MUHURI WA MUNGU AU ALAMA YA MNYAMA FUNGU KUU: UFUNUO 7:1-4; - TopicsExpress



          

MUHURI WA MUNGU AU ALAMA YA MNYAMA FUNGU KUU: UFUNUO 7:1-4; 13:14-18; 14:9 – 11; 16:2; EZEKIELI 9:1 - 6. UTANGULIZI Ulimwengu unakwenda kufikia mwisho wake. Kama ulivyoanza kwa kambi mbili baada ya dhambi kuingia- alama ya Kaini na Damu ya Habili! Ndivyo itakavyofungwa kwa kambi mbili tena. Kambi ya Kristo na Shetani – Muhuri wa Mungu au Alama ya Mnyama. Makundi haya mawili yapo kila dhehebu au dini yeyote duniani. Makundi haya yatakwenda sambasamba mpaka mwisho wa wakati. Muda mfupi kabla ya mlango wa rehema kufungwa kila mwanadamu atakayekuwa hai atakuwa amechagua upande wa kusimama. Kupokea alama ya mnyama ama kupokea muhuri wa Mungu. Kipimo cha mwisho na jaribu kuu la mwisho limejengwa katika UTII kama ilivyokuwa pale Edeni. Matunda yote Adamu alipewa kuyatunza na kuyatumia kasoro mti mmoja wa ujuzi wa mema na mabaya. Haukuwa na utamu au sumu tofauti na miti mingine, bali ulikuwa na tamko la Mungu kwamba USILE! Ulikuwa ni kipimo cha utii! Mungu ameweka siku saba katika juma. Siku zote zipo sawa machoni pa wanadamu wote. Bali kuna siku moja tu ambayo Mungu amesema TUSIITUMIE kwa shughuli zetu! Nayo ni siku ya Saba. Kutoka 31:12 – 17; 20:8-11. Hii ni amri ya milele. Lakini watu wamefanya mchezo ule ule wa Adamu na Hawa. Wameitumia kwa shughuli zao za maisha. Nyakati zinakuja siku ya Saba itasimama kama kipimo cha utii kwa wanadamu wote. Uamuzi usioyumba utaamuliwa juu ya maisha ya watu kwa namna tutakavyojibu kuhusiana na amri hii ya nne. Wengi wetu ndani ya kanisa tunaisogelea Sabato kama Hawa kwa kuiona kuwa ni siku ya kutamanika kwa kununua vocha zetu, kupasi, kutazama Televesheni, kupasi nguo, kununua vitu au kuuza kwa njia ya simu, usomaji wa magazeti siku ya Sabato ama kuangalia mipira na michezo ya kuigiza siku ya Sabato. Matendo hayo yote yanatupelekea katika uasi na uhalifu wa amri hii ya Mungu kwa kuiona siku hii kuwa sawa na nyingine. Jumapili na Jumamosi ndiyo kipimo pekee kitakachoamua kupokea alama ya mnyama au muhuri wa Mungu. Mama White anasema kuwa: “Ishara au muhuri wa Mungu umefunuliwa katika utunzaji wa Sabato ya siku ya Saba, ukumbusho wa Bwana wa uumbaji… Chapa ya mnyama ni kinyume cha hii – utunzaji wa siku ya kwanza ya juma.” – 8T 117 (1904). SOMO MUHURI WA MUNGU Muhuri wa Mungu unatiwa katika vipaji vya uso na wala sio katika mikono (Ufunuo 7:3; 14:1). Muhuri wa Mungu unatiwa katika paji la uso ikimaanisha lazima kila moja aukubali wokovu kwa hiari yake na sio kwa kulazimishwa. Muhuri wa Mungu ni tabia ya Kristo maishani mwetu. Ni alama ya Roho Mtakatifu maishani mwetu (Efeso 1:13). Mama White anasema kuwa: “Si muhuri au alama inayoweza kuonekana kwa macho, bali ni kule kutulia katika kweli, kiakili na kiroho, hata wasiweze kuondoshwa – mara tu watu wa Mungu watakapokuwa wametiwa muhuri na kutayarishwa kwa ajili ya kupepetwa, basi, kutakuja” (4BC 1161). Unapotunza amri kumi za Mungu chini ya maongozi ya Yesu Kristo maana yake ni kuivaa tabia Kristo. Mama White anasema kuwa, “Muhuri wa Mungu aliye hai utawekwa tu juu ya wale wanaofanana na Kristo kitabia” (7BC 970). Katika