SIMULIZI: JERAHA LA HISIA. MTUNZI: George Iron - TopicsExpress



          

SIMULIZI: JERAHA LA HISIA. MTUNZI: George Iron Mosenya. SEHEMU YA TANO. "Ulale pema peponi Maureen, msalimie bibi mwambie mchumba wangu Naomi sijui alipo, wasalimie baba na mama waambie nawapenda sana, kwaheri dada Maureen"Aliongea hayo Walter wakati anauaga mwili wa Maureen uliokuwa umepondekapondeka vibaya kutokana na majanga aliyoyapata, kwanza umeme halafu ajali mbaya ya gari. Maneno na sauti yake vilimchoma kila mtu aliyeyasikia,Walter alikuwa na jeraha kisogoni, nguo zake zilikuwa chafu sana. Hakuhitaji kubadilisha na hakuwepo wa kuweza kumshawishi lolote. "Nilitegemea kula nawe sikukuu za mwisho wa mwaka kwa nini hukusubiri lakini! Mbona hukutaka walau nipate dakika mbili za kukuona ukitabasamu. Ewe ardhi mwenye tamaa nimeze na mimi uridhike, hivi baba na mama hawakukutosha? Bibi naye je…haya na dadangu umemchukua….eeh Ardhi nimeze sasa hivi niondoke na Maureen" alishindwa kujizuia Walter akaangua kilio kikali, wakati huo Frank alikuwa hajiwezi ameishiwa nguvu akiwa amekaa chini, ulikuwa msiba ulioteka hisia za wengi sana katika mitaa mbalimbali jijini Dar-es salaam. Kilio cha mtu mzima kikachukua nafasi. **** Baada ya ardhi kugoma katakata kukisikia kilio cha Walter na badala yake kuyameza machozi yake bila shukrani hatimaye Walter akajikuta akiilaani ardhi ya Tanzania. Aliilaani kwa kuwa ilikuwa imempa uchungu ambao ulikuwa mgumu sana kufutika. “Huenda hata Naomi naye ilimmeza ardhi hii isiyokuwa na shukrani.” Walter alisema na nafsi yake wakati akimalizia kuilaani kwa lugha zote ardhi ya Tanzania. “Frank.” Walter aliita kisa akendelea, “Anko Muga.” Wote wakawa makini kumsikiliza. “Naapa mbele yenu, ndugu zangu mliosalia. Sitakaa niikanyage ardhi hii tena. Frank, usijisikie vibaya na kuhisi kuwa nakukimbia; hapana umekuwa msaada mkubwa sana kwangu, wewe ni baba mwema sana kwangu. Lakini haikupangwa tu nifurahi pamoja nawe. Labda sikustahili kuzaliwa katika nchi hii, n’do maana inanitenda hivi.” Walter alimaliza kuzungumza alichakuwa amepanga. Frank na Muga, wakabaki kimya, hakuna aliyejazia neno la ziada. Waliamini kuwa maneno yao hayawezi kumbadili Walter na msimamo wake. Baada ya siku mbili Walter akiambatana na Muga, wakaiacha ardhi ya Tanzania. Safari hii waliondoka kwa usafiri wa ndege. Lile gari jipya walilolitumia kwa safari ya Mwanzo, Walter akamtunuku Frank kama zawadi kwa moyo wake wa upendo. Maisha mapya yakaanza tena. **** BAADA YA MIAKA MIAKA MIWILI. Maandalizi ya tamasha kubwa la Muziki nchini Tanzania yalikuwa yamepamba moto, tamasha hili kwa mara ya kwanza liliwagusa hadi wafuatiliaji wengine katika nchi za jirani. Liliwagusa watu wengi kwa sababu moja tu, wasanii mapacha kutoka nchini Nigeria walikuwa wamekubali siku ya kilele cha tamasha lile. Walter aliipokea taarifa hii kupitia vyombo vya habari. Akakuna kichwa chake, akachangamka kuisikia habari hii. Akaikumbuka