni ile. Sehemu zote mbili kwenye ile ripoti iliyowasilishwa serikalini, zilikuwa zimesainiwa. Lakini wale askari waliona kuwa kulikuwa kuna utofauti kati ya zile saini mbili za Grayson Mochiwa kwenye ripoti zile. Saini ya kwenye ripoti moja ilikuwa imeghushiwa... ________________ Bilanga aliingia ofisini kwake pale Liquid Diamond na kupitiliza moja kwa moja hadi kwenye meza yake na kuitandika teke zito kwa kiatu chake kizito. “Pumbaaff!” Alijitukana kwa kushindwa kuutia mkononi ule mkoba ambao aliamini kuwa ndio ulikuwa na ule ushahidi ambao kwa hakika ungeisambaratisha ile kampuni yao kwa kiwango kikubwa kabisa. Na yeye alijua kuwa jukumu la kuhakikisha kwamba maswala yote ya kiusalama wa kampuni ile yanakuwa ndani ya mstari lilikuwa juu yake …yeye na Chabbi. “Shit! Chabbi naye hatoki tu huko mahabusu bloody kenges?” Alilaani tena na kujibweteka kitini. Akaangalia saa yake. Muda ulikuwa umesogea sana. Akampigia Suleiman Mwangi, mwanasheria wa kampuni. “Oya! Vipi kuhusu Chabbi? Namhitaji sana sasa hivi…muda wa kutoka si ndio umekaribia huu? Umesikia kuwa kuna mashitaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi yake?” Alimuuliza, na Mwangi akamjibu kuwa hakukuwa na mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi ya Chabbi mpaka muda ule. “Nenda kamtoe bwana! Mambo sio mambo huku!” Bilanga alisema kwa shinikizo, na kukata simu. Aliinuka na kwenda kwa Luis Kambesera ambaye alimkuta akiwa amejibweteka ki-hasara hasara ofisini kwake. Hakuwa ametoka kwenda popote siku ile na hata chakula kilimshinda kula siku nzima. “Oi! Mambo sio mambo…mpango wangu haukufanikiwa kule. Kweli jamaa wanao huo ushahidi. Nimehakiksha hilo…walikuwa na mkoba ambao walikuwa wamedhamiria kuulinda kwa kila hali usiwatoke!” Alimwambia bila ya utangulizi wowote. “Ohhh!” Luis alilalama kwa kukata tamaa. “Ooo nini sasa bosi? Hali ndio hiyo...inabidi tuingie kwenye plan B sasa...ama si hivyo meli inazama hii!” Bilanga alisema. “Oooh!” Luis alibwabwaja tena, na Bilanga akatupa mikono hewani kwa kukata tamaa. “Bosi. Tunahitaji kufanya kitu zaidi ya hizo ooooo, oooo zako sasa! Muda ni wa msingi sana, na Chabbi bado yuko himayani kwao. Nadhani yakupasa upige simu sasa!” Bilanga alizidi kumfahamisha. “Oooooohhoo!” Luis akazidi kuchanganykiwa. Jamaa alikuwa ameishiwa ujasiri kabisa. Bilanga akasonya na kuuelekea mlango wa kutokea nje ya ofisi ile, na alipofika pale mlangoni alimgeukia na kumtazama. “Piga smu hiyo bosi sasa! Mambo haya hayazibiki tena! Tutajitahidi kuyadhibiti kutokea hapa yalipofika, lakini plan B ni lazima…piga hiyo simu sasa hivi!” Bilanga alisema kwa hasira na kutoka nje ya ofisi ile. Huku nyuma Luis Kambesera alibaki akiwa amejiinamia huku akiwa amejishika kichwa kwa kukata tamaa. Alibaki katika hali ile kwa muda mrefu sana. Kisha akaguna na kutoa simu yake ya kiganjani. Akapiga simu ambayo alikuwa akichelea kuipiga kwa muda mrefu sana, na ambayo Bilanga alimsisitiza sana aipige, na ambayo naye pia alijua kuwa kwa pale walipofikia, hakukuwa na namna ya kujaribu kujiokoa