Rebecca (49) Ilipoishia jana... Kwanza mama yake hakuamini - TopicsExpress



          

Rebecca (49) Ilipoishia jana... Kwanza mama yake hakuamini habari hii. Alidhani kuwa huenda binti yake aliongea vile kwa sababu alimchukia James au kwa sababu ya kutoelewana kati ya James na Isabela. Kwa hivi hakuona sababu ya mwanawe kumshutumu James kwani mtu yeyote anaweza kufanya mauaji hayo na kwa sababu nyingine tofauti na aliyoitoa yeye. Endelea... Kama aliyehisi kutoeleweka kwa mama yake, Rebecca aliinuka kwenda chumbani na baada ya sekunde chache alirudi akiwa na simu mkononi na kumkabidhi mama yake. “Hii ni namba ya gari la yule jamaa niliyemuona kituo cha polisi siku ile na mtu huyo nimeambiwa na Isabela kuwa ni mpambe namba moja wa James na siku ile hotelini alikuwepo.” Mama yake akaipokea na kuanza kuzisoma zile namba, “TRM 85II” Alipomaliza kuzisoma alimrudishia simu na kukaa kimya akitafakari kama anayeanza kumuamini. Kimya kikatawala kati yao, huku wakionekana kama wanatafakari. Ukimya wao ukakatishwa na ngurumo za magari yaliyokuwa yanaingia eneo la kuegeshea magari. Ziliponyamaza ngurumo hizo, zikafuata vishindo vya miguu vikiambatana na sauti ya vicheko na maongezi. Wote kwa pamoja hawakupata shida kuwajuwa waliokuwa wanaongea. Alikuwa ni mzee Kimaro na James Maganga. “Hata sasa unaona ulivyokuja kuliko ungaliishia kule kule kwa bwana Jumbe. Hujakanyaga hapa wiki sasa, unataka mchumba wako akusahau?” Ikasikika sauti ya mzee Kimaro. “Hapana mzee wangu nilipanga kuja hapa kesho mchana. Leo nilikuwa busy sana. Mizunguko ilikuwa mingi, hata mwenyewe umeona nilivyochelewa kwenye kikao na bwana Jumbe kinyume na makubaliano yetu?” “Ni kweli bwana umechelewa sana. Miadi yetu ilikuwa tukutane saa moja unusu jioni. Wewe umekuja saa nne kasoro kidogo wakati tunamalizia. Naona kesi zimekuzidi umri!” Wakaangua kicheko wote wawili huku tayari wameukaribia mlango. Mzee Kimaro akagonga na Rebecca alishafika mlango hapo na kuufungua. Wakaingia ndani huku mzee Kimaro akiwa mbele na James akasimama mlangoni. Alikuwa amevaa nguo nyeusi tupu hadi viatu na alikuwa amevalia koti refu lililoishia chini kidogo ya magoti kama yale wavaayo madaktari, lakini hili lilikuwa jeusi. “Woow! My Rebecca hujalala tu hadi muda huu. Vipi kitabu umenitafutia mama?” Mzee Kimaro alifurahi kumuona bintiye tena na kumchangamkia huku akitabasamu. Kinyume na matarajio yake, aligundua Rebecca huyu hakuwa yule waliyeongea naye jioni. Rebecca wa jioni alikuwa mchangamfu na asiyekuwa na hata chembe ya hasira. Rebecca huyu wa sasa, alikuwa mkavu na alikuwa kama mtu asiyewahi kucheka kwa muda wa mwaka mzima. Macho yamemuiva na kuvimba kiasi yakionesha dalili ya kulia muda mfupi uliopita. Akajua tayari jini wake ameshampanda. Hakupata jibu lolote wala tabasamu kama jioni. Akaachana naye na kumpita pale aliposimama, akaenda kukaa karibu na mkewe. Sasa Rebecca akawa anakabiliana na James aliyekuwa bado amesimama mlangoni akimwangalia Rebecca huku anatabasamu. Rebecca akavunga kucheka huku anamfuata pale mlangoni taratibu. “James vipi mwanangu, mbona umeishia mlangoni, pita ndani.” Mama Rebecca akamsisitiza James. “Wala usijali bi mkubwa. Ngoja nisalimiane na mamaa hapa.” Rebecca alizidi kumuelekea James pale mlangoni na James alipomuaona anamkaribia, akainua mikono yake kujiandaa kumkumbatia. Walipokaribiana, Rebecca akamkwepa James kwa kupita ubavuni mwake upande wa kulia kuelekea nje. Katika harakati hizi, mkono wa Rebecca ukagonga kitu kama pochi lililoning’izwa kiunoni mwa James. Pochi hili lilikuwa na urefu wa kama ziraa moja na lilionekana kuwa na kitu kigumu ndani yake mfano wa chuma. Halikuweza kuonekana kwa kuwa lilifunikwa na lile koti refu. Kama ambaye hakuhisi