ndoto yake tangu anaanza kuwika katika shughuli za u-Dj. Ndoto ya kufanya kazi na wasanii wale. Lakini alipokumbuka kuwa wanaifanya kazi yao katika ardhi aliyoilaani nayo ikamlaani, munkari wake ulishuka sana. Na hamu ikamwisha. Kitu bora hutengenezwa na watu bora. Waandaaji wa tamasha lile walihitaji kufanya kitu bora sana katika kilele cha tamasha hilo. Hivyo katika sekta zote za muhimu walihakikisha zinashikiliwa na watu wa maana. “Hebu mpigie simu namba yake hii hapa.” Mshika dau mmoja alitoa wazo baada ya kuwa wamejadili kwa muda mrefu. Simu ikapigwa na wote wakaunda kimya kikubwa ikabaki kusikika simu pekee. “Hallo…” ilijibu sauti upande wa pili. “Unaongea na timu ya Chizika..bila shaka ni Dj Muga.” “Bila shaka.” Alijibu kwa utulivu. Upande wa pili ukazungumza lengo la kupiga simu. Walikuwa wakimuhitaji Dj ambaye alikuwa anafanya kazi akisimamiwa na Muga kama mkurugenzi wake. “Nitawapatia jibu baadaye.” Alijibu Muga baada ya kuwa amekosa jibu la moja kwa moja. **** MABISHANO yalikuwa makali sana, Walter hakutaka kujadili suala la yeye kurejea Tanzania. Muga alimsisitiza na kumtajia dau kubwa ambalo limetajwa kwa ajili yake. Dau halikumshtua Walter. Tayari alikuwa majeruhi, jeraha la hisia za ardhi ya Tanzania kuwa inamuonea zilimgalagaza na kumfanya ajione yu mtumwa utumwani. “Walter.” Muga alimuita kwa utulivu baada ya damkika kadhaa za kutupiana maneno japo si kwa ubaya. Walter akatikisa kichwa kuashiria amesikia. “Baba, mama, bibi, dada….wako wapi?” “Mbinguni.” Alijibu Walter. “Umewahi kufika huko ukawaona.” “Najua wapo mbinguni. Nilifundishwa hivyo tangu utotoni.” “Ok. Hivi unajua kuwa wanakuona unachofanya duniani.” “Ndio wananiona, hata hilo nilifundishwa pia.” Alijibu Walter upesi bila kuijua nia ya Muga. “Vyema kama unatambua kuwa wanakuona. Na watu wote hao uliowaheshimu wakati wapo hai umeshindwa hata kuheshimu makaburi yao, umeshindwa kuheshimu makazi yao ya sasa, umewakimbia. Walter watu hawa wa muhimu kwetu wanakutazama na wanalia juu yako. Kila mara ni mimi na Frank tunaenda kufanya usafi katika makaburi. Wewe umegoma, umegoma kuzisafisha nyumba zao.” Muga akaweka kituo kisha akaendelea, “Mimi sikulaumu wewe hata kidogo, ila naomba uamini kila kitu huja na hupita hata hayo yalitokea na yamepita. Kama unailaani ardhi ya Tanzania. Je watu wa Rwanda waliopoteza ukoo mzima wafanye nini?” alimaliza Muga. Kimya kikatanda, Walter alikuwa anatetemeka. Akajihisi mkosefu. Maneno ya Muga yalikuwa yamemvuruga kwa kiasi kikubwa. Na kwa upande mkubwa sana yalikuwa yana ukweli ndani yake. Muga alipomaliza akaaga ili aweze kuondoka maana alikuwa nyumbani kwa Walter wakati ule. “Anko….hebu subiri kidogo..” Walter akamzuia. Muga akabaki amesimama akimsikiliza Walter. Walter akatazama juu, kisha akashusha kichwa chake chini. “Kwa heshima yako, Frank na roho nilizozipenda lakini zikaitamanisha ardhi yenye tamaa ikazimeza. Nitarejea Tanzania. Kwa moyo mmoja