Rebecca (50) Ilipoishia jana... Alipohakikisha hakuna kitu - TopicsExpress



          

Rebecca (50) Ilipoishia jana... Alipohakikisha hakuna kitu kingine, aliupachika ule mkoba begani pake na kutembea kwa tahadhari hadi kwenye kibanda cha mlinzi. Akamkuta amesinzi kidogo huku silaha yake ameipakata. Akamsogelea kwa hadhari na kuichukua bunduki. Akarudi nyuma kwa mwendo kama aliokuja nao. Alipokiacha kibanda cha mlinzi kama mita kadha aligeuka na kukimbilia ndani kwa kasi. Endelea... Alipoingia wote waliokuwa pale sebuleni walishtuka kumuona ameshikilia mtutu wa bunduki akiuelekeza moja kwa moja kwa James. Alikuwa kama mtu aliyepotelewa na akili. Hakujua alilolifanya wala kusema. “Wewe muuaji umefuata nini humu ndani kwetu?” Mtutu wa bunduki ulikuwa umemuelekea James aliyepigwa na butwaa. Kwa kauli hii kila mtu akamwangalia James hasa mama yake. James hakujibu. “Nakuuliza wewe, mwanaharamu, umefuata nini hapa ndani? Nijibu upesi kabla sijakufanya kama ulivyowafanya Isabela na Mary muda mfupi uliopita.” Kauli hii ikamchanganya James. Akahisi mwili unamlegea na kuuma midomo. Uso wake ukaonesha wazi hofu na taharuki aliyokuwa nayo. Jasho likaanza kumtoka. Mzee Kimaro hakuelewa kinachoendelea, hivyo akapaza sauti. “We Rebecca unafanya nini wewe hebu toa hiyo bunduki hapo rudisha kwa mlinzi.” Mlinzi akashtuka na kujipapasa hakuona bunduki, akaangalia kulia, hakuna, kushoto hakuna. Akajua ni hiyo ilisemwa anayo Rebecca. Akachomoka kasi kuelekea kule ndani. Kabla ya kuingia akajibana mlangoni na kuchungulia kwa tahadhari. Akamuona Rebecca ameishikilia bunduki barabara kama alishawahi kupitia mafunzo ya kucheza na bunduki. Alikuwa ameielekeza kwa James aliyekaa hatua kadhaa mbele yake. Rebecca alikuwa anatetemeka mwili mzima. Mlinzi akatulia pale mlangoni huku akipanga namna ya kuingia ndani kumnyang’anya bunduki. James alipoona Rebecca hakuwa na masihara na alianza kuongea mambo ambayo yalikuwa siri yake, akasimama. Rebecca akarudi nyuma. “Usithubutu kunyanyua mguu wako kunifuata. Tafadhali mwathirika wa Ukimwi unayetumia fedha zako kuusambaza kwa wanawake wasio na hatia, nitakutawanya ubongo.” Rebecca hakuwa tena yule waliyemzoea, baba yake alizidi kuchanganyikiwa asijue la kufanya, amuite mlinzi au apige simu polisi. Mama yake hakujielewa kabisa. Alikuwa anaongea lugha aliyoielewa mwenyewe. “James wewe ni muuaji. Umemuua Isabela na kumjeruhi Mary kwa risasi zilizotoka katika bastola yako hiyo kiunoni. Umesababisha kifo cha Judith kuwa karibu kwa ukimwi wako. Pamoja na hayo yote bado hukuridhika ukataka kuuleta ukimwi humu ndani kwetu huku ukipanga kumuangamiza John bila sababu. Sasa, hapa ni mawili, utulie kama ulivyo na ipigwe simu polisi wakukute hapa au liitwe tori tori libebe maiti yako. Chagua moja.” Katika maisha yake hakuwahi kudharauliwa kama anavyofanya Rebecca. Siyo na mwanamke tu, bali hata na mwanaume. Kwa hivi aliona anaumbuliwa na kisichana kidogo sana ambacho hata maziwa ya mama yake hayajakauka ulimini. Akaanza kupanga mbinu za namna ya kujinasua. “Nani ana bastola? Hii huwa natembea nayo kwa ajili ya ulinzi usiku. Sijamuua Isabela wala kumjeruhi Mary. Mimi simfahamu Judith wala John. Wamekudanganya tu, wanakaa wapi?” James akawa anajichanganya, lakini kwa makusudi ili kumzuga Rebecca na kumtaka apotee kidogo afanye