Simulizi za Kalibonge Barua ya Halima (20) Ilipoishia - TopicsExpress



          

Simulizi za Kalibonge Barua ya Halima (20) Ilipoishia jana... Tukaingia wasiwasi mkubwa sana. Nikataka kwenda kumuangalia, lakini wakati najiandaa kufanya hivyo, akaacha kufanya hivyo, hivyo tukaendelea kulala.” Anaacha kusimulia, anakunywa maji kidogo, anapoiweka bilauri chini anaendelea, “Zikapita kiasi dakika mbili ama tatu, tukasikia tena mkoromo mkubwa. Hapa hakuna aliyesubiri kunyamaza kwake, haraka tukakimbilia chumbani kwake, masikini, alikuwa tayari amekata roho. Kumbe kukoroma kule kulikuwa ni ishara ya roho kuacha mwili.” Anasema mzee wa watu kwa masikitiko makubwa. Endelea... “Ni jambo la ajabu sana.” Anasema mzee Daud kabla ya kuendelea, “Hatukudhani kama angalifikia uamuzi huu wa ajabu, Halima hakuwa na tabia kama hii na alipotuambia tu juu ya mkasa wake tulifahamu halikuwa kosa lake. Hakupaswa kufanya hivi.” Anatulia tena, anaangalia chini kidogo na anapoinua kichwa anaendelea. “Usiku ule hatukuwa na jambo la kufanya na kwa sababu alikuwa tayari amekufa, tukawaarifu majirani ambao walianza kuja.” “Lengo letu tusubiri kupambazuke na tukae kikao cha familia ili kupanga wakati wa kuzika, lakini wakati kukikaribia kupambazuka, chumba kizima kilijaa harufu, alianza kuoza. Ona maajabu haya mtu amefariki saa chache zilizopita, lakini ameanza kuoza utafikiri amefariki siku kadhaa zilizopita.” “Harufu hii, ikatufanya tuingie kule chumbani alikohifadhiwa maiti, laa haula! Ndipo tukagundua kuwa amejiua, amekunywa sumu, kwani mwili ulivimba sana na ulikuwa mweusi ti! Baada ya kukagua ndipo tukaiona pakiti ya sumu, alibwia yote. Na mezani tukaikuta bahasha ambayo ilikuwa imeandikwa jina lako. Pia palikuwa na kikaratasi kidogo kimegandamiziwa na simu.” Mzee Daud anaacha kusimulia, anaingiza mkono kwenye mfuko wa shati na kutoa kipande kidogo cha karatasi, ananipa nami nakipokea na kukisoma. “Tafadhali, mpeni taarifa mwenye barua hiyo hapo mezani. Kama atawahi kunizika ama la, ila taarifa apewe. Tumieni simu hiyo na akifika akabidhiwe hiyo barua pia.” Namaliza kukisoma, pale chini ya karatasi paliandikwa namba yangu ya simu. “Kutokana na hali ile.” Anaendelea mzee Daud baada ya kuona nimemaliza kukisoma kilichoandikwa kwenye kile kipande cha karatasi. “Ikatulazimu kufanya mipango ya mazishi haraka. Tukawaamsha vijana ambao walikwenda kuchimba kaburi na tukamzika mara tu baada ya swala ya alfajiri. Watu wengi wamepata taarifa baada ya kuzikwa na hawakuamini kilichotokea.” Anatulia na kuvuta pumzi ndefu. “Baada ya kuzika ndipo nikafanya kama alivyoagiza marehemu, lakini hukupatikana hata nikashauriwa nikutumie ujumbe mfupi na utakapowasha basi utapata taarifa.” Anamaliza kusimulia na kutulia kimya. Naukumbuka ujumbe mfupi baada ya simu yangu kukubali kuwaka. “Halima amefariki dunia na ameacha ujumbe wako.” ******************** Ni asubuhi ya siku hii ndipo naupata ujumbe huu uliotumwa kiasi siku tatu nyuma. Nakuwa kama mtu mwenye ulevi kichwani. Wakati huo zimeshapita siku tatu tangu afariki lakini ni siku nne tangu nikutane naye