Riwaya:MUNGU PEKEE NDIYE ATAKAYENISAMEHE Sehemu: YA MWISHO KWA - TopicsExpress



          

Riwaya:MUNGU PEKEE NDIYE ATAKAYENISAMEHE Sehemu: YA MWISHO KWA FACEBOOK Mtunzi:Nyemo Chilongani Simu:0718 069 269 Ilipoishia jana.. “Hakuna tatizo. Mimi nataka kuwa dokta wa magonjwa ya wanawake tu inatosha” Juliet alimwambia Hans. “Utafanikiwa sana, nakuamini mpenzi, utafanikiwa sana” Hans alimwambia Juliet. “Asante kwa kunitia moyo” Juliet alimwambia Hans. Songa nayo sasa.. Siku ziliendelea kwenda mbele huku mapenzi yao yakizidi kuongezeka, kila mmoja aliendelea kumjali na kumsikiliza mwenzake, mapenzi yao ndani ya mioyo yao yalikuwa makubwa kiasi ambacho kiliwashangaza hata wao wenyewe. Shule iliendelea zaidi huku Hans akiendelea kujiita Dokta. Kila wakati alikuwa akivaa koti refu jeupe pamoja na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo ikiwa shingoni mwake. Baada ya miaka mingine miwili, wakamaliza kabisa elimu ya sekondari na kisha kuingia chuo. Kutokana na mapenzi makubwa ambayo walikuwa nayo hawakutaka kuwa mbali mbali, walichokifanya ni wote kuchagua kujiunga na chuo cha kulipia cha St; Corneus University ambacho kilikuwa pembezoni mwa jiji la Washington. Ukaribu wao ukazidi kushamiri huku wote wawili wakitumia muda mwingi kusoma pamoja na kufanya mambo mengine maishani mwao. Japokuwa maisha yalikuwa yakiendelea lakini Bwana Alan na Bi Albbertina hawakutaka kuwaambia watoto wao juu ya kile kilichokuwa kimetokea katika miaka ya nyuma, hawakutaka kuwaambia juu ya uadui mkubwa ambao walikuwa nao na Mmexico, Antonio. Bwana Alan alihakikisha watoto wake wanapata ulinzi wa siri katika kila sehemu watakazokwenda, hakutaka kuwapoteza wala kusikia kwamba watoto wake walikuwa wametekwa na kuanza kuingia gharama. Bwana Alan aliposikia kwamba mtoto wake, Alan alikuwa katika uhusiano na msichana Juliet, hakutaka kuchelewa, akawaagiza watu wake kuanza kumchunguza huyu Juliet alikuwa na nani na alikuwa mtoto wa nani. Hakutaka kumwamini mtu yeyote katika maisha ya watoto wake, alikwishawahi kuwa rafiki mkubwa wa Antonio lakini nyuma ya pazia Antonio alikuwa mtu mwingine kabisa ambaye alileta matatizo makubwa katika familia yake. Bwana Alan akaanza kusubiri majibu juu ya Juliet na majibu yalipokuwa tayari akapewa kwa kuambiwa kwamba Juliet alikuwa mtoto wa tajiri Mike, tajiri ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya kutengenezea karatasi nchini Marekani. Bwana Alana akaonekana kuwa huru, hapo hakukuwa na tatizo kabisa kwa kuamini kwamba mtoto wake, Hans angekuwa salama na si kama alivyokuwa akifikiria. Katika kipindi ambacho Hans na Catherine wanafikisha miaka kumi na nane ndio kipindi ambacho Hans akachaguliwa na kuwa Dokta katika hospitali ya Mississippi Medical Center iliyokuwepo hapo Mississippi. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, alikuwa amesoma kwa kipindi kirefu sana na alitegemea kwamba kuna siku angekuja kuwa dokta na katika kipindi hicho ndoto yake ikaonekana kukamilika japokuwa bado alikuwa akihitajika kusoma zaidi na zaidi kwa ajili ya kuwa bora zaidi ya alivyokuwa katika kipindi hicho. Hilo halikuwa tatizo kwa Hans, bado alikuwa akiendelea kusoma na kufanya kazi kama kawaida. Aliwahudumia wagonjwa kwa kuwapa huduma bora ambazo walivutiwa nae kila siku. Kutokana na ucheshi wake, Hans akajikuta akitengeneza urafiki na madaktari wenzake pamoja na wagonjwa ambao walikuwa wakifika mahali pale. Hakuwa amefikia uwezo wa kutengeneza dawa za kuua sumu ndani ya miili ya