chochote, Rebecca akapitiliza haraka hadi nje. Na James akaelekea sebuleni pale walipokaa wazazi wa Rebecca. Alikaa karibu nao kuilekea televisheni ambako sasa kulikuwa na taarifa ya habari za kimataifa. Kule nje, Rebecca alienda hadi lilipoegeshwa gari la James, alipofika akalitambua gari hili na kukumbuka aliliona wapi. Kwanza aliliona hapa hapa siku nyingi nyuma ambapo James alikuwa hakauki. Pili ameliona kule kituo cha polisi na yule jamaa. Na tatu ni leo hii hapa hapa kwao. Mara mbili lilikuwa chini ya James na mara moja lilikuwa chini ya Lis G. akaendelea kulikagua kwa msaada wa mwanga wa taa iliyowaka pale nje. Karibu na mlango wa dereva kwa kutokea mbele, akaona jina la gari lililoandikwa kwa herufi za chuma Mercedice Benz C200. Halafu akalizunguka kwa nyuma hadi sehemu ya namba za gari, hapo alikutana na namba “TRM 85II” zile zile alizoziona kule kituoni na kuzihifadhi kwenye simu. Herufi mbili za mwanzo zilifanana na zile zilizotajwa na mashuhudi kwenye taarifa ya habari, yaani TR, pia namba moja ya mwisho ilioana na ile iliyotajwa kwenye taarifa hiyo ya habari, yaani II. Zaidi ni aina ya gari na rangi yake ni vile vile. Hakuwa na shaka kuwa James amehusika katika mauaji ya Isabela na Mary. Hata kama siyo yeye aliyefyatua risasi, lakini atakuwa anahusika kufadhili kwa kila kitu; kuanzia fedha, na vitu vinginevyo kufanikisha mauaji hayo. Kadhalika kile chuma kilichofungwa pale kiunoni mwa James, nacho kilikuwa ni ushahidi tosha wa kuhusika na mauaji. Alijipa asilimia mia moja kuwa ile siyo simu ila bastola. Akakumbuka pia mavazi aliyovaa hasa lile koti refu jeusi. Ni yale yale yaliyosemwa ila wakati huu hakuwa na vitambaa vya kuficha sura wala gloves. Kwa mambo haya ni wazi kuwa James alikuwa ni muuaji wa Isabela na kumjeruhi Mary. Pengine ujio huu amekuja kummaliza na yeye kama sababu ya kufanya mauaji yale ni kuficha siri. Ni kweli anataka kuficha siri kwa kuwa Isabela alikataa kuungana naye katika mpango wake wa kumuangamiza John bila kosa. Hivyo kwa kuwa Isabela amekataa kushirikiana naye amemuua. Vipi akigundua kuwa ile siri ameishaitoa na aliyepewa ni yeye, itakuwaje. Bila shaka bastola iliyotumika kumuondoa Isabela na kumjeruhi Mary, itatumika kumtawanya na yeye pia. Akaendelea kulikagua lile gari na kugundua kuwa milango haikuwekwa lock na dirisha la mlango mmoja halikupandishwa kioo. Akasogea dirishani hapo na kuangalia ndani. Kwa msaada wa ule mwanga, alifanikiwa kuuona mkoba mmoja mweusi katika siti moja ya nyuma. Akaingiza mkono na kuuchukua kuutoa nje. Akasogea pembeni ya gari kidogo na kuanza kuupekuwa. Akakuta ndani yake vitambaa viwili na alipovianglia vizuri akagundua vilikuwa ni vile vitambaa vilivyotumika kufunika kichwa na kuacha sehemu ndogo ya macho. Pia akazikuta gloves jozi mbili, chupa moja kama ya perfume, bomba la sindano na sindano yake na kulikuwa na chuma cha urefu wa kama nusu rula kilichokuwa na uwazi katikati. Alipohakikisha hakuna kitu kingine, aliupachika ule mkoba begani pake na kutembea kwa tahadhari hadi kwenye kibanda cha mlinzi. Akamkuta amesinzi kidogo huku silaha yake ameipakata. Akamsogelea kwa hadhari na kuichukua bunduki. Akarudi nyuma kwa mwendo kama aliokuja nao. Alipokiacha kibanda cha mlinzi kama mita kadha aligeuka na kukimbilia ndani kwa kasi. ********** Rebecca anaridhika anaridhika na ukaguzi wake na kujipa uhakika aisilimia mia moja kuwa Maganga anahusika na mauaji ya Isabela baada ya kulikagua gari lake. Sasa ameichukua bunduki ya mlinzi wao na kukimbilia ndani kwa kasi. Je, atafanya nini? Ni kweli ana dhamira ya kumtawanya Maganga? Kesho nayo siku!. Tunawatakia siku njema___
Posted on: Thu, 24 Oct 2013 02:05:23 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015