RIYAA (SHIRKI ILIYOJIFICHA) Kilugha ‘Riyaa’ ni neno - TopicsExpress



          

RIYAA (SHIRKI ILIYOJIFICHA) Kilugha ‘Riyaa’ ni neno linalotokana na neno la Kiarabu ra-aa ambalo lina maana ya kuona, kutazama au kuangalia. Na haswa makusudio yake ni kujionyesha, unafiki na udanganyifu. Katika mtazamo wa kisheria Riyaa ina maana ya ‘‘kufanya matendo ambayo ni ya kumpendezesha Allaah lakini kwa nia ya kumridhisha asiye Allaah.’’ Au ni kufanya amali njema kwa makusudio ya kuonesha watu, ili uonekane ni mzuri au mwema kuliko ulivyo, ama upate kupendeza machoni mwao au upate kilicho mfukoni mwao au cheo. Na hii Riyaa ni namna ya shirki, kadhalika ni namna ya unafiki au wizi. Hivyo basi yoyote mazuri yafanywayo kwa kutaka na kutaraji manufaa ya kilimwengu na sio kumridhisha Muumba, basi yanageuka kuwa ni matendo ya kishetani. Riyaa ni moja ya mafungu ya matendo hatari mno ambayo ni vigumu sana kwa wengi kuyachuja na kuyatenga mbali na matendo yao. Ni vizuri na muhimu kuweza kulichunguza tatizo hili na kulijua undani wake ili tuweze kupambana nalo na kulitibu kwa ajili ya kufikia mafanikio ya kusafisha amali zetu na kukamilika Uislam na Uchaji Allaah wetu. Wanachuoni wa Ahlus-Sunnah wameelekea katika Qur-aan na Sunnah sahihi pamoja na mwelekeo wa wema waliotangulia ili kupata tiba ya ugonjwa huu hatari. Ni muhimu kuangalia hii Riyaa ilivyo tujue madhara yake na jinsi ya kutafuta kinga au ponya yake. NIYYAH Ni muhimu sana kufahamu maana ya Ikhlaas (utii kamili, kuitakasa niyyah) yaani kufanya jambo kwa ajili ya Allaah pekee. Hadiyth ifuatayo yatuonyesha namna gani tunapaswa kutilia umuhimu mkubwa juu ya Ikhlaasw na kuwa mbali na Riyaa. ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Allaahu anhu) kamnukuu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Hakika matendo yanatokana na niyyah, Na kila mtu atapata (malipo) kwa kile alichonuia … [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd]. Na Qur-aan vilevile inaonyesha na kueleza umuhimu wa ikhlaasw pale Allaah Aliposema: {{…wala msitoe ila kwa kutafuta radhi ya Allaah…}} [Al-Baqarah: 272]. Kizazi cha mwanzo cha Uislam kilizingatia mno umuhimu wa ikhlaas na jinsi ya kusafisha na kuzisahihisha niyyah zao. Tunapata mfano mzuri kutoka katika mapokezi haya ya Ibn Mas’uwd (Radhiya Allaahu anhu) aliyoyapokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Maneno pekee hayana faida kama hayajafuatiwa kwa vitendo, na maneno na vitendo pekee havina faida kama hadi yawe na niyyah safi. Na hayo maneno, vitendo na niyyah safi, yote hayana faida hadi yawe yamekubaliana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo basi, tunaona kuna mfululizo wa masharti ambayo ndiyo yanayosababisha vitendo vikubalike na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Sharti la kwanza ni kwamba lazima kitendo kifanywe kwa ajili ya Allaah pekee. Sharti la pili kitendo hicho kiwe kimekwenda sambamba kulingana na mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisiwe ni kitendo cha uzushi kilichoanzishwa na watu. HATARI AU MADHARA YA RIYAA 1. Shirki iliyofichikana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mapenzi yake makubwa mno kwa ummah wake alikuwa akichunga sana na kuchelea maafa kwa ummah wake kuliko mtu mwengine yeyote. Abu Sa’iyd (Radhiya Allaahu anhu) anaeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakuta wakijadiliana kuhusu Dajjaal na akawaambia: ‘‘Je, niwajulisheni kile nikikhofiacho zaidi kwenu kuliko hata hatari za Dajjaal? Basi ni shirki iliyojificha. Mtu anasimama kuswali, anaipamba na kuiremba swala yake kwa kujua kuwa kuna watu wanamtazama.’’ [Sunnan Ibn Maajah, namba 3389]. 2. Inadhoofisha imani na kumpwekesha Allaah Kwa kufanya Riyaa, mtu huwa anaiangamiza lengo kuu la uumbwaji, kwani badala ya kumuabudu Allaah, huwa anafanya ibada lakini kwa lengo na nia ya kuwaridhisha waja na kupata sifa kutoka kwa viumbe na wala si kwa ajili ya Muumba. Allaah Anasema: {{Sikuwaumba majini na wana Aadam ili wapate kuniabudu}} [Adh-Dhaariyaat: 56]. Vilevile Allaah Anawasifia wale waumini wa kweli wanaofanya matendo ya ibada zao kikamilifu na pekee kwa ajili yake Allaah na wala hawahitaji malipo au shukurani kutoka kwa viumbe wenzao. Anasema Allaah: {{Na (hao waumini) huwalisha chakula maskini na mayatima na wafungwa, na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho). (Hujisemea wenyewe katika nyoyo zao wanapowapa chakula hicho) Tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Allaah (tu) hatutaki kwenu malipo wala shukurani}} [Al-Insaan 8-9]. Na pia kwa upande wa pili kinyume na hao Allaah Anawaelezea wengine kwa kusema: {{Basi ole wao wale wanaoswali Swalah zao (kinafiki). Ambao wanapuuza maamrisho ya Swalah zao. Ambao hufanya (amali zao ili waonekane na watu) Riyaa. Na huzuia misaada (basi Swalah zao hazina faida).}} [Al-Maa’uwn: 4-7]. 3. Inazidisha upotofu Hakuna shaka mtu mwenye kufanya Riyaa huwa ni mwenye maradhi moyoni mwake, na kama ugonjwa huo hautotibiwa, uatapelekea kwenye matatizo mengi zaidi. Kulingana na hili Allaah Anasema: {{Wanajaribu kumdanganya Allaah na wale walioamini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui. Nyoyoni mwao mna maradhi (ya mashaka na unafiki), na Allaah Amewazidishia maradhi…}} [Al-Baqarah: 9-10]. 4. Inapokonya baraka ya matendo Katika Hadiyth nyingi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaelezea kwamba Allaah Hapokei matendo yanayofanywa kwa ajili ya kuwaridhisha viumbe. Amepokea Mahmuwd bin Labiyd (Radhiya Allaahu anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: Allaah Mtukufu Atasema wakati Akiyahesabu matendo ya viumbe (kuwaambia waliofanya Riyaa), ‘‘Nenda kwa wale uliokuwa ukiwaonyesha matendo yako (duniani) uone kama utapata malipo yoyote kutoka kwao.’’ [Swahiyh at-Targhiyb wat-Tarhiyb namba 29]. 5. Inamzuia mtu kwenda peponi Kufanya matendo mema kwa ajili ya kusifiwa na kuridhisha watu, huenda yakapelekea kumzuia mtu kuingia peponi. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu anhu) amemnukuu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Yeyote anayechuma elimu ambayo anapaswa kuitumia kwa ajili ya Allaah, (kisha akaitumia) kwa nia ya kupata manufaa ya kilimwengu, hatonusa hata harufu ya pepo siku ya Qiyaamah. [Abu Daawuwd namba 3656, na Ibn Maajah namba 255]. MAMBO YANAYOSABABISHA RIYAA KWA UJUMLA Kiburi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). kasema: ‘‘Kibr ni joho langu na ukubwa (utukufu) ni kanzu yangu, hivyo yeyote anayetaka kushindana nami (katika sifa hizo), basi nitamtosa katika Jahanam’’ [Swahiyh Muslim namba 6349]. Kisha Allaah Ameeonya vikali kwa mwenye kutumbukia katika sifa hii aliposema: {{Usidhani wale wanaofurahia mambo (mabaya) waliyoyafanya na wakapenda kusifiwa kwa yale wasiyoyafanya; usidhani wao watasalimika na adhabu; (hapana, bali) itakuwa kwao adhabu iumizayo.