katika zahma ile isipokuwa kwa kuipiga namba ile…na kuongea na mtu pekee ambaye angeweza kuwavusha kutoaka kwenye ile zahma ambayo yeye na wale watendaji wenzake wa Liquid Diamond Incorporated walijitumbukiza kwayo. “Na alaaniwe Inspekta Kwakwa, pumbavu zake!” Alinong’ona kwa hasira huku akiisikiliza ile simu ya yule mtu aliyempigia ikiita… ______________ “Sasa hii hali ni lazima iwekwe wazi mbele ya umma afande Kwakwa. Hawa jamaa lazima tuwaanike ili walichokifanya kijulikane!” Zay alisema, na Kwakwa akaguna. “Hapana Zay. Mambo hayaendi hivyo. Hii ni kesi kubwa sana iliyochukua uzito mwingine kabisa sasa. Hii sasa imekuwa uhujumu wa uchumi. Ni swala la Mkurugenzi wa makosa ya jinai mwenyewe sasa!” Kwakwa alimwambia, na Zay akamakinika. “Meaning what?” Alimuuliza, akimaanisha kwamba alitaka kujua ile kauli yake ilikuwa inamaanisha nini. “Okay…kiutaratibu, hatutakiwi kuiweka hadharani hii habari bali tuiwasilishe kwa wakuu kama ushahidi wa kuwatia nguvuni akina Luis…” Alimwambia, na Zay akatikisa kichwa kwa kukata tamaa. “Nilijua kuwa itafikia huko…nilijua tu! Mimi ndiye niliyeleta huu ushahidi, na Mwamtumu ndiye aliyehakikisha kuwa hauangukii mikononi mwa akina Luis na akapoteza maisha kwa hilo. Sasa tena unaanza kuleta habari za kuuweka ushahidi kwa mkurugenzi wa makosa ya jinai mpaka lini? Mi’ s’kubali bwana!” Alimjia juu. “Zay, we unajua ni jinsi gani mimi…sisi…tulivyo makini kwenye kazi. Na mpaka sasa unajua ni upande gani tuliopo katika hili. Lakini kama ulivyosema, Liquid Diamond ni kampuni kubwa. Tukikurupuka bila kufuata taratibu kwenye hili la uhujumu wa uchumi, wanaweza kuachiwa hivi hivi! Hapa ni kufuata taratibu tu Zay. Mchango wako na wa Mwamtumu mbona uko wazi tu? Tuamini sisi…tutahakikisha Luis na wenzake wanapata kinachowastahili!” Kwakwa alimwambia, na bado Zay hakuonekana kuridhika. “Na vipi akina Chabbi na Bilanga? Nao wanasubiri DCI apitishe taratibu zake?” Alihoji, akisema DCI kumaanisha Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai. “Wao kesi yao iko wazi… mauaji! Hao wako katika eneo letu la kujidai. Tunawatia nguvuni tu, na wao ndio watawataja wakuu wao! Chabbi hakumuua Grayson kwa utashi wake tu…na wala hakushirikiana na Bilanga kumuua Mwamtumu kwa kufurahisha nafsi yake tu. Alitumwa kufanya hivyo!” “Na Liquid Diamond chini ya Luis ndio waliomtuma!” Pojo alishadidia. “Exactly! So Liquid Diamond na Luis hawachomoki Zay. Si kwenye uhujumu wa uchumi, si kwenye mauaji. Swala hapa ni lipi kati ya haya mawili litawaganda mwanzo! Na kwa hali ilivyo, hili la mauaji ndilo litakalowanasa mwanzo. Na wakigandwa na hili, lile la uhujumu uchumi litawakuta tu…tuache taratibu zifuatwe tu juu ya hili la kuchakachua ripoti hii na kuihadaa serikali!” Kwakwa alimwambia. Zay akatikisa kichwa kwa masikitiko. “Kwa nini unakuwa mgumu kutuamini ghafla namna hii Zay?” Pojo alimuuliza. Zay alimtazama kwa muda. “Si kwamba siwaamini afande Pojo… sina mashaka nanyi hata kidogo. Ni huo utaratibu wenu ndio unaonitia mashaka…” Alimjibu. “Kivipi?” Zay akaguna. “Hivi