SHEIKH AZZAN AACHIWA KWA DHAMANA ******************* Jaji Mkuu wa - TopicsExpress



          

SHEIKH AZZAN AACHIWA KWA DHAMANA ******************* Jaji Mkuu wa Zanzibar Othman Omar Makungu leo ametoa dhamana kwa Kiongozi mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho Sheikh Azzan Khalid Hamdan, kwa ajili ya kupatiwa matibabu nchini India, baada ya kulazwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja tangu Septemba mosi mwaka huu. Jaji Mkuu wa Zanzibar ametoa uamuzi huo wa kumpatia Sheikh Azzan dhamana, baada ya kupokea maombi kutoka kwa mawakili wa upande wa utetezi, wakiongozwa na Salum Tawfiq. Tawfiq ameiomba Mahakama Kuu ya Zanzibar impatie dhamana Sheikh Azzan, ili aweze kwenda kutibiwa nchini India, kama ilivyoelezwa na ripoti ya madaktari wa hospitali ya Mnazi Mmoja, ambayo imekiri kuwa maradhi ya kiongozi huyo hayatibiki hapa nchini na hivyo kutakiwa kutibiwa nje ya nchi. Baada ya kuwasilisha maombi hayo na kuambatanisha na ripoti ya daktari pamoja na baadhi ya nyaraka nyingine muhimu, upande wa mashtaka umeeleza kutokuwa na pingamizi dhidi ya maombi hayo hasa kwa kuzingatia kuwa pamoja na kuwa ni mstakiwa, ana haki ya kuishi kwa mujibu wa katiba. Katika uamuzi wake, Jaji Mkuu Makungu ametaka Sheikh Azzan Khalid Hamdan aachiliwe kutoka katika mikono ya askari wa Magereza ili aweze kwenda kutibiwa nchini India, ndugu wawili wa kiongozi huyo wamchukulie dhamana na kuhakikisha anarejea nchini mara baada ya kupatiwa matibabu pamoja na kuzingatia ushauri wa daktari utakaotolewa baada ya matibabu hayo. Hata hivyo, Wakili Tawfiq amesema safari pamoja na matibabu yatagharamiwa na familia ya Sheikh Azzan, baada ya kukamilisha kwa taratibu zote za kisheria. Sheikh Azzan pamoja na wenzake tisa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 9 ya uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali za umma, ambapo hadi hivi sasa viongozi wako mahabusu, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim kufunga dhamana zao kwa maslahi ya Taifa.
Posted on: Fri, 27 Sep 2013 13:17:11 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015