WANAVYOSEMA JUU YA BIBI TITI NA TANU HADI KENYA TANU katika - TopicsExpress



          

WANAVYOSEMA JUU YA BIBI TITI NA TANU HADI KENYA TANU katika Mombasa, Kenya, 1957 Mwalimu Kihere alikuwa mwanasiasa wa msimamo wa wastani, alikuwa mbali na msimamo mkali dhidi ya serikali. Kwa ajili hii Mwalimu Kihere alielewana vizuri na utawala wa kikoloni. Hii ilikuwa kinyume kabisa na wazalendo wengine kama Mzee Makoko Rashid ambaye kwa miaka mingi alijulikana kwa chuki yake dhidi ya Waingereza. Inasadikiwa kwamba watu wawili wataingia katika historia kwa chuki zao mahsusi dhidi ya Waingereza, mtu wa kwanza ni Abdillah Schneider Plantan na wa pili ni Mzee Makoko Rashid. Wote wawili walifungwa gerezani kwa sababu ya msimamo wao dhidi ya serikali ya kikoloni. PC na DC wake wote wawili walikukubali mwaliko wa Mwalimu Kihere. Mwalimu Kihere alimtambulisha Nyerere kwa wageni mashuhuri na alimuomba azungumze maneno machache. Nyerere kwa kipaji chake cha ufasaha wa kuzungumza alitoa hotuba kuhusu lengo la TANU na kanuni za kidemokrasia kama zilivyoelezwa na Umoja wa Mataifa. P.C. alisimama baada ya Nyerere kuzungumza na akatoa hotuba kwa niaba ya serikali. P.C. alimsifu Nyerere kuwa ni mwanasiasa mzuri kinyume na vile alivyosikia kabla ya kukutana naye. Hapo hapo alitoa ruhusa kwa Nyerere na TANU kufanya mikutano ya hadhara katika wilaya zote za jimbo hilo. Lakini uhusiano huu haukudumu, serkali iliyapiga marufuku matawi kadhaa ya TANU Tanga mara tu baada ya kuundwa kwa UTP. Siku iliyofuata mabingwa wa hotuba wa TANU, Julius Nyerere na Bibi Titi Mohamed walihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Tangamano. Hii ilikuwa hatua kubwa sana kwa TANU, na kwa harakati dhidi ya ukoloni pale Tanga. Ilikuwa muda mrefu umepita tangu zile siku za zile siasa za wasomi katika Discussion Group, kikundi cha majadiliano; na ile mizozo baina yao na ule uongozi Waarabu katika TAA. Baada ya hapo, Mwalimu Kihere alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TANU Tanga badala ya Hamisi Heri na Amos Kissenge alichaguliwa katibu. Abdallah Rashid Sembe mmoja wa wanachama waasisi wa mwanzo kabisa wa TANU alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU akiwakilisha Jimbo la Tanga. TANU katika Mombasa, Kenya, 1957 Mambo yalikuwa yanageuka dhidi ya Waingereza katika makoloni yake yote Afrika ya Mashariki. Wazalendo walikuwa wakifanya harakati zao na kuvuka mpaka mmoja wa nchi hadi mwingine bila matatizo. Ule wakati wa wao kusafiri kwa kificho na kufanya mikutano yao nyakati za usiku mafichoni ulikuwa umepita. TANU ilikuwa na nguvu ya sasa kuangali nje ya mipaka yake. Katika pwani ya Kenya katika mji wa Mombasa, kijana mmoja kutoka Moshi, Ismail Bayumi, aliyeajiriwa na Mombasa Municipal Council akivutika na mwenendo wa matukio ya kisiasa kama yalivyokuwa yakitokea katika Afrika Mashariki, aliwashawishi Watanganyika waliokuwa wakiishi na kufanya kazi Mombasa kuunda kile kilichokuja kujulikana kama Mombasa TANU Club. Sheria ya Kenya haikuwaruhusu Watanganyika kuunda chama cha siasa katika ardhi ya Kenya, kwa hiyo