Riwaya:MUNGU PEKEE NDIYE ATAKAYENISAMEHE Sehemu:33 Mtunzi:Nyemo - TopicsExpress



          

Riwaya:MUNGU PEKEE NDIYE ATAKAYENISAMEHE Sehemu:33 Mtunzi:Nyemo Chilongani Simu:0718 069 269 Ilipoishia jana.. Bwana Maxwell akaushika usuknai, alichokifikiria ni kwenda katika hospitali ya McMillan Medical Center ambayo haikuwa mbali na pori hilo la Juddy Stone. Songa nayo sasa.. Alan hakutaka kuendelea na safari ya kuelekea kituoni, akamwambia polisi kwamba alitakiwa kusitisha safari ya kuelekea katika kituo cha polisi na alitakiwa kuelekea katika hospitali ya McMillan Medical Center. Hakukuwa na mtu aliyebisha, alichokifanya dereva ni kutii na kuanza kuelekea katika hospitali hiyo. Alan alionekana kuwa na presha, mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa yakimfikiria mke wake pamoja na watoto wake. Aliendelea kuomba Mungu kimya kimya huku akitaka amlinde mke wake na watoto wake wasiwe wamepata tatizo lolote lile. Ukiachana na hayo, bado alikuwa akiendelea kujiuliza maswali mengi kuhusiana na uwepo wa familia yake mikononi mwa Bwana Maxwell. Kila alipokuwa akijiuliza, alikosa jibu kabisa. Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekwishafika katika eneo la hospitali hiyo ambapo moja kwa moja wakateremka na kisha kuanza kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo. Mwendo wao ulikuwa ni wa kasi sana, walionekana kutotaka kupoteza hata sekunde moja. Walipofika ndani, sehemu ya kusubiria wagonjwa, macho ya Alan yakatua kwa Bwana Maxwell na mkewe, Jocelyn, akaanza kupiga hatua kuwafuata. “Imekuwaje tena?” Alan aliuliza hata kabla ya salamu. “Mke wako na watoto wako wapo salama ndani ya vyumba husika wakipatiwa matibabu” Bwana Maxwell alimwambia Alan huku akitoa tabasamu, bado Alan alionekana kutokuelewa kitu chochote kile. “Imekuwaje mpaka familia yangu kuwa mikononi mwako?” Alan alimuuliza Bwana Maxwell. “Nadhani ni mipango ya Mungu. Ila usijali, nitakwambia kila kitu, cha msingi tusubiri mpaka turuhusiwe kuingia mara baada ya kupatiwa huduma ya kutosha” Bwana Maxwell alimwambia Alan. Alan akatulia, bado alionekana kuwa na maswali mengi, bado alikuwa akiendelea kujiuliza ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka familia yake kuwa chini ya Bwana Maxwell na wakati mke wake, Albertina alikuwa ametekwa hospitalini na kupelekwa sehemu isiyojulikana. Waliendelea kusubiri zaidi na zaidi, baada ya masaa mawili, wakaruhusiwa kuingia. Kitu cha kwanza Alan akaanza kupiga hatua kumfuata mke wake ambaye alikuwa amelala kitandani, tabasamu kubwa liliutawala uso wa Alan mara baada ya kufika mahali pale na kugundua kwamba mtu aliyelala kitandani pale alikuwa ni Albertina ambaye alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine ya hewa safi. “Upo salama mke wangu” Alan alimwambia Albertina ambaye alikuwa amefumba macho tu. Alan hakutaka kurudhika, alichokifanya ni kuwaomba madaktari wamuonyeshee sehemu walipolazwa watoto wake, moyoni alikuwa na kiu kubwa ya kuwaona watoto wake, alitaka kuiona damu yake. Madaktari wale wakampeleka katika chumba kimoja ambacho kilikuwa na watoto wengi na kisha kumpeleka mpaka katika vitanda walivyokuwa wamelala watoto wake. “Hans….!” Alan alisema katika kipindi ambacho alionyeshewa mtoto wake wa kiume ambaye hakuonekana kuwa kwenye hali mbaya hata kidogo, huduma ambayo alikuwa amepatiwa ilionekana kuwa bora, huduma ambayo iliyanusuru maisha yake. Machozi yakaanza kumlenga tena Alan na baada ya sekunde kadhaa kuanza kumtoka. Hans alionekana kuwa mtoto mzuri mwenye mchanganyiko wa rangi, kitu ambacho kilikuwa kikimtoa machozi ni pale alipokuwa akifikiria jinsi ambavyo alitaka kumpoteza mtoto huyo katika masaa machache yaliyopita. Aliporidhika kumuangalia Hans, akapelekwa katika kitanda alichokuwa amelazwa Catherine. “Catherine…!” Alan aliita. Badomachozi yalikuwa yakimtoka, alimwangalia Catherine mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kabisa. Watoto wake walikuwa salama