Simulizi za Kalibonge Nilimuua dada yangu ili niolewe na - TopicsExpress



          

Simulizi za Kalibonge Nilimuua dada yangu ili niolewe na Shemeji Ilipoishia jana... Sijui hata machozi yalinitoka wakati gani, ila nilimuona dada naye akilia tena sana hata shangazi akaamuru nitolewe nje akiwa anagoma. “Nyie watoto wapumbavu sana. Kinachowaliza nini? Mmeambiwa hapa kuna msiba. Wacheni haraka na huo uchuro hatuutaki, ebo!” Nilipotolewa huko nikapelekwa chumbani kwa mama na baba. Nikajitupa kitandani na kupitiwa na usingizi mzito ambao sijawahi kulala hata siku moja. Nikiwa usingizini nikaota ndoto-ndoto ambayo sitoisahau hata siku kwani ndiyo hasa iliyonifanya kutokubali kushindwa. Endelea... Niliota kuwa, shamrashamra zile zote zilikuwa ni kwa ajili yangu na siku ilipofika mimi ndiyo niliolewa. Tena kitu cha kushangaza ni kuwa niliolewa na yule yule mchumba wake dada. Sikuweza kuimalizia ndoto hii kwani nilikuja kuamshwa na mama. “Wewe vipi, unaumwa?” “Hapana mama siumwi.” “Sasa unacholala namna hiyo nini?” “Nimechoka tu mama.” “Dada yako amekuja, anakutafuta.” Sikusubiri kufafanuliwa kuwa ni dada gani, akili yangu ilikwishajua ni dada yupi, hivyo nilikurupuka hadi sebuleni. Hapo niliishia mwilini mwa dada ambaye alinipokea na kunifunika na mwili wake. Alikuwa ni dada wa Uingereza, amekuja kwenye ndoa. Ingawa nilifurahi kumuona lakini niliumia sana. Dada amesafiri kutoka Uingereza tena akiambata na mumewe kuja kwenye ndoa hii, jamani! Nikiwa bado katika mwili wa dada, nikamsikia mama akisema kumwambia dada. “Kaka yako amepiga simu, yuko Nairobi. Wamekwama hapo kwa sababu ya hali mbaya ya hewa, hivyo amesema atakuja kesho usiku.” Moyo wangu ukazidi kugawanyika tena sasa haukuwa vipande viwili ila vipande vingi ambavyo hata ingalikuwa vipi, haviwezi kuunganishwa na kupata kitu kimoja. Nikajibandua mwili mwa dada halafu nikaenda hadi kwa shemeji kumsalimia huku dada akiingia chumbani kwa bibi harusi. Nilipotosheka kuongea na shemeji nikaingia tena chumbani kwa dada bibi harusi. Huko nikawakuta wamekaa, dada bibi harusi, dada mkubwa na shangazi; wale wataalamu walishaondoka kwani walimaliza kumchora bibi harusi. Nami nikajumuika nao, lakini wakati wote wa maongezi sikuchangia hata jambo moja huku nikimuangalia dada bibi harusi kila mara nilipopata nafasi. Alikuwa amependeza na michoro yake. Roho ikawa inaniuma na wivu ukizidi kuchukua nafasi yake katika moyo wangu. Nilihisi kuwa dada anapendwa zaidi kuliko watoto wengine. Haiwezekani mtu kutoka Uingereza kuja kwenye ndoa. Ni fedha kiasi gani ameteketeza kutoka huko hadi hapa? Kwani asingalikaa huko ndoa isingalipita? Sawa anayeolewa ni ndugu yake tena wa kuzaliwa tumbo moja na ana kila sababu ya kuja, lakini mimi sikuona umuhimu wa kuja. Na nililiona hili kwa sababu ya kuolewa dada na wivu niliokuwa nao juu yake. Wivu huu haukuishia hapo tu. Nikakumbuka kauli ya mama wakati anamwambia dada kuwa kaka naye yuko njiani. Huyu naye amesafiri kutoka