TANU Club ilisajiliwa kama chama cha starehe na ilikuwa na ofisi zake katika Barabara ya Lohana. Ismail Bayumi alichaguliwa rais wake wa kwanza. Lakini kwa hakika TANU Club ilifanya kazi kama chama cha siasa kwa niaba ya TANU, KANU na KADU kwa kiwango fulani. Wakati huo Jomo Kenyatta alikuwa Manyani akitumikia kifungo cha miaka saba gerezani kwa kuhusika na harakati za Mau Mau. Tom Mboya aliitumia TANU Club kuifanyia kampeni KANU na kupigania kufunguliwa kwa Kenyatta kutoka gerezani. Kote nchini Kenya KANU ilikuwa ikiibuka kama chama cha wananchi wote. Wakati sera za KANU zilikuwa zile za mwelekeo wa kuwaunganisha wananchi wote dhidi ya ukoloni, KADU chini ya Ronald Ngala, kwa upande mwingine, ilikuwa na labda isemwe, ufahamu mfinyu, KADU ikifungamanisha sera zake na siasa za ukabila na utawala wa majimbo. Kwa hiyo KADU ilikuwa ikikusanya nguvu za upinzani wa makabila madogo dhidi ya KANU. KANU chini ya Kenyatta, Jaramogi Oginga Odinga na Tom Mboya, ilichukuliwa kuwa ni chama cha makabila mawili makubwa nchini Kenya, yaani Wakikuyu na Wajaluo ambayo yakiachiwa kutawala yatameza makabila madogo. Nchini Tanganyika ambako ushindani wa kikabila katika siasa haukuwepo, TANU Club ilijikuta kiitikadi inapenda kuwa karibu zaidi na KANU kuliko KADU. TANU Club ilikuwa ikiandaa dansi katika Ukumbi wa Tononoka na dansi hizi zilikuja kupendwa sana na wanasiasa wa Kenya. Ilikuwa chini ya pazia la sherehe hizi katika Ukumbi wa Tononoka ndiyo wanasiasa wa Kenya na wale wa TANU Club walipata nafasi kupashana habari namna TANU ilivyokuwa ikiendelea nchini Tanganyika na nini TANU ingeweza kufanya huko Tanganyika ili kusaidia harakati za kudai uhuru nchini Kenya. Baada ya TANU Club kufanikiwa sana huko pwani uongozi wake uliamua kufungua tawi la TANU Club mjini Nairobi katika sehemu ya Pumwani. Tom Mboya na Ronald Ngala walikuwa mstari wa mbele katika sherehe zote za TANU Club, wakishiriki katika shuguli zake Mombasa na Nairobi. Msukumo mkubwa wakati ule nchini Kenya ilikuwa kufanya kampeni ya nchi nzima kuwashinikiza Waingereza wamwachie huru Kenyatta aliyekuwa akichukuliwa na wananchi wote kama kiongozi na nguvu ya umoja wa Waafrika wa Kenya. Katika wimbi hili la kutaka Kenyatta afunguliwe kutoka gerazani, Tom Mboya alimdokeza Ismail Bayumi kuwa TANU ingeweza kusaidia katika kampeni hii ya kuwashinikiza Waingereza kumtoa Kenyatta kifungoni. Ismail alifikisha wazo hili makao makuu ya TANU mjini Dar es Salaam kwa kupitia mtu maalum aliyekuwa akiwasiliana na Tom Mboya na Nyerere kwa siri. TANU ilimtuma Bibi Titi Mohamed kwenda Kenya kuzitia shime harakati za kufunguliwa Kenyatta. Wazalendo nchini Kenya walikuwa wameshindwa kabisa kuwaingiza wanawake ndani ya KANU hivyo kuzinyima harakati za uhuru nguvu kubwa sana na ya kutegemewa ya akinamama. 