binadamu lakini kila siku alikuwa akielekea maabara kwa ajili ya kuifanyia kazi dawa hiyo. Ilimchukua Hans miaka miwili, hapo ndipo alipofanikisha kutengeneza dawa aliyoipa jina la HAAC4, dawa ambayo ilikuwa inaherufi za mwanzo za majina yote ya watu wa katika familia yao yaani Hans, Alan, Albertina, Catherine huku namba 4 ikiwakilisha idadi ya watu hao. Dawa ikapelekwa katika sehemu za vipimo. Madaktari mabingwa wakakutana na kisha kuanza kuiangalia dawa hiyo. Dawa ilionekana kuwa yenye ubora na kila walipokuwa wameitumia kama jaribio kwa wagonjwa ilionekana kufanya kazi sana kwa kuua sumu mwilini mwa mwanadamu. Hiyo ikaonekana kuwa sifa kwake, jina lake likazidi kuvuma zaidi na zaidi. Kulikuwa na madaktari wakubwa ambao walikuwa na masters zao lakini hakukuwa na madaktari hao ambaye alikuwa ametengeneza dawa yoyote ile. Kitendo cha Hans kutengeneza dawa kilionekana kuwa cha tofauti sana, alionekana kuwa na kitu cha ziada kichwani mwake. Dawa ile ikaanza kutangazwa na kisha kuingizwa sokoni. Dunia ikaonekana kupata ahueni, watu wengi walikuwa wameathiriwa na sumu miilini mwao, dawa ile ikaonekana kuwa mkombozi. Serikali ya Marekani ikaingia mkataba na Hans kwa kumlipa zaidi ya dola milioni mia moja na thelathini kila mwaka kwa ajili ya kuisambaza dawa hiyo duniani kote. Hans hakuonekana kuwa na tatzio, japokuwa fedha hazikuwa za kutosha lakini akaamua kuruhusu kwa sababu alitaka watu wengi wapate tiba juu ya sumu ambazo walikuwa nazo miilini mwao. Hans hakumsahau Juliet, bado alikuwa akiendelea kuwa nae kila siku. Katika kipindi hicho Juliet alikuwa Dokta kama alivyotaka kuwa, Dokta ambaye alikuwa akishughulika na magonjwa ya wanawake tu. Ukaribu wao ukaongezeka mara baada ya Juliet kuomba uhamisho wa kuhamishiwa katika hospitali ya Mississippi Medical Center, hakukataliwa, akaruhusiwa kwenda kufanya kazi katika hospitali hiyo. “Nimekukumbuka sana mpenzi” Hans alimwambia Juliet. “Hata mimi kipenzi” “Umekumbuka nini kutoka kwangu?” Hans alimuuliza Juliet. “Kila kitu” “Kama kipi?” “Tabasamu, kicheko, meno yako meupe, macho yako mazuri, yaani kila kitu” Juliet alimwambia Hans. Wawili hao waliendelea kuwa karibu zaidi na zaidi. Mioyo yao bado ilikuwa na mapenzi mazito, walipendana na kujaliana kila siku katika maisha yao. Hawakuwa na muda wa kugombana, mara kwa mara walikuwa wakiyafurahia maisha yao ya mahusiano ya kimapenzi. “Nataka nikuoe. Upo tayari?” Hans alimuuliza Juliet. “Kwa nini nisiwe tayari mpenzi” Juliet alimuuliza Hans. “Inawezekana usiwe tayari” “Nipo tayari. Unataka tuoane lini?” “Kuna mkutano wa matajiri utafanyika kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini duniani, nadhani baada ya hapo, tutaoana” Hans alimwambia Juliet. “Sasa harusi yetu inahusika vipi na huo mkutano?” Juliet alimuuliza Hans. “Baba amehitaji niwe pamoja nae” “Wapi?” “Kwenye mkutano huo” Hans alimjibu Juliet. “Basi sawa. Utaanza lini?” “Miezi sita ijayo” “Hakuna tatizo” KIla mmoja akaonekana kuwa na presha, wote kwa pamoja walikuwa wakitamani sana kuingia katika maisha ya ndoa. Ndoa baada ya miezi sita kilionekana kuwa kipindi kirefu sana lakini hawakuwa na jinsi, walitakiwa kusubiria mpaka pale ambapo mkutano huo ungefanyika na kisha kumalizika. Hapo ndipo miezi ikaanza kukatika, ukaanza mwezi wa kwanza mpaka ulipotimia mwezi wa sita. Katika kipindi hicho Bwana Alan hakuonekana kuwa na raha hata kidogo. Alikuwa tofauti na kipindi cha nyuma hali ambayo ilionekana kumjaza maswali mengi Hans lakini hakuwa na cha