Nigeria hadi hapa kuja kwenye ndoa. Bado moyo wangu uliumia sana nilipoyawaza mambo haya. Niliona wazi nafasi yangu inapungua kutoka kwa ndugu zangu na swali nililokuwa najiuliza ni kuwa, je wakati wa ndoa yangu, watu hawa watafunga safari kutoka maeneo yao ya mbali kuja kuungana na familia? Sikupata jibu ingawa wakati mwingine nilipata jawabau la ndiyo kuwa watakuja kwa kuwa nami ni mmoja wa wanafamilia ambaye nina haki kwao nao wana wajibu kwangu. Na hapa likaibuka swali linguine, kama watakuja, hizo shamrashamra zake zitakuwa kama hizi ninazoziona hapa? Hapa nikapata majibu yenye utata huku nikiamini kuwa pengine wakati huo hawatokuwa katika hali walizokuwa nazo sasa, watakuwa katika hali gani? Jibu lake ni kitendawili cha maisha. ******************** Hatimaye siku yenyewe ikawadia. Ilikuwa siku ya maumivu pasipo mfano na ilikuwa siku ya furaha pasipo mfano. Kwangu ilikuwa ni kuugulia maumivu ingawa nilishiriki katika kila tukio nililotakiwa kushiriki. Sikuwa na uwezo wa kukataa kufanya jambo lolote nililotakiwa kufanya. Kuna wakati niliazimia kutofanya jambo lolote, lakini nafsi ikawa inanisuta hata nikashindwa. Upande wa dada ilikuwa ni furaha na masham sham kila nilipomuangalia alikuwa ni mtu wa kutabasamu kila wakati. Ndoa ilipangwa saa saba mchana ambapo shughuli zote za kuozesha zitafanyika hapa nyumbani halafu ikaandaliwa karamu katika ukumbi mmoja maarufu jijini. Hadi kufikia majira ya saa nne asubuhi, maeneo yote kuzunguka nyumba yalikuwa na wageni waalikwa. Waliokaa barazani, sebuleni, uwanjani na popote palipoonekana kufaa kukaliwa na watu. Kila mtu alivaa nguo zilizompendeza; baba, mama, dada, kaka na mdogo wetu hata mimi. Familia ilikutana tena na kuwa kitu kimoja. Huku wenzangu wakifurahi kwa kumaanisha furaha yao kwa tukio hili, mimi nilifurahi ili nisijulikane nina nini ndani yangu. Niliungua ndani kwa ndani ingawa nje nilikuwa mtu mwenye furaha pengine hata kuwazidi watu wote waliohudhuria. Wakati huo bado bwana harusi alikuwa hajawasili, lakini mambo yalikuwa yamepamba moto, watu wengi walihudhuria, rafiki zake dada bibi harusi hasa yule shoga yake ambaye alikuwa mpambe wa bibi harusi, alipendeza sana, na wale wa dada mkubwa. Rafiki zake kaka nao walikuwepo na rafiki zangu pia. Ilipotimia saa sita unusu, tukaona msururu wa magari ambayo yalikuwa yamepambwa vizuri. Kwa haraka sikuweza kufahamu bwana harusi alikuwa katika gari lipi kwa sababu yote yalipambwa kwa namna moja. Msafara ule ukaelekezwa sehemu maalumu ya kupaki na baada ya kupaki watu wakaanza kuteremka mmoja mmoja. Katika gari moja waliteremka watu watatu; wanawake wawili na mwanaume mmoja. Hawa walikuwa ni watu wazima kiasi na sikupata shida kumtambua huyu mwanaume kwani alifanana sana na bwana harusi ambaye hadi wakati huu sijamuona. *************** Msikose kuungana nasi tena Jumatatu!. Tunawatakia Al Jumaa al kareem___
Posted on: Fri, 08 Nov 2013 02:07:07 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015