SEHEMU YA TATU MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA - TopicsExpress



          

SEHEMU YA TATU MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI 200.-(1) Kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye atateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma. (2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Serikali atashika wadhifa huo mara tu baada ya kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano. 201. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atateuliwa kutoka miongoni mwa watumishi wa umma wenye sifa zifuatazo: (a) aweamefuzu mafunzo ya juu ya uhasibu na kusajiliwa na mamlaka husika; (b) ana uzoefu usiyopungua miaka kumi na tano katika utumishi wa umma; (c) ana uzoefu usiyopungua miaka kumi na tano katika masuala yanayohusu ukaguzi wa hesabu za Serikali; na (d) ni mtu mwenye heshima, weledi, uaminifu, uadilifu na asiye na upendeleo unaotiliwa shaka na jamii. 202.-(1) Kazi na majukumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yatakuwa ni: (a) kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe; (b) kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge, na kwambazimetumika kwa ajili ya shughuli zilizohusika na matumizi ya fedha hizo na matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo; (c) angalau, mara moja kila mwaka, kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za Mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge; na (d) kutayarisha ripoti ya mwaka na kuiwasilisha Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa mapendekezo. (2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atakuwa huru katika utekelezaji wa kazi na majukumu yake, na kwa mantiki hiyo, hataingiliwa na mtu au mamlaka yoyote katika utekelezaji wa kazi zake. (3) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kila mtumishi wa Serikali aliyeruhusiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atakuwa na haki ya kuchunguza vitabu, kumbukumbu, hati nyinginezo zote zinazohusika na hesabu za aina yoyote iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya Ibara hii. (4) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii. (5) Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile ulipoanza Mkutano huo, na iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge, basi Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali atawasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge au kwa Naibu Spika iwapo nafasi ya madaraka ya Spika iko wazi,ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwa Bunge. (6) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atakuwa pia na jukumu la kutekeleza kazi na shughuli nyingine, na atakuwa na madaraka mengine ya namna mbalimbali, kama itakavyoelezwa na sheria kuhusu hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au hesabu za vyombo vya umma au hesabu za mashirika. (7) Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (1), (3), (4) na (5) ya Ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali,lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo. (8) Bunge linaweza kutunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, matumizi ya mamlaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. 203.-(1) Muda wa kukaa madarakani kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali itakuwa ni kipindi kimoja cha miaka saba mfululizo. (2) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaweza kujiuzulu wadhifa wake kwa kutoa taarifa ya siku thelathini kwa Rais...
Posted on: Thu, 29 Aug 2013 09:39:18 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015