amri kumi za Mungu ipo alama moja tu ya kuwatambua wale ambao walio na muhuri wa Mungu. Ni Sabato ya Siku ya Saba ya Juma. Utunzaji wa Sabato unaozungumzwa hapa sio utunzaji wa dini bali mahusiano yetu na Mungu tunayokuwa nayo katika ibada yake takatifu. Wapo wengi ambao wanaoitwa Wasabato lakini haiamanishi kuwa watakuwa na muhuri wa Mungu. Zingatia muhuri wa Mungu ni tabia ya Yesu maishani mwetu. Kumvaa Bwana Yesu kikamilifu! Mama White anaeleza swala la Sabato kama muhuri wa Mungu wakati wa pambano kuu la mwisho katika jumapili na Sabato ya Kweli – Jumamosi. Anasema kuwa, “Utunzaji sahihi wa Sabato ndiyo ishara ya utii wetu kwa Mungu” (7BC 981). Sabato ya siku ya Sabato itakuwa ni ishara ya kuwatambua watu wa Mungu pale tu watakapojitoa kuitunza kwa usahihi na pia kusimama imara wakati wa jaribu kuu la mwisho. Paulo anasema kuwa “Imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu” – Waebrania 4:9-11. Anakazia kwa kusema kuwa raha hiyo tunaingia kwa kupumzika kama Mungu alivyopumzika na kuacha kufanya zetu siku ya Sabato. Hivyo muhuri wa Mungu aliye hai kwa watu wa Mungu wa siku za mwisho ni SABATO! Mama White anasema, “Kutakuwa na alama itakayowekwa juu ya watu wa Mungu, na alama hiyo ni utunzaji wa Sabato yake takatifu” (7BC 981)…. Kwetu, Sabato imetolewa kuwa ‘agano la milele’ sawa na ilivyokuwa katika Israeli. Kwa wale wanaoiheshimu sana siku yake takatifu, Sabato ni ishara inayoonyesha kwamba Mungu anawatambua wao kuwa ndio watu wake wateule. Ni ahadi yake kwamba atawatimizia agano lake. Kila roho inayopokea ishara ya serikali ya Mungu inajiweka yenyewe chini ya agano lake takatifu na la milele. Inajifungamanisha yenyewe kwenye mnyororo wa dhahabu wa utii, ambao kila pete yake ni ahadi. Ni amri ya nne peke yake katika zile kumi iliyo na muhuri wa Mtoa-Sheria Mkuu, Muumba wa mbingu na nchi” (6T 350; PP 307). Wale wote watakaopokea muhuri wa Mungu na kukubaliwa kuuridhi uzima wa milele wanapaswa kuwa na sifa zifuatazo: Watakuwa ni watu walioangazwa na Neno la Mungu. “Umwagaji mkuu wa Roho wa Mungu ambao unaangaza dunia kwa utukufu wake, hautakuja mpaka tuwe watu walioangazwa”. – Review and Herald, May 29, 1826. Wamekuwa washindi wa dhambi maishani mwao. Ushindi usiokoma wa dhambi. Watakuwa watu wenye upendo – upendo wa kidugu – wenye shauku kuona wengine wanaokolewa. “Kila alichosema Yesu pendaneni ninyi kwa ninyi kitakapotiliwa maanani ndani ya waumini-wivu, chuki, masengenyo, mawazo mabaya hayatatamanika tena: hayatakuwa na sehemu katika ujenzi wa tabia.” – Review and Herald, October 6, 1890. Watu wenye maombi ya dhati na tena binafsi. “Lakini Mungu ni lazima aamuru mvua kunyesha. Hivyo hatupaswi kuzembea maombi na dua…Hebu tukiwa pamoja na mioyo iliyotubu, tuombe sana kwa dhati kwamba sasa, wakati wa mvua ya masika, manyunyu ya neema yaweze kutumwagia juu yetu”. – Testimonies to Ministers, p. 590. Watu wanaofanya kazi ya Mungu – kuokoa roho za watu. “Umwagwaji mkuu wa Roho Mtakatifu, ambao uliangaza dunia yote kwa utukufu wake, hautakuja mpaka tuwe watu walioangazwa, kwamba kujua kwa uzoefu inamaanisha nini kuwa watendakazi pamoja na Mungu. Wakati tutakapojitoa moyo wote