kuuliza zaidi ya kubaki kimya huku akijitahidi kupeleleza ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwa baba yake. “Antonio nae atakuwepo” Bwana Alan alimwambie mke wake, Albertina. “Kwenye huo mkutano?” “Ndio” “Mungu wangu!” “Yaani nimeshtuka sana, sijui nitakaa vipi na mbaya wangu meza moja” Bwana Alan alimwambia mke wake. “Haina jinsi. Kuna mwingine?” “Watakuwepo matajiri kutoka sehemu mbalimbali duniani pamoja na katibu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Powell” Bwana Alan alimjibu mke wake, Albertina. “Usijali mume wangu, nadhani Antonio atakuwa amesahau kila kitu” “Sina uhakika juu ya hilo. Ngoja tusikilizie” Bwana Alan alimwambia mke wake, Albertina. ***** Nchi masikini zilizidi kuongezeka duniani, uchumi ulikuwa umeyumba sana kiasi ambacho Umoja wa Mataifa ukaonekana kushangaa. Vyakula havikuwa vikipatikana vya kutosha hasa katika nchi zilizokuwa katika bara la Afrika kitu ambacho kilionekana kuleta maafa ya njaa. Maswali mengi yakaanza kumiminika vichwani mwa watu wengi kwamba ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Msaada ulikuwa ukihitajika sana, kilichofanyika, mwenyekiti wa Umoja wa Mataifa, Bwana Powell akaandaa mkutano jijini Washington, mkutano ambao ungehudhuriwa na matajiri kutoka katika bara la Afrika, Marekani kusini na kaskazini, Ulaya na Asia huku bara la Ulaya wakipewa nafasi ya kuhudhuria matajiri wawili tofauti na mabara mengine. Bwana powelndiye ambaye alikuwa msimamizi wa mkutano huo, yeye ndiye ambaye alikuwa amewaita matajiri hao kwa ajili kuhudhuria mkutano huo ambao ulikuwa ukisikiliziwa na mataifa mengi duniani ili kujua ni kitu gani ambacho kilikuwabaliwa kufanywa kama njia mojawapo ya kutokomeza njaa. Bill Gates alitakiwa kuwepo kwenye mkutano huo ila kwa sababu alionekana kuwa bize barani Afrika katika kutembelea vituo mbalimbali vya watoto yatima, nafasi yake ikachukuliwa na Bwana Alan ambaye alihakikisha kuiwakilisha vyema Marekani. “Jiandae, kesho ndio siku ya kwanza ya mkutano” Bwana Alan alimwambia Hans. “Hakuna tatizo, nimekwishajiandaa vya kutosha” Hans alimwambia baba yake. Kesho ilipofika, wote wakaanza kuondoka kuelekea katika hoteli ya kimataifa ya MGM Grand iliyokuwa Las Vegas na kisha kuanza kuhudhuria mkutano huo. Muda wote Bwana Antonio hakuwa akimwangalia kwa macho mazuri Bwana Alan, kwa mtazamo ambao alikuwa akimuonyeshea, alionekana kuwa na kitu moyoni mwake, alionekana bado kuwa na kila sababu za kumuua Bwana Alan, ikiwezekana hata Hans pia. Huo ndio ulikuwa mkutano ambao ulimfanya Hans kuizunguka dunia kwa ajili ya kuwaua matajiri hao, mauaji ambayo yalimfanya kuwa mtu anayehitajika zaidi duniani kuliko mtu yeyote yule. Kwa kutumia sindano iliyokuwa na sumu, alikuwa akiwateketeza matajiri wote, sababu kubwa, ilikuwa ni njia mojawapo ya kulipiza kisasi kwa kile kilichokuwa kimetokea. SHUKRANI. Huu ndio utakuwa mwisho wa kuiendeleza hadithi hii mahali hapa, hii ndio imekuwa hadithi yangu ya mwisho kuiandika katika mtandao wa facebook. Katika kipindi kirefu nilihitaji kuandika hadithi magazetini, tena yasiwe magazeti yoyote bali nilijiwekea kufanya kazi chini ya kampuni ya Shigongo ya Global Publisher kwani nilitamani kuwa karibu na mtu huyo kwa sababu yeye ndiye amenifanya niandike hadithi namna hii, yeye ndiye Role Model wangu ambaye nafuata hatua zake za uandishi.Nilichokihitaji, kimekamilika na hatimae nimeanza kufanya kazi katika kampuni hiyo. Kwa sasa nahitaji kuwa mwandishi nisiyekuwa na mambo mengi, kwa