Simulizi za Kalibonge Nilimuua dada yangu ili niolewe na - TopicsExpress



          

Simulizi za Kalibonge Nilimuua dada yangu ili niolewe na Shemeji (8) Ilipoishia Ijumaa iliyopita... Ilipotimia saa sita unusu, tukaona msururu wa magari ambayo yalikuwa yamepambwa vizuri. Kwa haraka sikuweza kufahamu bwana harusi alikuwa katika gari lipi kwa sababu yote yalipambwa kwa namna moja. Msafara ule ukaelekezwa sehemu maalumu ya kupaki na baada ya kupaki watu wakaanza kuteremka mmoja mmoja. Katika gari moja waliteremka watu watatu; wanawake wawili na mwanaume mmoja. Hawa walikuwa ni watu wazima kiasi na sikupata shida kumtambua huyu mwanaume kwani alifanana sana na bwana harusi ambaye hadi wakati huu sijamuona. Endelea... Wale wanawake wawili sikuweza kubashiri walikuwa ni akina nani ila nadhani mmoja wao ni mama wa bwana harusi ingawa sikuwa na uhakika. Baada ya kuteremka nikamuona baba akiwakimbilia halafu wakakumbatiana na yule baba yake bwana harusi. Akawasalimia na wale wanawake kisha akawaongoza kuingia ndani. Watu wakateremka katika magari yote isipokuwa gari moja na baada ya wale waliotangulia kuteremka kuoneshwa sehemu ya kukaa, sasa ikawa zamu ya watu wa gari hili kuteremka. Kwanza waliteremka watu watatu halafu wakajipanga mstari mmoja kama wafanyavyo wanajeshi, halafu mmoja kati yao akaenda kufungua mlango wa gari. Hapo akateremka mtu mmoja mrefu wastani. Vile alivyo nikashtuka, nilidhani bwana harusi, lakini hakuwa ndiye. Walifanana sana ila tofauti yao ni kuwa huyu alikuwa na nywele nyingi na alikuwa miraba minne, tofauti na muhusika mkuu ambaye hupenda kunyoa nywele na kuziacha chache sana na alikuwa mwembamba ingawa wembamba wake uliendana naye. Pia huyu alionekana mkubwa kutokana na kidevu chake kukomaa na kuashiria amenyoa mara nyingi sana. Alikuwa amevaa suti nyekundu ambayo ilionesha wazi kuwa ni ya bei mbaya na ilimkaa vema. Alipoteremka, akalizunguka gari hadi upende ule wa pili. Huko aliufungua mlango na akateremka mtu ambaye hakuwa mgeni machoni pangu ila vile alivyotokelezea, jamani roho ikaniuma sana. Shemeji alikuwa amevalia suti nyekundu kama alivyovaa kaka yake na ilimpendeza sana. Baada ya kuteremka alimshika mkono na kumuongoza kulizunguka gari tena kuja upande huu walikosimama wale vijana wengine watatu. Walipowakaribia, kijana mmoja kati yao akatangulia mbele, halafu wakafuatia bwana harusi na kaka yake, kisha wakafuatia wale vijana wawili. Wakawa wanatembea taratibu sana huku wakisindikizwa na shangwe na vigelegele. Walipoikaribia nyumba, akatokea baba na kaka wakawapokea na kuwaingiza ndani. Baada ya dakika tano baada ya watu hawa kuingia ndani, vikasikika vigelegele na shangwe nyingi sana kutoka ndani. Shangwe na vigelegele vile vikapokewa na watu wa nje hasa akina mama. Kila mtu alikuwa anafurahia kwa namna yake, wengine walipiga makofi, wengine wapiga mabati alimradi kila mmoja alionesha kufurahi. Sasa ukafika ule wakati uliokuwa unasubiriwa na watu wengi; wakati wa bwana harusi kumuona bibi harusi. Wakati huu ulikuwa mgumu sana kwangu. Niliumia kuliko kawaida, moyo ulichoma kama kidonda kibichi kilichotiwa chumvi, nyie wacheni tu jamani mapenzi haya! Bwana harusi akaelekezwa chumbani kwa bibi harusi. Akaingia huko akiambatana na kaka yake na baba yake. Nyuma yao alikuwa baba na kaka. Wakaingia chumbani kwa bibi harusi ambako kulikuwa na watu kadhaa; mama, dada, shangazi, mimi, bibi harusi mwenyewe na shoga yake ambaye ndiyo mpambe wake na wale wanawake walioteremka garini ambao baadaye nilikuja kumfahamu mmoja kuwa ni mama yake wa kufikia, mama yake mzazi alishafariki zamani. Walipoingia chumbani, ukafanyika utambulisho mdogo wa haraka haraka na baada ya kufahamiana sasa ikawa zamu ya bwana harusi kumfunua bibi harusi. Hapo sasa nilipotamani ardhi ipasuke ili niingie ndani nijifiche huko kwani sikutaka kushuhudia tukio hili. Bwana harusi akasogea mpaka pale dada alipo kisha akamfunua na kumbusu kisha wakakumbatiana. Vikafuata vigelegele ambavyo kama kawaida vikapokelewa huko nje. Zikafuata taratibu nyingine ikiwa ni pamoja na kusaini cheti cha ndoa na shughuli nyingine. Zikapigwa picha za kutosha kwa ajili ya kumbukumbu na baada ya kukamilika shughuli hii ya hapa nyumbani. Matukio hayo yalipokamilika, bwaba harusi alikabidhiwa mkewe kisha wakaondoka kwa mtindo ule ule waliokuja nao kuelekea upande wa mwanaume huko Kimara. Pale nyumbani walibakia wanafamilia wachache na watu wengine huku, mimi, baba, mama, dada, kaka na shangazi tukimsindikiza bibi harusi. Huko tukakuta watu wengi ajabu na walionekana kuwa na shauku ya kumuona bibi harusi. Tulipofika, tuliteremka garini na kuelekezwa sehemu ya kukaa kisha maharusi nao wakateremka wakaingia ndani hadi chumbani ambako kulikuwa maalumu kwa ajili yao. Walipoingia huko nami nikaingia na waliponiona walifuarahi sana hasa shemeji alifurahi kuniona. “Wow! Bi mdogo nilidhani tumekuwacha kule nyumbani, kumbe umekuja huku. Karibu sana.” “Mniache na nikubali kuachwa, we unafanya mchezo nini?” tukataniana sana hata tukafurahi. Kitu ambacho kilinishangaza siku hii ni kumuona dada kutonichangamkia. Na alionekana kama mtu mwenye duku duku moyoni na alikuwa anataka kusema ila alishindwa. Pia alikuwa mtu mwenye aibu nyingi sana kila tulipokutanisha macho aliinamia chini na kusugua vidole. Sikujua hali hii imetokana na nini au ndiyo ndoa hiyo. Sikumuuliza ana kitu gani na vile alivyokuwa ananiangalia mara kwa mara nilihisi labda kuna kitu amekigundua kwangu hasa vile nilivyokuwa najilazimisha kufurahi na kuzungumza nao. Nilijua amenishtukia hivyo nikajitahidi kutoonesha hali yoyote ya kumchanganya zaidi. ************ Itaendelea kesho!. Tunawatakia siku njema___
Posted on: Mon, 11 Nov 2013 01:56:52 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015