175 Huko Mombasa TANU Club ilifikiria kuwa kumleta Bibi Titi kuja Kenya kuifanyia kampeni KANU ilikuwa ni kitu kipya cha kuwahamasisha wanawake ndani ya KANU na kwa hiyo kuongeza nguvu mpya na kutia ari ya utaifa katika Kenya. Bibi Titi alikuja Mombasa na kufanya mkutano Ukumbi wa Tononoka. Kwa kawaida kwa madhumuni ya kupata kibali mikutano hii ilikuwa inahesabiwa kama ni mikusanyiko ya kufanya sherehe siyo mikutano ya siasa na ilikuwa ikifanyika ndani. Lakini mkutano huu ulikuwa na umuhimu wake kwa sababu ya kuwako Bibi Titi Mohamed mjini Mombasa. Wengi walikuwa wamemsikia Bibi Titi lakini hawakuwa wamepata kumuona. Watu walijaa ndani ya ule ukumbi hadi nje kuzunguka viwanja vya Ukumbi wa Tononoka. Kwa kweli kwa hali yoyote mkutano ule usingeweza kuitwa kuwa ni mkutano wa wanachama wa TANU Club mjini Mombasa, au hata mkutano wa TANU Club Kenya nzima, kwa sababu wanachama wa KANU waliwazidi wanachama wa TANU Club kutoka Tanganyika. Kenya ilikuwa bado haijaweza kumtoa hata mwanamke mmoja wa kiwango cha Bibi Titi. Kwa wakati ule kumwona mwanamke wa Kiislamu amesimama bila baibui akihutubia halaiki ya wanaume ilikuwa ni jambo la kushangaza sehemu za pwani, ambako wanawake walitembea huku wamejifunika mabaibui na hawakutakiwa hata kufanya kazi maofisini. Bibi Titi alifanya mikutano kule Mombasa na Nairobi akiwasisitizia watu wasikate tamaa wasimame pamoja hadi Kenyatta amefunguliwa kutoka gerezani. Habari za mikutano hii iliandikwa kwa mapana na marefu na magazeti ya Mombasa Times na Taifa Leo. Miongoni mwa Wakenya kule pwani waliyofanya kazi karibu sana na TANU Club walikuwa Msanifu Kombo na Abdallah Ndovu Mwidau. Kombo na Mwidau kwa sababu ya mchango wao kwa KANU kupitia chama chenyewe na kupitia TANU Club wakaja kuwa na ushawishi mkubwa kwa Rais Kenyatta. Wazalendo hawa wawili baada ya uhuru wa Kenya wakawa watu wenye sauti kubwa kule pwani. Hakuna mtu kutoka pwani alikuwa anaweza kuteuliwa na kushika nafasi yoyote muhimu na Kenyatta bila Abdallah Mwidau na Msanifu Kombo kumuunga mkono. Mara tu baada ya kufunguliwa kutoka gerezani, Kenyatta alikwenda Mombasa kutoa shukrani zake kwa Msanifu Kombo, Abdallah Mwidau na TANU Club kwa msaada wao kwa KANU na kwa kufanya kampeni ya kufunguliwa kwake. Mkutano ulitayarishwa kule Tononoka na Kenyatta alikuja kutoa hotuba ya shukrani na kukutana na wanachama wa TANU Club. Mkutano wa Tabora ¬ Njia Kuelekea Uhuru, 1958 Mkakati wa Tanga, 1958 Mwaka 1958 serikali ya kikoloni iliandaa uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya utaifa. Kulikuwa na viti kwa ajili ya Wazungu, Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka, awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika kazi maalum. Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza kukubalika na TANU. TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa 1958 mjini Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari kujadili miongoni mwa mambo mengine ikiwa ishiriki katika uchaguzi chini ya masharti haya ya kibaguzi yaliyowekwa au wasuse. Mkutano ule ulitishia kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU katika makao makuu, na Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa TANU, kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama kama isingelikuwa busara ya Julius Nyerere, Rais wa TANU. Lakini ili kuzielewa hisia za wanachama wa