pale Jamatini. Napagawa sana hata sijui nifanye nini, najikuta naparamia gari langu na kuliwasha halafu kwa mwendo wa kasi, naitafuta barabara ya Iringa, hata nikafika kijijini hapa. Nikasimamisha gari mbele ya nyumba ambayo kwa nje tu ilionesha huzuni kuu ndani yake. Nadhani ni muungurumo wa gari ndiyo uliotoa mzee huyu niliyemuona siku ile asubuhi. Sikufahamu kuwa ndiye baba yake marehemu mpaka pale alipojitambulisha. Akanikaribisha ndani ambako kulikuwa na watu wachache hasa wanaume. Pia ukumbi mwingine kulikuwa na wanawake wachache. Yule mzee akaingia chumbani na kutoka na bahasha, akanikabidhi, nikaipokea na kuanza kuisoma. Nikaisoma mara ya kwanza, nikaimaliza, nikairudia tena na tena na tena na zaidi. Nikalia sana na kuumia moyo wangu. Wakati nasoma barua hii, ndipo mzee Daud akaniuliza. “Vipi baba hupendi kwenda kupaona alipolala mwenzio?” Sikumjibu bali nikasimama ishara ya kutaka kupelekwa huko haraka. Tukatoka nje na wale watu wengine na safari ikaanza kuelekea makaburini. Tukiwa njiani, ndiyo mzee huyu akanitambulisha wale vijana wake. “Huyu ni kaka yake marehemu, anaitwa Sufiani na huyu hapa ni pacha wake, Jemedari.” Baada ya utambulisho huo kikatawala kimya mpaka tunafika makaburini. ******************** Muda umekwenda sana, natoa simu yangu mfukoni na kuangalia, naona kuwa ni saa tisa unusu alasiri. Namuangalia mzee Daud, yupo kimya, namuangalia Sufiani, naye yupo kwenye tafakuri nzito, nayarejesha macho kwa Jemedari, namuona ameinamisha kichwa chini. Amedhoofu ghafla na mnyonge kuwahi kumuona. Nami natulia kimya. Sasa kila mtu yupo kimya. Naamua kuuvunja ukimya huu. “Baba!” Naita. Mzee Daud haitiki, bali ananiangalia usoni. “Mimi naomba ridhaa yenu!” Namwambiaa. Bado hasemi kitu, ila anasimama, nami nasimama, na Sufiani na Jemedari. Tunasimama halafu taratibu tunatembea kuelekea kwenye nyumba. Tunalifikia gari na tunasimama. “Haya kijana, safari njema.” Ananiambia huku ananipa mkono, nami naupokea. “Asante baba, tutaonana siku nyingine. Naomba mnipe taarifa wakati wa arubaini yake.” Nasema huku nikiacha mkono wa mzee Daud. Nauzungusha mkono hadi kwa Sufiani, kisha moja kwa moja kwa Jemedari, naagana nao halafu naingia kwenye gari langu. Nalitia moto na kurudi nyuma, naligeuza na kushika njia kurudi mjini. Mwisho. *********** NB: Simulizi hii ni ya kubuni tu na katu haihusiani na tukio lolote la kweli. Majina ya wahusika na mandhari vimetumika ili kuipa uhalisi. Mtiririko wa visa na matukio ni ubunaji utokanao na zao la akili ya mtunzi na mwandishi. Tunawashukuru sana wasomaji wetu na wapenzi wote wa ukurasa huu kwa kutuunga mkono. Tunajivunia thamani ya uwepo wenu na tunaahidi kuyafanyia kazi mawazo na maoni yenu ambayo baadhi yunu mmukuwa mkitutumia. Pia waweza kututumia maoni yako kupitia chiefmakolekoii@yahoo au msg katika ukurasa wetu huu. Tukutane jumatatu panapo uhai ambapo tutakuwa na RIWAYA ya kusisimua, REBECCA ambayo awali ilitoka kupitia blog yetu ya makoleko.blogspot/ Tunawatatkia Ijumaa njema___
Posted on: Fri, 16 Aug 2013 01:50:16 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015