mweupe kabisa nitarejea katika ardhi niliyoichukia, kama bado ina kinyongo nami kwa kosa nisilolijua basi na inimeze, kama haina kinyongo nami na inihifadhi kwa upendo isiniumize tena siku hizi za karibuni. Ni heri inimeze mimi kuliko kuimeza roho yoyote ninayoifahamu. Nina jeraha kubwa sana ambalo halina dalili ya kupona. Sihitaji kujitonesha upya.” Walter alimaliza kuzungumza. Muga akamsogelea na kumpigapiga mgongoni ishara ya kumpooza. Akazua kilio kingine. Walter hakuweza kustahimili kumbukumbu ngumu za kipindi cha nyuma. Ikabaki kazi ya Muga kumbembeleza. **** UKUMBI mkubwa na wa kisasa wa Diamond Jubilee ulikuwa umefurika watu wa haiba mbalimbali. Burudani ilikuwa haijachangamka bado. Hadi pale alipotangazwa Dj atakayekuwa katika mtambo. Nani ambaye hakumfahamu Walter. Ni mara ngapi aliitwa kuja kufanya shughuli Tanzania akawagomea wadau. Akatangazwa kuwa ana dharau sana. Sasa leo yupo nchini Tanzania. Baada ya kutambulishwa kila mtu alipiga kelele za aina yake, wapo waliomzomea kwa sauti za juu, na hawa n’do walikuwa wengi, wachache walipiga miluzi ya kumshangilia. Walter aliligundua hilo, akakichukua kipaza na kusimama mbele ya mashabiki baada ya Mshereheshaji kumruhusu. Walter akazungumza maneno ambayo yaliunyamazisha ukumbi huo mkubwa wa Diamond. Wengine aliwaliza, wengine walipiga moyo konde, na wengine waliopitia magumu zaidi yake walipuuzia. Shuguli ikaanza rasmi. Hakika Walter alikuwa habari nyingine. Alipangilia mambo kimataifa. Majira ya saa sita usiku ndipo alipoanza kuzorota. Ni baada ya kushuhudia jambo la ajabu linalofanana na ndoto. Jukwaa lilikuwa limekabwa na wacheza viduku, ilikuwa zamu yao kuburudisha watazamaji. Walter akaona umbo ambalo aliwahi kuliona tena hapo kabla. Alitamani sana katika mtindo wao wa kucheza waweze kumgeuzia sura amtazame vyema. Kama walimsikia, huo mtindo ulikuwepo. Akawa anamrushia jicho. Sasa aliweza kumwona vyema zaidi. Alikuwa yeye. “Naomi….Naomi wangu..” walter alijisemea huku akiduwa na kushindwa kufanya michanganyiko ya hapa na pale inayoburudisha. Alitegemea kuwa baada ya tamasha lile angeweza kuonana naye lakini haikuwa hivyo. Watu walikuwa maelfu asingeweza kumwona binti yule. Ulikuwa muujiza mkubwa sana kuweza kumwona Naomi tena baada ya harakati za muda mrefu kugonga mwamba. Sasa amemwona tena. Walter akahisi hiyo ilikuwa nafasi nyingine tena ya yeye kuipata furaha iliyopotea katika ardhi ya Tanzania. Hakujalisha ni miaka mingapi ilikuwa imepita tangu waonane kwa mara ya mwisho. Walter aliamini kuwa Naomi alikuwa msichana wa kipekee sana. Si kwamba hakuwa na msichana mwingine kwa wakati huo la. Alikuwa naye lakini hakuwa na wazo la kumuita mke. Sasa amemuona Naomi ambaye marehemu bibi yake alimbarikia kwa kumwita mkewe. “Huenda bibi amenionyesha tena.” Alijisemea Walter baada ya tamasha hilo. ***ITAENDELEA………
Posted on: Tue, 30 Jul 2013 05:52:39 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015