wakfu kwa kazi ya huduma ya Kristo, Mungu atautambua ukweli huu kwa kumwagwa kwa Roho wake pasipo kipimo; lakini hili halitakuwa wakati sehemu kubwa ya kanisa siyo watendakazi pamoja na Mungu” – Christian Service uk. 253 (EV. 699). Kazi ya umishonari inaamsha roho na kuleta kwa wingi zaidi Roho Mtakatifu katika maisha ya mkristo. Maana ni kweli kuwa “kanuni ya kujihudumia mwenyewe ni kanuni ya kujiangamiza mwenyewe. Kanuni ya kujitoa mwenyewe ni kanuni ya kujihifadhi (kujitunza) mwenyewe”. DA, uk. 623. Watu wenye kiasi. Wanaoishi kwa kanuni za afya ya kimwili, kiroho na kiakili. “kuwa na kiasi hutufundisha kutokutumia kabisa kitu chochote chenye kudhuru na kutumia kwa busara vile vitiavyo afya”.-Patriach and Prophets, uk. 562 [1890]. “uvunjaji wa kanuni za mwili ni uvunjaji wa kanuni za Mungu … kila tendo ambalo linaharibu mwili, akili na uwezo wa kiroho ni dhambi”. – CDF, p. 43. Wanaoutunza Sabato kikamilifu na Amri zote Kumi za Mungu Isaya 56:1-2. ALAMA YA MNYAMA Alama ya mnyama ni kitambulisho cha wale wote waliokataa neema ya Kristo. Wamekataa huruma za Mungu katika maisha yao. Alama ya mnyama ni kinyume cha Muhuri wa Mungu. Alama ya mnyama inatiwa katika paji la uso na katika mkono wa kuume. Hili linaamanisha kuwa wale watakaopokea kwenye paji la uso ni wale waliofanya uchaguzi wao binafsi wa kutomkutii Mungu. Katika mkono wa kuume ni wale ambao wamelazimika kupokea kwa sababu ya hali ya uchumi au ulazimishwaji kwa njia ya mateso. Mama White anasema kuwa: “Chapa ya mnyama ni sabato ya kipapa. (EV 234)…. Wakati wa kupimwa utakapofika, itaonyeshwa dhahiri kile ilicho chapa ya mnyama. Ni utunzaji wa Jumapili” (7BC 980). Je kuna watu ambao wamepokea alama ya mnyama sasa? Jawabu la! Jumapili itakuwa alama ya mnyama mara itakapowekwa kama sheria ya siku ya kuabudu kinyume cha Sabato ya siku ya Saba – Jumamosi! Mama White anasema kuwa: “Utunzaji wa Jumapili bado siyo chapa ya mnyama, na haitakuwa mpaka amri kuu imetolewa ikiwafanya watu kuiabudu sanamu hii ya Sabato. Wakati utafika ambapo siku hii itakuwa ndicho kipimo, lakini wakati huo bado haujafika” (7BC 977; Matukio, uk. 205, 206). “Hakuna mtu yeyote mpaka sasa aliyekwisha kupokea alama ya mnyama” (Ev 234). Ni wakati gani alama ya mnyama itakuwa imepokelewa maishani mwa mtu? Ni pale atakapokuwa amepata ukweli wote juu ya Sabato ya Kweli, kisha akaendelea kukataa hata mara baada ya sheria ya kuabudu siku ya Jumapili itakapokuwa imetangazwa. Mama White anasema, “Wakati utunzaji wa Jumapili utakaposhurutishwa kwa sheria, na ulimwengu utakapokuwa umepata nuru juu ya uwajibikaji wa kutunza Sabato ya kweli, hapo yeyote Yule atakayeasi amri ya Mungu ili aitii kanuni ambayo haina mamlaka ya juu zaidi ya yale ya Roma, atakuwa hivyo anaheshimu upapa zaidi ya Mungu. Anatoa heshima kwa Roma, na kwa mamlaka yanayoshurutisha taasisi iliyoagizwa na Roma. Anaabudu mnyama na sanamu yake.” Matukio, uk. 206, 207. MWITO. Maandalizi ya kupokea muhuri wa Mungu ni tendo ambalo lisilo la bahati nasibu. Maandalizi ya msingi yanachukua maisha mkristo ya kuwa na uzoefu na Mungu wakati wote wa maisha yake. Mungu anatoa wito wake kwetu kuwa kila mmoja wetu azikabidhi