kabisa na ni mke wake tu, Albertina ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa kufumbua macho. Alan akataka kurudishwa mpaka katika chumba alichokuwepo mke wake, katika kipindi chote hicho Bwana Maxwell, Jocelyn na polisi yule walikuwa pamoja nae. “Ni kitu gani kilitokea?” Alan alimuuliza Bwana Maxwell ambaye alianza kuelezea mwanzo mpaka mwisho, kila mmoja akaonekana kushangaa. “Mungu ni mwema!” Alan aliwaambia huku akipiga magoti chini. Siku hiyo Alan hakutaka kuondoka, muda wote alikuwa pembeni mwa kitanda alichokuwa mke wake, hakutaka kumuacha chumbani pale peke yake, alikuwa akimpenda na kumhitaji sana katika maisha yake, kuwa karibu nae alijiona kupata faraja sana. Bwana Maxwell na Jocelyn ndio walikuwa na kazi ya kuleta vyakula mahali pale, walikuwa wakifika mara kwa mara huku wakiwa na mifuko ya vyakula na kumkabidhi Alan ambaye aligoma kabisa kutoka ndani ya chumba kile mpaka pale ambapo mke wake angefumbua macho. Siku ya kwanza ikakatika, bado Albertina aliendelea kutibiwa kama kawaida. Siku ya pili ikaingia mpaka siku ya tatu ndipo ambapo Albertina aliweza kufumbua macho. Kitu cha kwanza tu kuulizia kilikuwa ni kuhusu watoto wake, madaktari wakamuondoa wasiwasi kwa kumwambia kwamba watoto wake walikuwa salama hivyo hakutakiwa kuhofia kitu chochote kile. “Pole sana mpenzi” Alan alimwambia mke wake na kisha kumbusu katika paji la uso. “Asante sana. Watoto ni wazima?” Albertina alimuuliza Alan huku akimwangalia usoni, sauti yake ilikuwa ni ya chini kabisa. “Ni wazima, wanataka kukuona mama yao” Alan alimwambia Albertina. “Ni watoto wazuri?” “Kama ulivyo wewe mama yao. Ni watoto wazuri mno, muda wote wamekuwa wakitabasamu tu, wamenifanya kuwafananisha sana na wewe ile siku ya kwanza nilipokutana nawe” Alan alimwambia Albertina. “Nani alikuwa wa kwanza kutoka?” “Bwana Maxwell aliniambia alikuwa Hans na kisha Catherine kufuata” Alan alimwambia Albertina. “Kwa hiyo wanaendelea vizuri?” “Ndio. Hawana tatizo lolote lile” Alan alimwambia Albertina. Siku hiyo ikaonekana kuwa furaha kwa Alan, muda wote alikuwa pembeni ya mke wake akimhudumia katika kumlisha. Huyo ndiye alikuwa mke wake mpandwa ambaye alimchagua kwa moyo wote na alimpenda kwa mapenzi yote moyoni mwake. Hakutaka kumuacha, aligundua kwamba Albertina hakuwa na mwanaume yeyote wa kumfariji zaidi yake yeye, hivyo alitamani kuwa nae karibu kila wakati. Albertina alikaa hospitalini kwa muda wa wiki nzima na ndipo aliporuhusiwa kurudi nyumbani. Alan akaonekana kubadilika, japokuwa zamani alikuwa na furaha lakini katika kipindi hicho alikuwa na furaha zaidi. Hakwenda kazini, alishinda nyumbani pamoja na watoto wake. Ulinzi ukaongezeka nyumbani kwake, hakutaka mtu yeyote aingie ndani ya nyumba hiyo bila ukaguzi. Wakawaweka watoto wao katika chumba maalumu, chumba ambacho kilikuwa na kila kitu ambacho mtoto alitakiwa kuwa nacho. Waliwawekea vitu vingi vya kuchezea, japokuwa walikuwa wadogo mno lakini walionekana kuwa wazuri sana. Alan akaahidi kuwapa kila kitu ambacho kilikuwa kikihitajika katika maisha yake, hakutaka mtu yeyote aingilie katika maisha yao. Alikuwa akifanya mengi kwa ajili ya watoto wake lakini akili yake ilikuwa ikimfikiria Antonio tu. Alijua fika kwamba bado Antonio alikuwa na kisasi moyoni mwake na angeweza kulipiza kisasi muda wowote ule. Hakutaka kuliona hilo likitokea na ndio maana aliuweka ulinzi mkubwa nyumbani kwake. “Nitataka Hans awe dokta mkubwa hapo baadae” Alan alimwambia Bwana Maxwell. “Kwa nini usitake awe polisi kama nilivyokuwa?” Bwana Maxwell aliuliza huku akionekana kutania. “Hapana. Sitotaka awe polisi, ningependa awe daktari tu” Alan alimwambia Bwana Maxwell huku akicheka. “Au hautaki ashike bunduki?” “Nadhani hiyo ni sababu mojawapo” “Bila bunduki unafikiri mambo mengine yatasonga? Kama nisingekuwa mtu wa kushika bunduki kweli ungekuwa hai sasa hivi?” Bwana Maxwell alimuuliza Alan. “Sidhani, ila sitaki mtoto wangu awe muuaji> Nitafanya kila