}} [Al-‘Imraan: 188]. Kujionyesha na kujisifu Allaah Anasema katika Qur-aan: {{Hakika wanafiki wanataka kumdanganya (hata) Allaah Atawaadhibu kwa huko kujaribu kwao kumdanganya. Na wanaposimama kuswali, husimama kivivu (na kichovu) na ni kuchache mno kumkumbuka kwao Allaah}} [An-Nisaa: 142]. Pia mtu kufanya ibada kwa bidii na kuiremba na utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu kwa sababu kuna watu wanamuona au kumtazama, lakini anapokua peke yake ibada ile huifanya kwa haraka haraka na kilegevu na uchovu kama mtu aliyelazimishwa. Ama mtu anatoa msaada au sadaka pale anapoona watu wapo au kuna mtu ambaye anamuheshimu au kumjali yupo hapo. Ni mfano wale tunaowaona wanapotoa mchango au msaada wanaita waandishi wa habari na wapiga picha na televisheni wachukue maelezo na picha wakati anapotoa ili ulimwengu wote ujue fulani katoa na ni mtu mzuri! Ajabu, yote hayo ni kwa maslaha ya kiulimwengu na hakuna nafasi ya Allaah ya kutiiwa na kuridhishwa. Allaah Hakuliacha hili pia kulikemea: {{Kwa yakini hao hawatokufaa chochote mbele ya Allaah. Na hakika madhalimu ni marafiki wao kwa wao. Na Allaah ni rafiki wa wale wenye kumcha.}} [Al-Jaathiyah: 19]. Kumridhisha Allaah na hapo hapo huwaangushi viumbe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ‘‘Allaah Mtukufu Anasema: ‘‘Mimi ni mwenye kujitosheleza, sihitaji msaada wala mshirika. Kwa hiyo, yule afanyaye kitendo kwa ajili ya kumfanyia kiumbe (na hapo hapo anakifanya kwa ajili Yangu), (sitokihitaji kitendo chake hicho) nitamwachia huyo aliyemfanyia kunishirikisha Nami’’ (hatopata ujira wowote kwa kitendo hicho). [Swahiyh Muslim namba 7114]. Mavazi Suala la mavazi linaweza kumsababishia mtu kuingia katika Riyaa, mathalan, utakuta mtu anavaa vizuri akishindana na kila mitindo mipya itokayo na akitaka watu wamuone kuwa anakwenda na wakati. Na mtu mwingine akawa anavaa ovyo ovyo (akijiweka kama hao wanaojiita madaruweshi) akionyesha watu kuwa haijali dunia bali yeye ni wa Akhirah tu n.k. Wengine wakivaa mavazi fulani fulani yanayoonekana ya kidini ili asemwe kuwa yeye Shaykh au Mwanachuoni. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: {{Na unapowaona, miili yao inakupendeza, na wanapoongea, unasikiza usemi wao (kwa vile unavyovutia na kupendeza); lakini wao ni kama boriti zilizotegemezwa; (kama magogo ya miti isiyo na faida); wanadhani kila kishindo (kinachosikika) ni juu yao (kinawatafuta wao). Hao ni maadui, jihadhari nao. Allaah Awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki!!}} [Al-Munaafiquwn: 4]. Watu kama hao tunao katika jamii yetu, ambao kazi yao ni kutumia ulimi wao kudanganya watu na kufitinisha baina ya Waislam, na kuwazulia watu mambo kadha wa kadha ili wasiwe na thamani katika jamii! Na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba jamii inafunika maovu yao na inashirikiana nao na kuwapa nafasi katika mambo ya dini na uongozi. MAMBO YENYE KUHUSISHWA NA RIYAA Sifa zisizokusudiwa Endapo watu watahudhuria shughuli ya dini kama mhadhara n.k. ambapo kuna manufaa na kunafanywa kwa Ikhlaasw, si kunafanywa kwa malengo tofauti kama ya kujionyesha kwa watu kuwa mnaisimamia dini na hali hamna malengo yoyote wala hamjali kinachozungumzwa hapo kinafanywa kwa ikhlaas au kwa sifa na kutaka tu watu waseme: ‘‘jamaa wanafanya harakati maa shaa Allaah.’’ Shughuli kama hiyo ikiwa ni ya Ikhlaasw na wasikilizaji wakampongeza Mhadhiri, basi pongezi hizo hazitomharibia vitendo vyake maadam hajaigeuza au kuibadili ile nia yake kutoka kwa ajili ya Allaah na ikageuka ikawa ni kwa ajili ya wale wenye kumpongeza na kumsifu. Abu Dharr (Radhiya Allaahu anhu) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). ‘‘Ee Mjumbe wa Allaah! Je, unaonaje kama mtu anafanya matendo mazuri, kisha watu wakamsifia kwa matendo yake? Akajibu: ‘‘Hiyo ni sehemu ya baraka na radhi kwa Muumini (zitakazohifadhiwa kwake siku ya Qiyaamah. [Swahiyh Muslim namba 6388]. Lakini awe makini mwenye kupongezwa au kusifiwa kwa matendo yake mazuri, kuwa pongezi hizo anazosifiwa akiwa ni Mhadhiri, Msomaji Qur-aan au Mdarisiji, zisije zikambadilisha nia yake na akawa kila mara anafanya jitihada zaidi kuremba mawaidha au kisomo chake ili azidi kusifiwa na kupata umaarufu! Kuna wengine maskini hujitahidi na kujipinda, majasho yakawatoka na koo likawakauka kuiga watu mashuhuri ili wasifiwe na kufananishwa nao. Pia wenye kumwaga sifa, nao watoe sifa au pongezi zao kwa ikhlaas na si kinafiki. Maana utawasikia wengine wakiwaendea wenye kuwasifu na kusema ‘‘Al-Habib, si mchezo mawaidha ya leo, maana nakwambia watu wote walikuwa wamezimia.’’ Kama vile huyo Mhadhiri alikuwa hawaoni hao watu. Au mwengine atasema: ‘‘Muadhamu, leo ulikuwa ukitoa kama Sheikh fulani Wallaahi’’!! Sifa kama hizo ambazo mtoaji anazitoa na hali anajua ni kujipendekeza tu kwa huyo amsifiaye na kutaka aonekane mzuri, ni sifa za kinafiki na tabia chafu ambayo hupelekea wale wenye kufanya matendo mazuri, wakaathirika na wakawa hawafanyi tena kwa ajili ya Allaah, bali kwa kuwafurahisha hao akina Al-Habib na kina Al-Muadham. Na siku zikikosekana hizo sifa, basi huyo aliyezoea kusifiwa, anakuwa mnyonge na huenda pia ikapelekea hata mwisho kuacha shughuli hizo za kheri kwa ajili hakuna sifa wala kushukuriwa, au akaacha kwenda kwenye mhadhara kwa kuwa hawatokuwepo watu wengi na hatosikika. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ‘‘Ukiwaona wale wenye kuwapa watu sifa, wamwagie vumbi usoni mwao.’’ [Swahiyh Al-Bukhaariy namba 830, na Swahiyh Muslim namba 7143]. Mwengine ataudhiwa na watu na atasusia hata kushiriki katika shughuli hizo na kuapa, lakini baada ya muda unamuona huyoo yuko nao tena na akiulizwa vipi anadai aah nimeona nifanye maana haya ni maslahi ya Uislam, sasa je, hayo maslahi ya Uislam hapo alipojitoa mwanzo alikuwa hayajui? Huko ni kukosa Ikhlaasw. Na matendo kama hayo yanafanya mtu asiaminike pande zote hata na hao wanaoshirikiana naye, kwani wanajua kama aliwahi kususa basi hawezi kuacha kususa tena na huko mbeleni. Maana huyo hafanyi kwa ajili ya Allaah bali ni kwa ajili ya watu. Kususa kunakokubalika ni pale watu wanapokuwa katika misimamo inayopingana na Dini kama watu wa bidah na wale wanaowatetea watu wa bidah na kushikamana nao; hao ndio wanaopaswa kususwa kama zilipokelewa kauli nyingi kutoka kwa Mtume, Maswahaba na wema waliotangulia kuhusiana na hilo. Kutotaka kuwaangusha watu Kuna wengine wana tabia ya kuridhisha watu na kutotaka kuonekana wabaya, hata kama itakuwa ni kufanya tendo lisilo kwa ajili ya Allaah au la uzushi, au tendo la kheri lakini ndani yake kumekusudiwa shari. Na