haijawapitia akilini mwenu kuwa hawa Liquid Diamond watakuwa na mtu…au watu…wakubwa tu serikalini wanaowabeba? Watu humo humo serikalini ambao wameridhia Liquid Diamond iwasilishe ripoti feki kwa maslahi yao binafsi na ya hao Liquid Diamond vile vile? Did that not cross your minds? Au mnadhani kila mtu ana mioyo kama yenu ya kupenda kazi yake na uaminifu kwa taifa lenu? Get real, guys!” Zay aliwajia juu, na wale askari wakabaki vinywa wazi. “Okay, tunajua kunawezekana hilo, lakini taratibu zinatutaka tulishughulikie hili kwa mfumo huo Zay! Kama kuna mchezo mchafu ulioihusisha serikali kwa namna fulani katika hili, vitajulikana tu huko mbele, sio?” Kwakwa alimwambia, na simu ya Zay ikaita. Alipoipokea alibaini kuwa alikuwa ni mama Mwamtumu akimpigia kwa kutumia simu ya mmoja kati ya jamaa zake. Mama alimjuza kuwa Mwamtumu atazikwa kesho yake saa saba mchana kule shambani kwa mama yake, Gezaulole. “Itanibidi niende mazikoni kesho…Gezaulole!” Zay alisema baada ya kuongea na simu ile. “No!” Kwakwa alipinga. “Huwezi kwenda!” Pojo naye alipinga vilevile, na Zay akawajia juu. “Naenda! Rafiki yangu afe kwa kuwa nilishindwa kuwa naye wakati aliponihitaji, basi hata kwenye maziko yake nisiende? No way! Naenda!” “Uko hatarini sana Zay! Si umeona jinsi Bilanga alivyotukosakosa leo hii kule? Sasa hivi wewe ni sumu kwa Liquid Diamond, watakuwinda tu! Endelea kubaki chini ya ulinzi mpaka tuwadhibiti, kisha utaenda hata kuhani!” Kwakwa alimwambia. “Basi wawekeni chini ya ulinzi wao, sio mimi, khah! Mi’ lazima niende kwenye maziko ya rafiki yangu!” Zay alimjia juu, na Kwakwa na Pojo wakatazamana. “Look Zay. Tungeweza kwenda nawe na kukuwekea ulinzi muda wote ukiwa huko. Lakini sisi kesho tutakuwa na kazi kubwa ya kuwasilisha ushahidi huu kwa wakuu wetu na bila shaka tukahitajika kwa DCI…hatutaweza kwenda nawe huko…” “Sijataka mje nami! Nitaenda mwenyewe!” “Hauwi mwenye busara hapo Zay!” Pojo alimwambia. “Poa tu!” Kwakwa na Pojo walitazamana. Dakika ishirini baadaye alikuwa wakiongea na IGP pamoja na Mrakibu Mwandamizi juu ya ule ushahidi mpya uliopatikana, ile ripoti halali ya hayati Grayson Mochiwa mtafiti ikiwa mezani kwa IGP. “Lah! Lazima niseme kuwa hii ni kazi nzuri sana vijana! Mpaka hapa naona kesi imeshakamilika…tena ndani ya muda mliopewa. Kilichobakia sasa ni kuwakamata watuhumiwa wote na kuwaweka chini ya ulinzi kwanza. Kisha taratibu nyingine zitafuata…” IGP alisema, na Kwakwa na Pojo wakatazamana. “Yes sir!” Mrakibu aliafikiana naye, na kuendelea, “Sasa kwenye kuwakamata hawa watu, itabidi tupate nguvu ya ziada…wanatakiwa wote wakamatwe kwa wakati mmoja, hivyo basi, nitaongeza askari wengine kwenye hii kesi sasa, mkuu!” “Nakubaliana nawe!” IGP alimjibu, na Kwakwa akajikohoza kidogo. Wakamgeukia kwa macho ya viulizo. “Er, mimi nilikuwa naomba Bilanga na Chabbi Cheka niachiwe mwenyewe wazee…” Alisema. “Sioni tatizo kwenye hilo…isipokuwa tu kwamba Chabbi tayari tunaye!” Mrakibu alisema, “Sio kwa mauaji afande…tunaye kwa tuhuma za kuhusika na kupotea kwa Mwamtumu, ambaye