sababu nimesomea uandishi, nimekuwa mwandishi ndani ya kampuni hiyo. SItokuwa na muda wa kuandika hadithi facebook, nitakuwa bize kuandika habari mbalimbali na hata hadithi katika magazeti hayo. Hadithi zangu za Kahaba kutoka China na Hili ni Jiji la New York zitaanza katika magazeti ya kampuni hiyo hivi karibuni, wewe kama mdau wangu namba moja natumaini utakuwa nami mpaka huko pia. Ninamshukuru sana Andrew Carlos, amekuwa msaada mkubwa sana kwangu kwa kuniruhusu kuandika hadithi mahali hapa. Nilihitaji watu wengi wanifahamu, na kweli wengi wamenifahamu. Hakuwa na roho ya ubinafsi, akaniachia uwanja na mimi kufanya yangu. Ninamshukuru sana kwani amejitoa kwa mengi kwa ajili yangu na kila siku ataendelea kuwa rafiki yangu wa karibu sana hasa kwa waandishi wa Facebook. Pia ningependa kukushukuru wewe msomaji. Umekuwa mstari wa mbele kunipa LIKE yako ambayo huonyesha ni jinsi gani watu wanafuatilia, mlipokuwa hampaelewi mliniomba niwaelekeze na hata kwenye makosa mlinisahihisha, nawashukuru sana kwa hilo. Sisi ni binadamu ambao tunaishi ndani ya ndoto, kila mmoja ana ndoto yake, mimi kama mimi nilikuwa na ndoto ya kufanya kazi karibu na Role Model wangu, SHigongo na hatimae ndoto yangu imekamilika baada ya miaka tisa kupita. Leo, nakaa jengo moja na yeye, nitakapotaka ushauri ananishauri ninapotaka maelekezo juu ya nini cha kufanya ananielekeza. Nyemo The Prince, ni moja ya jina linalojulikana sana Facebook ila ningependa mjue kwamba nilijipa The Prince kwa sababu nilimpa Shigongo heshima ya kuwa The King na mimi kuwa mtoto wake kwenye uandishi wa hadithi, na itaendelea kubaki hivyo siku zote. Kwa sasa nahitaji kusonga mbele zaidi, nahitaji kuyatafuta mafaniko zaidi. Natumaini Andrew Carlos atakuwa pamoja nanyi, ataendelea kuwaburudisha kama kawaida. SIkutaka kuiandika sehemu hii ila Andrew alinitaka niiandike na niwaambie fans wa uwanja huu inachoendelea. Kwa kumalizia, ningependa niwaachie hadithi zangu mbili ambazo kwa atakayetaka ataweza kuuziwa, moja ni Sms Chatting, najua waliosoma Facebook Chatting watakuwa wanaelewa ni aina gani ya uandishi unaotumika. Hiyo nimeiandika yote na mtaweza kuinunua online, yaani kupitia inbox au email. Nyingine ni SCAMMER (Tapeli wa Mtandaoni). Kwa wasioijua ni kwamba nimejiandika mimi kama mpelelezi ambaye nilitumiwa meseji facebook kwamba msichana amenipenda kwa kupitia profile langu na sasa anataka niwasiliane nae kwenye email. Ni hadithi nzuri sana ambayo hautakiwi kuikosa, nimecheza kama mpelelezi ambaye nilisafiri kutoka Uingereza kuja Tanzania na kuelekea Nigeria kumtafuta tapeli huyo kwa lengo moja la kumuua tu. Hautakiwi kuikosa, gharama yake utaambiwa. Naomba sana muendelee kuwaambia watu kuhusu ukurasa huu, ni ukurasa pekee wa hadithi wenye fans wengi na pia tunataka watu wengi waje huku kwani kupitia ukurasa huu Shigongo alipewa taarifa kwamba kuna mtu anaandika hadithi kama yeye na mwisho wa siku kukutana nae, nadhani mlikwishaiona picha iliyowekwa ambayo nilipiga nae siku za nyuma. SINA CHA KUSEMA ILA NINASHUKURU SANA KWA KAMPANI YENU. HADITHI HII ITAPATIKANA MWANZO MPAKA MWISHO GAZETINI SIKU ZA USONI, HAUTAKIWI KUIKOSA KWANI NI HADITHI AMBAYO ITAKULIZA SANA HASA MARA BAADA YA KUGUNDUA SABABU ILIYOMFANYA HANS KUWAUA MATAJIRI KAMA KISASI, JE NI KISASI JUU YA NANI? UTALIPATA JIBU GAZETI. ASANTENI SANA, NAOMBA TUWE WOTE MPAKA GAZETINI. MUNGU AWABARIKI. NYEMO THE PRINCE.
Posted on: Sun, 03 Nov 2013 07:37:12 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015