linalowezekana, sitaki mtoto wangu aje kuua kama nilivyoua” Alan alimwambia Bwana Maxwell. “Hakuna tatizo. Ni malezi yako mazuri ndio yatakayoweza kumfanya mtoto kuwa kama wewe utakavyo. Na vipi kuhusu Catherine?” Bwana Maxwell alimuuliza Alan. “Nadhani huyu anatakiwa kuwa mwanasheria wa serikali” Alan alimwambia Bwana Maxwell. “Basi hakuna tatizo. Bado malezi yako bora kama baba yanahitajika” Bwana Maxwell alimwambia Alan. ***** Mawasiliano kati ya Brian na Stacie yalikuwa yakiendelea kama kawaida, tayari walikuwa na mahusiano ya kimapenzi, walionyesheana mioyo ya kupendana sana kiasi ambacho hata wao wenyewe walionekana kujishangaa. Mara kwa mara Stacie alikuwa mtu wa kusafiri na kuelekea nchini Tanzania, hakutaka kukaa sana nchini Marekani kwa kuwa mpenzi wake alikuwa nchini Tanzania na alitaka sana kuwa karibu yake zaidi. Kila mmoja alionekana kuridhika moyoni mwake, walikuwa wakipendana kwa mapenzi ya dhati, walikuwa wakisikilizana na kujaliana. Nchini Tanzania, huko ndipo ambapo wakavarishana pete na kuwa wachumba. Bado mahusiano yao yaliendelea kukua kwa kasi sana. Ukaribu wao ukawafanya kuwa miongoni mwa wapenzi ambao hawakuwa na dalili za kuachana hata siku moja. Kama kulikuwa na tofauti ambazo zilikuwa zikitokea, waliwekana chini kama wapenzi na kisha kuelezana, kilichofuatia ni kupeana mabusu motomoto kwa kuonyesha kwamba kila kitu kilikuwa safi. Mahusiano yao yaliendela hivyo hivyo mpaka katika kipindi ambacho wakaamua kufunga ndoa. Hilo halikuonekana kuwa tatizo, wakafunga ndoa ndani ya kanisa la Praise And Worship lililokuwa nchini Tanzania na kisha sherehe kubwa kufanyikia nchini Marekani na kuendelea na maisha huko. Waliishi maisha ya ndoa kwa kuheshimiana sana, walikuwa wakiskilizana sana mpaka pale ambapo Brian akaanzisha biashara mbalimbali, biashara ambazo ziliwafanya kuingiza kipato kikubwa cha fedha ukiachana na utajiri aliokuwa nao wazazi wake na Stacie. Ndani ya miezi miwili ya ndoa yao, Stacie akapata ujauzito na baada ya miezi tisa kupata mtoto wa kike ambaye walimpa jina la Elizabeth. Elizabeth akaonekana kuwa furaha kwao, walimlea Elizabeth katika malezi bora huku wakijitahidi kumpa kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji. Watoto wote wa mzee Ruttaba, Brian na Albertina walikuwa wakiishi nchini Marekani. Hilo wala halikuonekana kuwa tatizo, kila walipotaka kwenda nchini Marekani, walikuwa wakielekea huko na kuonana na watoto wao. Waliwapenda na kuwathamini, wao walionekana kuwa furaha kuu katika maisha yao. Walipokuwa wakimuona Elizabeth, walimbeba na kufurahi pamoja nae, walipokuwa wakimuona Catherine pia walikuwa wakimbeba na kufurahi pamoja nae na hata walipokuwa wakimuona Hans hali ilikuwa hivyo hivyo. Sura ya Hans toka utotoni ikaanza kuonekana kuwa sura ya kipole kupita kawaida. Hakuonekana kama mtu ambaye angekuwa na vurugu au ugomvi katika maisha yake ya baadae. Sura yake ya upole ambayo ilikuwa imefanana na Catherine ilionekana kuwa tofauti na mambo ambayo angeyafanya katika maisha yake ya baadae. Ile ilionekana sura ya upole lakini moyo wake haukuonekana kuwa na upole hata kidogo, endapo ungemkasirisha na kuuharibu moyo wake, angefanya chochote kile kukuua, haijalishi kama angeyapa gharama maisha yake, alichokuwa akikitaka ni kukuua tu. Hilo wala halikuonekana mbele ya macho ya wazazi wake, babu wala bibi, hicho kilikuwa ni kitu kilichokuwa moyoni, kitu ambacho kilikuwa tofauti na sura yake ya upole mara anapokasirishwa na mtu yeyote yule. Je nini kitaendelea? Je ni mambo gani atayafanya Hans huko mbeleni? Je atayafanya peke yake au kutakuwa na mtu mwingine pia? Je kisasi cha Antonio kitaishia wapi? Itaendelea. Uchache wa LIKE unafanya hadithi kuandikwa kwa kurasa mbili na nusu na wingi wa LIKE unafanya hadithi kuandikwa kwa kurasa nne, kazi ni kwako kuchagua. Ukitaka ndefu, LIKE, ukitaka fupi, POTEZEA.
Posted on: Fri, 01 Nov 2013 05:27:45 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015