mambo. “Ona unavyojichanganya. Kama huna bastola hapo ulipo na hivi ni nini katika huu mkoba?” Rebecca akasema huku anautoa mkoba begani na kumimina vilivyomo. Vikadondoka vile vitambaa, gloves, bomba la sindano na sindano yake, kile chuma ambacho mzee Kimaro alipokiona alikigundua kuwa ni kiwambo cha kuzuia sauti na ile chupa kama ya perfume. “Sema! Na hivi ni nini na kazi yake nini? Nimevikuta katika gari lako na hilo gari limeta…” Kabla hajamalizia kusema, taarifa ya habari ilikuwa inafika ukingoni ambapo mtangazaji alikuwa anasoma muhtasari wa habari zilizopewa uzito wa juu. Taarifa ya mauaji ya Isabela yaliyofanywa na watu wawili wasiojulikana ikasomwa tena kwa muhtasari kama mwanzo. Mzee Kimaro alisikiliza kwa makini. Akazisikia herufi zilizotajwa na namba iliyotajwa, aina na rangi ya gari na mavazi ya wauaji. Vitu hivi vyote alikuwa navyo James mwilini mwake na vingine vilikuwa katika mkoba ingawa vingine havikutajwa. Bastola iliyotumia kiwambo kile chini hakuiona ila kiwambo chenyewe alikiona kwa kuwa anakifahamu. Akamgeukia James ambaye alikuwa anapuna jasho kwenye maji lake la uso uliobadilika kwa kuumbuka. Akakumbuka namna alivyochelewa kwenye kikao kule kwa bwana Jumbe. Badala ya saa moja unusu, alifika saa nne kasoro, hivyo kukosa kikao kwani alikuta ndiyo wanamalizia. Na alipofika alikuwa mwenye wasi wasi na asiyejiamini huku anahema kama mbwa. Alipoulizwa sababu ya kuchelewa alidai alikuwa na mambo ya kesi anayakamilisha ili kesho jumatatu aanze nayo. Mzee Kimaro, akatamani kumrukia na amtie kabari, lakini alishindwa. Zaidi ya akili kufanya kazi, mwili wote ulikufa. Hakuwa na nguvu. Alijawa na hasira huku akijilaumu kumwamini dudu kama hili. Akawa sasa anafura kila sekunde kwa hasira na chuki kama swira tayari kumdhuru mtu. James aliyemuamini miaka mingi hata kudiriki kutaka kumpa bintiye ndiye huyu anayeonekana hapa na shutuma kibao: mauaji, kusambaza ukimwi na kubambikia watu kesi. James akaona sasa uwezekano wa yeye wa ama kutoka hai au kukwepa mikono ya sheria ni mdogo. Mambo yote yako hadharani-nje. Kama kuvuliwa nguo, tayari ameshavuliwa na kila mtu amemuona alivyo kwa ndani. Akaamua kuivua ngozi ya kondoo na kubaki na ngozi yake halisi ya chui-chui mwili mzima, nafsi, uneni na matendo. Akawa tayari kwa lolote huku mtu wa kuanza naye akiwa huyu aliyesimama mbele yake. Huyu ndiye aliyemvua nguo sokoni tena mchana kweupe huku hadhira kubwa ikishuhudia. Taratibu akaanza kumfuata Rebecca na mkono wake wa kuume akiuelekeza kiunoni mwake. Rebecca alipoona James anamsogelea, akawa anarudi nyuma huku anatetemeka ajabu. Ujasiri aliokuwa nao mwanzo ukayeyuka kama barafu juani, woga ukachukua nafsi yake. Askari pale mlangoni aliyasikia yote na vitendo vya pale sebuleni. Na wakati huu akamuona namna James alivyobadilika na kuwa na dhamira ya kufanya mauaji. Akawa anamwangalia vile anavyomfuata Rebecca na mkono wake akiulekeza kiunoni. Akajua wazi kuwa anataka kutoa bastola. Akajiweka tayari kuingia ndani. Rebecca alisogea na sasa alikuwa karibuna televisheni, wakati huo mkono wa James ulishafika kiunoni. Mlinzi alipoona vile kengelea hatari ikagonga kichwani. ******************* Itaendelea Jumatatu!. Tunawatakia Ijumaa njema___
Posted on: Fri, 25 Oct 2013 02:18:38 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015