watu kama hao hawataki kuwavunja wengine kwa matakwa yao, ima kwa nia ya kujenga urafiki, au kupata maslaha fulani au kumkomoa fulani au asichukiwe ikiwa atakataa. Kwa hiyo atafanya jambo hata kama anajua fika ndani ya jambo hilo hakuna ikhlaas wala yeye mwenyewe haliamini kama ni sahihi. Na wakiulizwa kwanini wanafanya jambo ambalo halina Ikhlaas ndani yake, hutoa udhuru zaidi ya sabini. KINGA NA NJIA ZA KUZUIA RIYAA 1. Kuongeza elimu Mojawapo ya kinga ya matatizo mengi yanayowakabili Waislam, ni kuongeza elimu zaidi na sahihi kuhusu dini yao. Tunajua kuwa elimu chache ina matatizo na elimu kubwa isiyo sahihi nayo ni msiba. Na kuwa na elimu sahihi ndipo utakapoweza kupambanua haki na batili na yale yenye utata yaliyofichikana, na pia ndipo utakapofikia lengo la kumcha Allaah. Allaah kwa kulithibitisha hili Anasema: {{…hakika wanaomcha Allaah miongoni mwa waja wake ni wale Wanachuoni}} [Faatwir: 28]. Ni muhimu kutambua kwamba, kutafuta elimu sahihi ni jukumu la kila Muislam mwenye kumcha Mola wake, na wala si jukumu tu la Viongozi wa dini kama Masheikh, Maimaam, Maustadh n.w. Kuna wengi miongoni mwetu hawajishughulishi kusoma dini yao wala si jambo lililozoeleka kukuta katika nyumba za Waislam maktaba au hata vitabu vichache muhimu vya dini! Na sahemu nyingine kama Ulaya, utakwenda kwenye nyumba ya Muislam ukakosa hata Qur-aan! Wengine hawajui hata Qiblah kilipo. 2. Du’aa Katika kizuizi na chukizo kubwa la Riyaa na kilicho chepesi kukifanya ni du’aa. Abu Bakr Asw-Swiddiyq amemnukuu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ‘‘Shirki iliyomo ndani yenu inajificha zaidi kuliko mtambao wa sisimizi (si rahisi kuonekana), na nitawaambia kitu, mtakapokifanya, basi kitawaondoshea ndani yenu Shirki ndogo (Riyaa) na kubwa. Sema: ‘‘Allaahumma iniy auwdhu bika an ushrika bika wa ana a’alam, wa astaghfiruka lima la a’alam” (maana yake: “Ee Mola wangu, naomba unihifadhi na kutomuabudu mwengine asiyekuwa wewe (kushirikisha), na naomba msamaha kwa (kufanya) kile nisichokijua.’’ [Swahiyh Al-Jaami’. namba 3731]. 3. Kufikiri juu ya Pepo na Moto Jambo la tatu lenye kusaidia kumweka mtu mbali na Riyaa ni daima kuzingatia juu ya siku ya kiama. Mazingatio ya siku ya Qiyaamah yanasaidia sana kukuza khofu ya Jahannam, na kuongeza matashi ya kuipata Pepo. Ikiwa mwanaadam atazingatia kuwa lengo kuu la kuishi kwake hapa duniani si kupata umaarufu na sifa, bali ni kujilinda na adhabu ya Moto na kutaraji kuingia Peponi, atajaribu kwa kadri ya upeo wake kujiepusha kabisa na Riyaa. Allaah Anasema katika Qur-aan: {{… Basi anayependa kukutana na Mola wake na afanye matendo mazuri na asimshirikishe yeyote katika ibaadah ya Mola wake}} [Al-Kahf: 110]. Ndugu Waislam, tujue kuwa Riyaa ni kinyume cha Ikhlaasw, palipo na Ikhlaasw hapana Riyaa, na palipo na Riyaa hapana Ikhlaasw. Tujitahidi kutazama nafsi zetu na kujihesabia matendo yetu tuyafanyayo kila siku, tunapotaka kufanya tendo lolote, ni vizuri tujiulize kwanza, ‘‘Je, nafanya hili kwa ajili ya Allaah pekee? Au kwa sababu ya fulani? Ili afurahi au aridhike n.k. Ni tatizo ambalo si rahisi mtu kuligundua katika nafsi yake ndio maana Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) akalifananisha na mtambao wa mdudu chungu au sisimizi. WA ALLAAHU AALAM
Posted on: Fri, 22 Nov 2013 05:35:09 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015