njia zake mbele za Bwana ili atuongoze hatua zetu za maisha yetu. Na hatimaye kukimbia ajali kuu inayoujilia ulimwengu wote. Mama White anazungumzia kipindi hiki cha amani tulicho nacho ndicho cha kufanya maandalizi yote ya msingi ya kuachana na dhambi na kudumu katika kweli kwa kusema kuwa: “Kama waumini katika ukweli hawakutegemezwa na imani yao angalau katika siku hizi za amani, ni nini kitakacho waimarisha wakati kipimo kikubwa kitakapokuja na amri kutolewa dhidi ya wale wote ambao hawataabudu sanamu ya mnyama na kupokea chapa yake katika vipaji vya nyuso zao au katika mikono yao? Kipindi hiki kizito hakiko mbali sana. Baada ya kuwa wadhaifu na kutokuwa dhabiti, watu wa Mungu wangepaswa kuwa wanakusanya nguvu na ujasiri kwa ajili ya wakati wa taabu. – 4T 251 (1876). Matukio, uk. 204. “Katika pambano kuu kati ya imani na kutoamini ulimwengu mzima Kikristo utahusika. Wote watachagua upande wa kusimama. Wengine yawezekana hawajishughulishi na upande wowote katika pambano. Waweza wasionekane wakichagua upande kinyume cha ukweli, lakini pia hawatajitokeza kwa ujasiri kwa ajili ya Kristo kwa sababu ya hofu ya kupoteza mali au ya kupatwa na shutuma. Wote hawa wanahesabiwa pamoja na maadui wa Kristo.” RH Feb. 7, 1893. Lazima kila mtu achukue msimamo dhabiti dhidi ya kweli za Mungu: kutii ukweli au kuasi. Mama White anasema tusilee dhambi: “Ngome ya uovu iliyo imara zaidi ya zote katika ulimwengu wetu siyo mdhambi kuishi maisha ya uovu wa kupindukia au maisha ya kujivunjia heshima na kutengwa na jamii bali ni maisha yale ambayo vinginevyo yaonekana kuwa yenye uadilifu, ya heshima ya adili lakini ambayo ndani yake dhambi MOJA inalelewa, uovu MMOJA unaendekezwa …. Kipaji kikubwa na uelekevu, talanta, huruma, ukarimu na matendo ya wema, hivi vyote vyaweza kutumia kama mtego wa Shetani kuwashawishi watu waje kwenye poromoko la uangamivu.” – (Ed. 150; Matukio, uk. 143, 144.) WITO: Tuache kulea na kunyonyesha dhambi yeyote ndani ya kanisa ama familia zetu ili tuweze kupokea mvua ya masika! VITABU VILIVYOTUMIKA KUANDAA MASOMO HAYA NI:- DHIKI KUU INAKUJA LAKINI KUNA TUMAINI: Sura 1 – 15. MATUKIO YA SIKU ZA MWISHO (Toleo la kwanza: Sura 11, 12, 13,15.) VIFUPISHO VYA VITABU VILIVYOTUMIKA 1. AA – The Acts of the Apostles 2. BC – The Seventh-day Adentist Bible Commentary (with Ellen White Comments). 3. CDF – Counsels on Diet and Food 4. CM – Colpoteur Ministry 5. Ed – Education. 6. EV – Evangelism 7. GC – Great Controversy Between Christ and Satan 8. OHC – Our High Calling. 9. T – Testimonies for the Church 10. EW – Early Writtings. 11. FE – Fundamentals of Christian Education. 12. ChS – Christian Service 13. PK - Prophets and Kings 14. PP – Patriachs and Prophets 15. TM – Testimonies to Ministers 16. RH – Review and Herald 17. SM – Selected Messages 18. SP – The Spirit of Prophecy SOMO HILI: LITATUMIKA MAKANISANI NA MAKUNDINI KWA AJILI YA JUMA HILI MAALUMU LA MAOMBI. SABATO YA MWISHO ITAKUWA NI SIKU YA KUFUNGA NA KUOMBA! BWANA AWATANGULIE KATIKA HUDUMA ZOTE NA HUSUSANI MAANDALIZI YA UMWAGWAJI WA MVUA YA MASIKA!
Posted on: Sat, 06 Jul 2013 12:19:31 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015