TANU, fikra za uongozi wake na nguvu zilizokuwa zikidhibiti siasa Tanganyika wakati ule wa ukoloni, na ili kuelewa kwa nini kura tatu ilileta mgogoro na kutoelewana katika uongozi, inatubidi turudi nyuma tufuatilie mwanzo wa siasa mjini Tabora, mahala ambapo TANU ilifanya uamuzi wake ya kihistoria na kuwanasa Waingereza katika mtego wao wenyewe. Tunahitaji kuyatazama mambo kwanza kuanzia Tanga mahali ambapo Nyerere na uongozi wa TANU pale Tanga walikutana kwa siri kuweka mikakati ya mkutano wa Tabora. Baada ya kufanya hivyo tufichue jambo moja baada ya jingine katika ule mkutano ambao wajumbe wa TANU walikutana katika ukumbi wa Parish wa Kanisa Katoliki, Tabora. Hii itatuwezesha kujua kwa nini mkutano mkuu huu ulikuwa muhimu na kwa nini kutokana na mkutano huu Waislam ambao walijitoa mhanga sana katika kudai uhuru, mara tu baada ya uchaguzi huo walianza kupoteza nguvu yao katika siasa hatimaye kutupwa nje na katu hawakuweza kurejesha tena nguvu hiyo hadi hivi sasa. Akiiandikia Fabian Colonial Bureau, katibu mwenezi wa TANU, Zuberi Mtemvu ambae alikuwa amelichambua jambo hili la utatanishi aliandika: Katika nchi kama Tanganyika, utajiri na elimu vimo mikononi mwa wageni. Mwafrika ni maskini na hana elimu. Upigaji kura wenye masharti magumu yaliyoegemezwa kwenye mali na elimu utawaathiri Waafrika peke yao bila kuwagusa Wazungu na Waasia hata kidogo. 176 TANU kwa hakika kilikuwa chama cha Waislam; kwa hiyo ilikuwa ni dhahiri kuwa kuyakubali masharti yale ya kibaguzi ya upigaji kura ilikuwa sawasawa na kuwasukuma Waislam ambao ndiyo walikuwa wafuasi wakubwa wa chama nje ya wigo wa siasa. Nimtz ameandika kwa ufupi hali ya Waafrika katika uchaguzi wa mwaka wa 1958 na 1959 katika mji wa Bagamoyo, mji ambao ni wa Waislam: ...kutokana na sifa za wapiga kura na masharti magumu ambayo serikali ya kikoloni iliweka, upigaji kura ulibakia kwa asilimia ndogo sana ya Waafrika ambao ndiyo waliokuwa wengi. Katika Wilaya ya Bagamoyo ambako uchaguzi ulifanyika mnamo Septemba, 1958, watu 630 tu, katika idadi ya watu 89,000, ndiyo waliyojiandikisha. 177 Ujumbe wa Nyerere mwenyewe kutoka makao makuu ulikuwa na watu wengi ambao wasingeweza hata kidogo kusimama kama wagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao makuu ya TANU yalikuwa yanawakilishwa kwenye mkutano mkuu na Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Haidari Mwinyimvua na Rajabu Diwani. Hii ilikuwa na maana uongozi wa Waislam kule Dar es Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine nchini Tanganyika usingeweza kusimama kama wagombea uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi. Serikali ya kikoloni, ikishirikiana na wamishionari, walikuwa wamewanyima Waislam elimu, sharti lile lile ambalo sasa linawekwa kuwazuia Waislam kushiriki katika siasa. Mkutano wa Tabora ulikuwa uamue ikiwa TANU itashiriki katika uchaguzi na kushindana na UTP au ingesusia uchaguzi huo na hivyo kumpa mshindani wake mkubwa na hasimu wake ushindi wa bure.
Posted on: Sat, 29 Jun 2013 13:46:01 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015