sasa ni marehemu!” Kwakwa alisema. “Good point!” IGP aliunga mkono. Muda huo ujumbe mfupi wa simu uliingia kwenye simu yake, naye akausikia. Hakuusoma muda ule. Isingekuwa nidhamu kwa wale wakibwa zake. “Na vipi kuhusu hili la serikali kudangnaywa na hii Liquid Diamond?” Kwakwa alisaili tena. “Kiutaratibu nitaliwasilisha hilo kwa DCI…yeye atalishughulikia hili ipaswavyo. Uzuri ni kwamba bila shaka muda huo ukifika, watuhumiwa wote tutakuwa nao kwa tuhuma za mauaji ya Grayson na Mwamtumu! Hii ni open and shut case jamani, shukrani nyingi kwenu Kwakwa na Pojo!” IGP alisema, Pojo akihisi moyo wake ukipoteza mapigo pale alipomsikia IGP akimtamka kwa jina bila ya shaka yoyote. Dakika tano baadaye walitoka nje ya ofisi ya IGP wakiwa na ruhusa ya kuwatia mbaroni watendaji wote wa Liquid Diamond. Hakika ilionekama kuwa kama alivyosema IGP…ni open and shut case, kesi ya kufungua na kuifunag hapo hapo… Haikuwa hivyo. _____________ “Umenipigia…ina maana kuna tatizo kubwa!” Sauti iliyopokea simu ya Luis ilisema, na Luis akahisi kitetemeshi. “Er, ndio mheshimiwa. Hali imekwenda vibaya upande wetu…kopi ya ripoti ya mwanzo ya…” Luis alianza kuongea lakini jamaa alimkatisha. “Inatosha! Utaingia kwenye gari nitakalokutumia hapo ofisini kwako baada ya muda mfupi. Dereva atakuleta mahala ambapo tutaongea vizuri juu ya hili, okay?” Sauti ilimkatisha kwa kumpa maelezo. “Okay mheshi…” Luis alianza kujibu lakini ile simu ilikuwa imeshakatwa. Alibaki akiwa amepigwa butwaa akiitazama ile simu kama kwamba ndio kwanza alikuwa anaiona ikiwa mkononi mwake. Dakika ishirini baadaye, baada ya kupokea maelekezo ya simu, Luis Kambesera alitoka nje ya jengo la ile ofisi yale na kuingia kwenye sehemu ya nyuma ya gari aina ya Toyota Verosa nyeusi, yenye vioo vilivyotiwa weusi pia. Akiwa kule kwenye kiti cha nyuma alishituka kumkuta mwenyekiti wa kamati ya bunge inayosimamia maswala ya nishati akiwa ameketi kule nyuma. “Ah, mheshimiwa…si ulisema kuwa…?” “Dereva atakuleta mahala ambapo tutaongea? Change of plans…tutaongea humu humu garini…” Yule mtu miongoni mwa wazito kabisa nchini, ambaye pia alikuwa na wadhifa mzito na nyeti bungeni alimwambia. E bwana we! “Oh, okay…” Luis alisema huku lile gari likianza kuondoka taratibu eneo lile, mmoja wa wale askari wawili waliowekwa na Kamishna John Vata kumfuatilia Luis kila aendapo, alipanda pikipiki yake na kuanza kulifuata lile gari kwa umakini. Yule askari mwingine wa kike alituma ujumbe mfupi wa simu kwenda kwa Inspekta Kwakwa. “Kenge katoka bwawani, tuko makini nyuma yake. Fuatilia mmiliki wa Verosa Tango 636 Alpha Alpha Bravo.Yuko pamoja na kenge. O&O.” Ndio ujumbe aliomtumia Kwakwa. Yeye alibaki pale pale nje ya jengo lenye ofisi za Liquid Diamond, kusubiri iwapo Luis atafanikiwa kwa namna moja au nyingine, kumchenga mwenzake huko walipoelekea, na kurudi pale ofisini. ***Kumbe wazito wanaibeba Liquid Diamond? Nini kitajiri? ITAENDELEA LEO SAA SITA MCHANA, HAPA HAPA KONANI!!!
Posted on: Tue, 15 Oct 2013 04:00:00 +0000

Trending Topics




© 2015